Yafuatayo ni maelezo ya Mchungaji John Mulinde:
Napenda nikushirikishe
ushuhuda wa kijana mmoja ambaye aliokoka; kijana ambaye alikuwa akimtumikia
ibilisi. Na mtu yule alipotoa ushuhuda wake, ulinitia changamoto kubwa sana.
Sikutaka kuamini. Ilinibidi nifunge kwa muda wa siku kumi mbele za Bwana, huku
nikimuuliza, "Bwana, hivi mambo haya ni kweli?" Na ilikuwa ni
katika wakati huo ndipo Bwana alipoanza kunifundisha kile kinachotokea kwenye
ulimwengu wa roho pale tunapoomba.
Kijana huyu alizaliwa
baada ya wazazi wake kuwa wamejiweka wakfu wao wenyewe kwa lusifa. Wakati bado
akiwa tumboni, walifanya matambiko mengi na kumweka wakfu awe mtumishi wa
lusifa. Alipozaliwa na kufikisha miaka minne, tayari alianza kutumia nguvu zake
za kiroho. Hata wazazi wake walianza kumwogopa! Akiwa na miaka sita, baba yake
alimkabidhi kwa wachawi ili akapatiwe mafunzo. Na akiwa na miaka kumi, alikuwa
akifanya mambo makubwa katika ufalme wa ibilisi. Alikuwa akiogopwa hata na
wachawi wa kawaida.
Alikuwa bado ni kijana
mdogo, lakini mambo aliyokuwa anafanya yalikuwa ni mabaya mno. Alikua hadi kufikia
miaka ya ishirini akiwa na damu nyingi ya watu mikononi mwake. Aliua watu kila
alipotaka. Alikuwa na uwezo wa kutoka nje ya mwili wake kupitia taamuli ya
kinjozi (transcendental meditation), yaani kitendo cha kutuliza mawazo na mwili
kama wafanyayo Wahindukatika yoga. Tazama mfano HAPA.
Katika huko kutaamuli, angeweza hata kunyanyuka kimwili kutoka ardhini pale
alipokaa na kuelea hewani (levitate). Tazama mfano HAPA. Wakati
mwingine aliweza kutoka nje ya mwili; akauacha mwili wake na kwenda nje huko na
kule kufanya mambo mbalimbali (astro-travelling). Na kijana huyu
alitumiwa na shetani kuharibu makanisa mengi; na kuwaharibu wachungaji wengi.
Siku moja, alipangiwa
kwenda kuharibu kanisa moja ambalo lilikuwa na maombi ya kutosha. Kulitokea na
migawanyiko mingi kanisani na kuchanganyikiwa kwingi. Alianza kufanya kazi kwenye
kanisa hili; lakini mchungaji wa kanisa lile aliitisha mfungo wa kanisa zima.
Kanisa lilipoanza kufunga, watu walitubu sana na kufanya mapatano mengi. Na
watu wakawa kitu kimoja, na wakaanza kuomba kwa ajili ya kazi ya Bwana katikati
yao. Na wakaendelea kufanya maombezi na kumlilia Mungu ili awarehemu na
kuingilia kati maishani mwao. Na kadiri siku zilivyoendelea, bwana huyu alikuwa
akija tena na tena akiwa na mapepo kinyume na kanisa hili. Lakini lilitoka neno
la kinabii likiwaambia Wakristo wasimame pamoja na kufanya vita dhidi ya nguvu
za giza ambazo zilikuwa zinashambulia kanisa lile.
Siku moja, kijana huyu
aliuacha tena mwili wake chumbani kwake na akatoka nje. Aliongoza jeshi kubwa
la mapepo moja kwa moja hadi kwenye kanisa lile ili kwenda kufanya vita vya
kiroho.
Sasa, ufuatao ni ushuhuda
wake.
Roho yake ilikuwa inapaa
hewani juu ya kanisa lile na kujaribu kulishambulia, lakini kulikuwa na kifuniko
cha nuru juu ya kanisa hilo. Wakati waliendelea na mapambano, ghafla, kulikuja
jeshi la malaika ambalo liliwashambulia na kukawa na mapambano makali pale
hewani. Hatimaye, mapepo yalikimbia, lakini yeye alikamatwa na wale
malaika.
