MUGABE ASHINDA UCHAGUZI WA ZIMBABWE
By Apostle Damacy
|
Ndugu Robert Mugabe, Rais wa Zimbabwe. |
RAIS wa Zimbabwe Robert
Mugabe ameshinda uchaguzi wa rais, baada ya kupata asilimia 61.9 ya
kura. Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai ni wa pili na asilimia 33.9 ya kura
Kiongozi wa upinzani
Morgan Tsvangirai ameueleza uchaguzi huo kuwa ni wa bandia na
udanganyifu mkubwa na chama chake cha Movement for Democratic Change
(MDC) kimeapa kutokubali matokeo, hali inayozusha hofu ya kurejewa kwa
ghasia zilizomwaga damu ambazo zilitokea baada ya uchaguzi wa mwaka
2008.
Katibu mkuu wa Umoja wa
Mataifa Ban Ki-moon amezitaka pande zote mbili "kutoa ujumbe wa wazi wa
utulivu" kwa wafuasi wao wakati hali ya wasi wasi ikiongezeka.
Ban ana matumaini kuwa
hali hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa shwari na ya amani katika
siku ya uchaguzi , itaendelea wakati wa zoezi la kuhesabu kura na hata
baada ya kukamilika zoezi hilo," amesema msemaji wa katibu mkuu Martin
Nesirky.
|
Ndugu Morgan Tsvangirai. |
Jumuiya ya maendeleo
kusini mwa Afrika SADC ambayo ina ushawishi mkubwa pia imewataka
"Wazimbabwe wote kuwa na uvumilivu,na utulivu."
Macho yote sasa
yanaelekezwa kwa chama cha MDC ambacho kilitarajiwa kutoa taarifa yake
leo Jumamosi (03.08.2013) kufuatia mkutano wao wa siku mbili.
Kabla ya mkutano huo ,
afisa wa ngazi ya juu wa MDC Roy Bennett alitoa wito wa kampeni ya
upinzani wa chini kwa chini, akiwataka watu "kuifikisha nchi hiyo katika
hali ya kutoweza kufanya lolote".
Waangalizi wanaonekana kutofautiana kuhusiana na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa.
Mkuu wa ujumbe wa
uangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika , Olusegun Obasanjo , amesema
muda mfupi baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa kuwa uchaguzi huo
umekuwa wa "amani , uliofuata utaratibu, huru na wa haki".
SADC imeshindwa kuutangaza uchaguzi huo kuwa wa "haki" lakini imesema ulikuwa " huru na wa amani".
"Tumesema uchaguzi huu
ulikuwa huru, kwa hakika ulikuwa huru," amesema kiongozi wa kundi la
uangalizi la SADC Bernard Membe. "Hatujasema ulikuwa wa haki...
hatukutaka kutoa maamuzi katika wakati huu."
Membe alikutana na Mugabe
siku ya Ijumaa, "kumtakia kila la kheri wakati akijitayarisha na hatua
ya kuapishwa," aliwaambia baadaye waandishi habari.
SADC ilijadili kuundwa
kwa serikali ya kugawana madaraka baada ya uchaguzi uliomwaga damu wa
mwaka 2008. Kukiwa na waangalizi 600 katika uchaguzi huo, uamuzi wao na
hatua inayofuata itaangaliwa kwa karibu na mataifa ya magharibi ambayo
yamekataliwa kuangalia uchaguzi huo.
Hata hivyo wanadiplomasia
wa mataifa ya kigeni wameueleza uchaguzi huo kuwa umeendewa kinyume
kimsingi na mtandao wa usaidizi wa uchaguzi nchini Zimbabwe umeripoti
kuwa zaidi ya wapiga kura milioni moja walizuiwa kupiga kura katika
maeneo ambayo ni ngome kuu ya Tvangirai. Lakini imesisitiza kuwa wasi
wasi ambao umeelezwa kuhusiana na maeneo fulani ya hatua za uchaguzi
yanapaswa kufuatiliwa kupitia njia sahihi za utaratibu wa kisheria.
Toa Maoni Hapa Chini