Ndiyo, alikamatwa na
malaika! Alijiona akiwa ameshikiliwa na malaika sita. Na wakamleta kwa
kumpitisha kwenye paa hadi kwenye madhabahu ya kanisa. Akawa yuko pale huku
watu wanaendelea kuomba. Walikuwa wamezama kwenye maombi, wakifanya vita vya
kiroho; wakifunga na kuvunja, na kutupa nje. Mchungaji alikuwa kwenye madhabahu
akiongoza maombi hayo na vita. Roho wa Bwana akaongea na mchungaji, akisema, "Nira
imevunjika, na mhusika yuko hapa mbele yako. Msaidie kwa kumfungua."
Mchungaji alipofungua
macho yake, alimwona yule kijana akiwa ameanguka pale hajitambui. Mwili wake ulikuwa
pamoja naye! Kijana yule anasema kuwa haelewi ni kwa vipi mwili wake uliungana
naye; maana alikuwa ameuacha nyumbani. Lakini ndio alikuwa pale; hajui ni kwa
vipi aliingia, isipokuwa tu malaika walimpitishia kwenye paa.
Sasa, mambo haya ni magumu
kuamini, lakini mchungaji alinyamazisha kanisa na kuwaambia kile ambacho Bwana
alimwambia. Kisha akamwuliza yule kijana, "Wewe ni nani?" Kijana
yule alikuwa anatetemeka wakati mapepo yalipoanza kumtoka.
Kwa hiyo, waliomba kwa
ajili ya kufunguliwa kwake, na hatimaye baadaye alianza kusema ushuhuda wake.
Hivi sasa kijana huyu ameshaingia kwa Bwana na ni mwinjilisti, akihubiri
Injili. Anatumiwa sana na Bwana kuwaweka huru watu wengine.
Usiku mmoja, mimi (John
Mulinde) nilienda kwenye chakula cha usiku mahali fulani. Sababu hasa ya kwenda
pale ni kwa vile kuna mtu alinieleza habari za huyo kijana; na nilikuwa na
shauku kubwa sana ya kumwona, na kuona kama kweli hadithi yake ina ukweli
wowote. Kwa hiyo, nilipofika, nilikaa mezani. Na jioni ile, kijana huyu alipewa
nafasi ya kutoa ushuhuda wake. Alizungumza juu ya mambo mengi sana. Mara
nyingine alilia kutokana na mambo aliyoyafanya. Alipomaliza kusema, alitoa
ombi.
Kulikuwako na wachungaji
wengi pale kwenye ukumbi. Alisema, "Ninawaomba ninyi, wachungaji. Tafadhalini,
wafundisheni watu namna ya kuomba.” Watu
ambao hawaombi, wanaweza kuchukuliwa na chochote, katika chochote na ibilisi;
na ziko hata njia za adui za kutumia maisha yao na maombi yao. Adui anajua hata
namna ya kutumia kwa faida yake maombi ya watu wasiojua kuomba. "Wafundisheni
watu namna ya kutumia silaha za kiroho ambazo Mungu amezitoa."
Kisha alieleza jinsi
ambavyo alikuwa akiongoza mapambano kwenye anga. Alikuwa akienda pamoja na
maajenti wengine wa shetani na mapepo mengi hadi angani. Ilikuwa kama zamu.
Inabidi kwenda kutekeleza zamu yako. Kwa hiyo, ni mara nyingi tu alikuwa na
muda wa kwenda kwenye anga ili kufanya vita. Na akasema kuwa kule angani,
kwenye ulimwengu wa roho, kama anga limefunikwa na blangeti la giza, blangeti
hilo linakuwa ni nene sana; na ni kama jiwe. Na linakuwa limefunika eneo lote.
Na mapepo haya yanaweza kwenda juu yake na chini yake. Na yakiwa huko, yanaweza
kuathiri matukio yanayoendelea duniani.
Pale mapepo wachafu pamoja
na maajenti wa shetani wa kibinadamu wanapomaliza zamu yao, wanashuka duniani
kwenye maeneo ya kimaagano, iwe ni kwenye maji au ardhini, ili kuweza kurejesha
upya nguvu zao, maana zinakuwa zimepungua kutokana na kufanya kazi angani
wakati wa zamu yao. Na wanarejeshaje nguvu zao? Ni kupitia kafara ambazo watu
wanatoa kwenye madhabahu hizi. Kafara zinaweza kuwa ni uchawi wa wazi, damu za
aina zote, ikiwa ni pamoja na utoaji mimba, vita, na utoaji wa kafara za
wanadamu na wanyama. Zinaweza pia kuwa ni kafara za uzinzi, pale ambapo watu
wanafanya uzinzi na uashetati wa kila aina. Na matendo haya maovu yanaleta nguvu
kwenye ulimwengu wa giza. Na ziko aina nyingi za kafara.
Kijana huyo alisema kuwa,
maajenti wa shetani wanapokuwa juu kwenye anga, na Wakristo wakaanza kuomba
hapa duniani, maombi ya Wakristo huonekana kwa namna tatu. Maombi yote
huonekana kama moshi ambao unapaa kuelekea mbinguni.
Baadhi ya maombi huonekana
kama moshi, na yanaenda juu kiasi na kupotelea hewani. Maombi ya aina hii
hutoka kwa watu ambao wana dhambi maishani mwao na hawako tayari kushughulika
nazo. Maombi yao ni dhaifu sana, kiasi kwamba yanapeperushwa na kupotelea
angani.
nyingine ya maombi nayo ni
kama moshi ambao unainuka juu hadi unapofikia kwenye ule mwamba, lakini hayana
nguvu ya kupenya mwamba huo. Kwa kawaida, hawa ni watu ambao hujaribu
kujitakasa, lakini hawana imani juu ya kile ambacho wanakifanya pale wanapoomba,
yaani wanaomba lakini moyoni hawana ujasiri kwamba kile wanachokiomba
watakipokea. Mara nyingi huwa wanapuuzia mambo mengine ya muhimu yanayotakiwa
wakati mtu anapoomba.
Aina ya tatu ya maombi ni
kama moshi ambao umejaa moto. Yanapokuwa yanapaa, yanakuwa ni ya moto sana
kiasi kwamba yanapoufikia ule mwamba, unaanza kuyeyuka kama nta. Yanapenya
mwamba huo na kuendelea hadi juu.
Mara nyingi watu
wanapoanza kuomba, maombi yao huonekana kama aina ya kwanza ya maombi. Lakini
kadiri wanavyoendelea kuzama, yanageuka na kuwa ya aina ya pili. Na wakiendelea
zaidi, ghafla yanalipuka moto. Na maombi hayo yanakuwa yana nguvu sana kiasi
kwamba yanapenya kabisa ule mwamba.
Mara nyingi maajenti wa
uovu hubaini kwamba kuna maombi yanabadilika na kuelekea kwenye kuwa moto.
Kisha huwasiliana na viumbe vingine vilivyoko duniani na kuwaambia, "Mvurugieni mtu huyo maombi! Mfanyeni aache
kuomba! Mwondoeni kwenye maombi!"
Mara nyingi Wakristo
hushindwa na mbinu hizi. Wanakuwa wanaomba kwa nguvu; wanatubu; wanaruhusu Neno
kukagua nafsi zao; imani inaanza kujengeka. Maombi yao yanaanza kuwa na shabaha
zaidi. Kisha ibilisi anaona kuwa maombi yao yanaanza kukusanya nguvu. Ndipo vurugu
zinaanza ili kuharibu maombi hayo. Mara simu inalia. Wakati mwingine, katikati
ya maombi ambapo mtu alikuwa amezama kabisa, , simu inaweza kulia na unawaza
kuwa, ngoja niende nikaipokee kisha nitarudi kuendelea na maombi.
Mbinu zingine za kuvuruga
maombi nazo zinaweza kutumika; hata kama ni kukugusa mwili wako na kuleta
maumivu mahali fulani. Hata pia kukufanya ujisikie njaa ambapo utajisikia kwenda
jikoni kutengeneza japo chakula kidogo. Ilimradi tu wakiweza kukufanya utoke
mahali pale, wanakuwa wameshakushinda. Wachungaji, ni lazima muwafundishe watu
jinsi ya kuomba. Tengeni muda, si tu kwa ajili ya maombi ya juujuu. Mara moja
kwa siku, Wakristo wanatakiwa kuwa na muda wa kujielekeza kwa moyo wote kwa
Mungu, bila kuwapo kwa kitu chochote cha kuwaharibia umakini wao.
Na kama watu waking’ang’ana
kabisa kwa njia hii ya maombi na kuruhusu kupata mwongozo wa kiroho, kisha
wakawa wanaendelea na kuendelea, lazima kitu kitatokea rohoni. Moto utalipuka
na kugusa ule mwamba na kuuyeyusha! Kuyeyuka kunapoanza, ni moto sana kiasi
kwamba hakuna pepo ambaye anaweza kustahimili. Wala hakuna roho ya mwanadamu inayoweza
kustahimili pia. Wote wanakimbia.
Kama mtu atajitoa kuomba
kwa bidii na kwa kumaanisha namna hiyo, hatimaye kutafuata kufunguka kwa
ulimwengu wa roho. Na mara hili linapotokea, matatizo yote haya katika maombi
yanafikia mwisho! [Yaani ule ugumu na ule uzito unakwishilia mbali!] Yule
ambaye anakuwa anaomba duniani anakuwa sasa anajisikia kuwa maombi ni kitu kilaini
kabisa, cha kuburudisha, na chenye nguvu.
Na nimegundua kuwa wakati
huo, huwa tunapoteza kabisa hisia za muda na mambo mengine. Si kwamba tunakosa
mpangilio; la hasha! Mungu anakuwa anashughulika na muda wetu. Lakini inakuwa
ni kama unaachilia kila kitu, na unaunganishwa moja kwa moja na Mungu. Maombi
yako yanapopenya, kunakuwa hakuna kizuizi tena kuanzia hapo; na mtu anayeomba
anaweza kuendelea kwa muda mrefu kama apendavyo. Hakuna kabisa kizuizi.
Na mara anapomaliza
kuomba, lile tundu linabakia wazi.
Kijana huyu pia alisema
kuwa, watu wa namna hii wanapomaliza kuomba na kuondoka mahali hapo, lile tundu
linakuwa linaondoka pamoja nao. Wanakuwa hawaenendi tena chini ya lile blangeti
la jiwe. Wanakuwa wanaenenda chini ya mbingu zilizo wazi. Na akasema kwamba,
katika hali hiyo, ibilisi hawezi kufanya kile anachokitaka kwao. Na uwepo wa
Mungu unakuwa kama nguzo kutoka mbinguni ikiwa iko juu ya maisha yao.
Wanalindwa; na kunakuwa na nguvu kubwa sana ndani ya hiyo nguzo kiasi kwamba
kadiri wanavyotembea huku na kule, uwepo huo unakuwa unagusa hata watu wengine.
Nguzo hiyo inakuwa inatambua kile ambacho adui amefanya kwa watu wengine. Na pale
watakatifu hao wanapozungumza na watu wengine, na wale watu wakawa wamesimama
nao, wanaingia ndani ya nguzo hiyo. Na mradi tu wakiwa ndani ya ile nguzo, vifungo
vyote vya adui vinadhoofika.
Kwa hiyo, watu hawa wenye
mpenyo huu wa kiroho wanapowashuhudia wenye dhambi habari za Yesu Kristo,
upinzani wa wenye dhambi unakuwa wa chini. Ni rahisi kuwaleta wenye dhambi kwa
Kristo. Wanapoomba kwa ajili ya wagonjwa, au kwa ajili ya mambo mengine, maombi
yao yanakuwa na nguvu sana.
Na kama kuna sehemu ambako
maombi ya namna hii huombwa mara kwa mara, uwepo wa Mungu unakuja mahali pale
na hauondoki. Hivyo, hata watu wasiomjua Mungu wanapokuja kwenye sehemu kama
hizo, ghafla vifungo vyao vinakatika.
Na kama atatokea mtu wa
kusema nao kwa uvumilivu na kwa upendo, wanaweza kugeuka haraka sana; si kwa
nguvu au kwa uwezo, bali ni kwa Roho wa Mungu, ambaye anakuwa yuko pale. Na
kama hakuna mtu atakayewajali watu hawa, wanakuja kwenye uwepo wake na
kujisikia hatia, wanaanza kujadili kama wakubali au la. Pale watakapoondoka,
vifungo vinakuwa na nguvu zaidi kwao. Na ibilisi anajihadi kwa kila njia
kutowaruhusu kurudi tena kwenye sehemu kama hizo.
Je, shetani anakaa kimya tu baada ya mtu kupata mpenyo?
Kijana huyu alisema kuwa,
ibilisi anawachukia sana watu wa namna hiyo, yaani wale waliopata mpenyo wa
maombi.
Sasa unaweza kupiga picha,
sote tulikuwa tumekaa chini tunamwangalia kijana huyu akieleza ushuhuda wake.
Alikuwa anatueleza mambo ambayo yeye mwenyewe alikuwa akiyafanya na
aliyoyashuhudia kwa macho yake. Alitueleza kile ambacho walifanya kwa watu
ambao walipata mpenyo katika maombi. Alisema kuwa waliwaweka akilini sana watu
kama hao. Kisha waliwafuatilia sana na kujifunza kuhusu wao ili kuwajua vizuri.
Walitafuta kila kitu kuwahusu. Hivyo, walifahamu udhaifu wao wote, na ikitokea
mtu akawashinda kwenye maombi na kupenya, wanawasiliana na wengine kwenye
ulimwengu wa giza na kusema, "Mumlenge
mtu huyu kwenye eneo hili na hili. Udhaifu wake uko hapa na hapa."
Kwa kuwa mtu wa aina hii
anapotoka nje ya kifuniko cha maombi, roho ya maombi inakuwa juu yake, uwepo wa
Mungu upo juu yake, roho yake inakuwa iko juu, na furaha ya Bwana ndiyo nguvu
zake; anapokuwa anaenda, adui anajaribu kila njia kuleta yale mambo ambayo
yatamvuruga ili asielekeze macho yake kwa Bwana.
Kama, kwa mfano,
imeshajulikana kuwa udhaifu wake uko kwenye eneo la hasira, basi adui atasababisha
watu watende mambo ambayo yatamfanya akasirike. Na kama hayuko makini
kumsikiliza Roho Mtakatifu, na akaingiwa na hasira, basi ataondoa macho yake
kwa Bwana. Na anapokuwa na hasira hivyo, ghadhabu zinamjaa. Baadaye anapokuja
kujirudi, anakuwa anataka kutupilia mbali hali hiyo na kuendelea na furaha ya
Bwana, lakini anajikuta hajisikii tena ile furaha kama mwanzo. Anajitahidi
kujisikia vizuri tena; lakini haiwezekani tena. Kwa nini? Alipojiachilia kwenye
kishawishi cha hasira, mapepo walifanya bidii zote katika muda huo kufunga lile
tundu kule juu. Na mara waliporudishia lile jiwe, uwepo wa Bwana unakuwa
umekatika, yaani ile nguzo iliyokuwa inatokea mbinguni na kumfunika inakuwa
haimfikii tena!
Mtu huyo hataacha kuwa
mwana wa Mungu. Lakini ule upako wa ziada uliokuwa unaandamana naye maishani;
ule uwepo uliokuwa ukitenda mambo bila yeye kutumia nguvu zozote, unakuwa
umekatika! Maana pepo wachafu wanatafuta uliko udhaifu wako.
Kama udhaifu wa mtu ni
kwenye masuala ya mapenzi, adui ataandaa watu, matukio, na mambo ambayo
yatainua hisia za mtu huyo za tamaa ya kimapenzi. Na kama mtu huyo atazikubalia
hizo tamaa na kufungua akili yake kuyapokea mambo hayo, na kuyalea nafsini
mwake, pale anapomaliza kila kitu na kutaka kurejea tena kwenye hali ya upako
ili asonge mbele, anakuta kwamba ule uwepo haupo tena. Labda unasema, “Hii si
vizuri kabisa.” Kumbuka tu Biblia inasemaje, "
Tena ipokeeni chapeo ya wokovu. Vaeni dirii ya haki." Mara nyingi hatuoni haja ya silaha hizi za kivita. Lakini
kumbuka Yesu alivyotuambia juu ya namna ya kuomba "Usitutie majaribuni,
lakini utuokoe na yule mwovu."
Kila mara unapopata mpenyo
katika maombi, unapofika mwisho, kumbuka kuwa wewe bado ni kiumbe mwanadamu
aliye dhaifu. Kumbuka kuwa haujakamilishwa bado. Mwombe Bwana, useme, "Bwana,
nimefurahia wasaa huu wa maombi, lakini nitakapotoka nje kwenye dunia,
usiniongoze kwenye majaribu. Usiruhusu niangukie kwenye mtego wa ibilisi. Najua
kuwa adui anatega mitego kule nje. Sijui ni mitego ya namna gani. Na ninajua
kuwa bado mimi ni dhaifu katika baadhi ya maeneo. Kama nikiingia kwenye hali
fulanifulani, nitaanguka. Unilinde, Bwana. Unapoona ninaelekea kule ambako kuna
mitego niliyotegewa, nifanye nielekee upande mwingine. Uingilie kati, Ee,
Bwana. Usiche niende tu kwa nguvu zangu na uwezo wangu. Niokoe na yule mwovu.”
Mungu anaweza kufanya
hivyo. Lakini, kama kuna kitu kibaya kitatokea, ambacho kitakufanya uondoe
macho yako kwa Kristo, wewe sema tu, “Asante Yesu.” Ndiyo sababu Mtume Paulo
aliandika, “Mshukuruni Mungu kwa kila jambo.” Baadhi ya mambo si mazuri.
Yanaumiza, na tunashangaa kwa nini Mungu anayaruhusu yatufikie. Lakini kama tu
tungejua kwa njia hiyo anatuokoa na mambo yapi,
tungemshukuru. Tukijifunza kumwamini Bwana, tutamshukuru kwa kila jambo.
Yule kijana aliendelea kusema
kuwa, unapopata mpenyo katika maombi, majibu yako ni lazima yatakuja. Alisema kuwa jibu mara zote huja, lakini mara
nyingi, huwa halifiki kwa mtu aliyeliomba. Kwa nini? Ni kwa sababu ya mapambano
yaliyoko kwenye anga. Pia, majibu yanaweza kuzuiliwa iwapo viumbe waovu wa
rohoni watafanikiwa kurejesha ule mwamba na kuziba tundu ambalo mwombaji alifanikiwa
kulitoboa kwa njia ya maombi yake.
Kisha aliongea jambo
ambalo kwa kweli lilitikisa imani yangu. Binafsi ilinibidi niingie kwenye
mfungo wa siku kumi, ili kumwuliza Bwana kama hilo alilosema lilikuwa na ukweli
wowote. Basi sikiliza haya: Kijana huyu alisema kuwa, kila Mkristo anaye
malaika ambaye anamtumikia Mkristo huyo. Nasi tunafahamu kuwa Biblia inasema
kuwa malaika ni roho wanaotutumikia. (Waebrania 1:14). Alisema kuwa watu
wanapoomba, majibu huletwa kwa mikono ya malaika. Malaika huleta majibu, kama
ambavyo tunasoma kwenye kitabu cha Danieli. Kisha alisema jambo ambalo ni gumu
sana. Alisema kwamba, kama yule anayeomba anafahamu silaha za kiroho na
amejivika silaha hizo, majibu nayo huja kwa kupitia malaika ambaye, naye
amejivika kikamilifu kwa silaha hizohizo.
Lakini, kama anayeomba
hajali silaha za kiroho, basi malaika nao wanakuja bila silaha hizo. Wakristo
ambao hawajali kile ambacho kinaingia mawazoni mwao; hawashindani kuangusha
mawazo yasiyofaa; malaika wao huja bila chapeo. Silaha zozote utakazoacha kuzitilia
maanani duniani, malaika anayekutumikia naye anakuwa hanazo. Kwa maneno
mengine, silaha zetu za kiroho hazitulindi miili yetu, bali zinalinda vitu vile
vya kiroho tunavyofanikiwa kuvipata kutoka kwa Bwana.
Malaika anapokuwa anakuja,
mapepo wanamtazama na kumkagua na kubaini maeneo ambayo hajajifunika; na hayo
ndiyo maeneo ambayo watashambulia. Kama hana chapeo kichwani, basi
watashambulia kichwani. Kama hana dirii, watashambulia kifuani. Kama hana
viatu, watajaribu kutengeneza moto ili kumwunguza miguuni.
Sasa, najua kuwa hili ni
gumu kuamini; mimi narudia tu kile ambacho kijana huyu alisema. Kisha
tulimwuliza, “Je, malaika wanaweza kuungua moto?” Na unajua alisema nini?
Kumbuka kuwa huu ni ulimwengu wa roho. Hizi ni roho kwa roho zinapambana.
Mapambano ni makali sana, na pale wanapomshinda malaika wa Mungu, jambo la
kwanza wanalokimbilia ni lile jibu alilobeba; na wanalichukua hilo. Na hizi zinakuwa
ni zawadi ambazo hutolewa kwa watu kupitia imani za siri, au uchawi.
Kumbuka kile ambacho
Biblia inasema kupitia kitabu cha Yakobo. Vipawa vyote vyema hutoka kwa Mungu
(Yakobo 1:17). Kwa hiyo, shetani anapata wapi vitu vizuri anavyowapatia watu?
Baadhi ya watu ambao hawawezi kupata watoto, huenda kwa wachawi na waabudu
shetani, na wanapata mimba! Mtoto anakuwa ametoka wapi? Je, shetani ni
muumbaji? HAPANA! Anaiba kutoka kwa watu ambao hawaombi maombi yao hadi mwisho.
Katika Biblia, Yesu alisema,
"Ombeni bila kukoma." Pia alisema, "atakapokuja
Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? " Je, Yesu atakukuta bado unangojea? Au utakata tamaa na kumwacha
adui aibe kile ambacho umekuwa ukikiombea?
Na hawaridhiki tu na kuiba
jibu la maombi. Wanataka pia kumweka malaika kifungoni. Na wanaanza kupambana
naye. Wakati mwingine wanafanikiwa kumkamata na kumfunga malaika. Inapotokea
hivyo, Mkristo anakuwa kama chakula chao duniani. Wanaweza kumfanyia chochote
maana hana ulinzi tena kwenye ulimwengu wa roho.
Nilimwuliza kijana huyo,
“Una maana kuwa malaika anaweza kushikiliwa katika ulimwengu wa giza?” Sasa
alikuwa anaeleza uzoefu wake, na akasema, hawatamshikilia malaika kwa muda
mrefu kwa sababu ya Wakristo wengine ambao wanaomba mahali pengine. Jeshi la
ziada litatumwa, na malaika atakuwa huru. Na kama yule Mkristo anayehusika
hajaomba hadi kwenye mpenyo, basi atabakia mateka. Ndipo shetani atatuma
malaika wake na malaika wa nuru kwa mtu
huyu, na hapo ndipo uongo na udanganyifu unapotokea; maono ya uongo na unabii
wa uongo. Uongozi wa uongo, na kufanya kila aina ya maamuzi mabaya. Na mara
nyingi, mtu wa namna hii anaweza kupata mashambulizi na vifungo vya kila aina.
Niliondoka kwenye kile
chakula cha jioni huku na mawazo mengi sana. Nikasema, “Bwana, sitaki hata
kujaribu kuamini jambo hili.” Linaondoa ujasiri na usalama wangu wote!
Nilipoenda kumlingana Bwana, ilikuwa ni kwa siku kumi; na Bwana alifanya mambo
mawili. Kwanza, si tu kwamba alithibitisha mambo hayo niliyoyasikia kutoka kwa
yule kijana, bali pia alifungua akili zangu zaidi ili kuona mambo mengine mengi
zaidi ya yale ambayo niliyasikia. Pili, aliniongoza kuona kile ambacho
tunatakiwa kukifanya wakati mambo haya yanapotokea ili tuweze kuwa washindi.
Alinipa mambo matatu:
Moja: namna ya kutumia silaha za vita vyetu vya kiroho.
Biblia inaziita silaha za Mungu. Si silaha zetu. Tunapozitumia, tunamruhusu
Mungu kupigana kwa niaba yetu.
Mbili: tambua uhusiano wa roho zinazotutumikia, yaani
malaika, na maisha yetu ya kiroho. Na ni lazima kuwa makini sana na kile
kinachotokea mioyoni mwetu; kama mwongozo wa kile ambacho kinatakiwa kutokea
rohoni kutuhusu sisi.
Tatu: ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hatakiwi kuja
kama mtumishi wetu, kututumikia na kutuletea vitu mbalimbali. Hakimbiikimbii
kwa Baba kumweleza kile ambacho tunataka. Hiyo ni kazi ya malaika. Lakini Yeye
husimama pamoja nasi. Anafanya nini? Anatuongoza, anatufundisha, anatutangulia,
anatusaidia kuomba inavyotakiwa. Na mambo haya yanapotokea kwenye ulimwengu wa
roho, anatuambia. Wakati mwingine anakuamsha usiku na kukwambia, “Omba.” Wewe
unasema, “Hapana! Muda wangu haujafika.” Na anasema, “Omba sasa!” Kwa nini
inakuwa hivyo? Ni kwa sababu Yeye anaona kila kinachoendelea kwenye ulimwengu
wa roho. Wakati mwingine anasema, “Kesho ni kufunga.” Wewe unasema, “Hapana,
nitaanza Jumatatu!”
Lakini kumbuka kuwa Yeye
anaelewa kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Ni lazima tujifunze kuwa
makini na Roho Mtakatifu. Anatuongoza kwenye njia za haki. Wapendwa, tuishie
hapa. Labda wakati mwingine tutaongea jinsi ambavyo tunaweza kuomba hadi kupata
mpenyo, maana sasa tunajua mapambano yaliyoko rohoni na jinsi ya kupenya; na namna
tunavyoweza kudumu tukiwa na mpenyo tuliopata. Na mara tunapojifunza hili,
linakuwa ni jambo la furaha sana. Tukumbuke tu jambo moja: vita si vyetu, bali
ni vya Bwana! Haleluya!
Hebu tusimame. Mwangalie
mwenzio machoni na utafakari ni mara ngapi amekosa kile ambacho Mungu
alikiandaa kwa ajili yake. Lakini shikaneni mikono kama inawezekana; watu wawili
au watatu, kisha tu muambiane, “Hakuna haja ya kushindwa tena! Tunaweza
kushinda! Iko nguvu ya kutosha kushinda! Yesu tayari ameshafanya kazi yote.”
Muombeane ninyi kwa ninyi ili Bwana aweze kutusaidia kushinda. Hatutakiwi
kushindwa. Iko neema ya kutosha; nguvu ya kutosha kuleta ushindi!
Asante Yesu.
**********************
Unaweza pia kusoma
ushuhuda huu kwa Kiingereza (pamoja na shuhuda zingine) kwa kubofya HAPA.
Usikate tamaa. Simama
imara katika imani. Unaweza kushinda. Bwana si dhalimu; anakupenda na amekuwa akijibu
maombi yako siku zote. Je, Biblia si inasema kuwa KILA aombaye hupokea? (Mathayo
7:8). Na kwamba Mungu si mwanadamu hata aseme uongo (Hesabu 23:19).
Tumia mafunzo haya
kusonga mbele katika wokovu na imani yako. Bwana Yesu akubariki sana.
Toa Maoni Hapa Chini