Askofu Mkuu Dk. Barnabas Mtokambali,Roho ya Mpinga Kristo imeingia Tanzania
Kanisa la Tanzania limeitwa kusimama imara na kuchagua njia salama ya
kuelekea, wakati huu ambao roho ya Mpinga Kristo imeingia nchini na
kusababisha mateso makali, na hata mauaji ya watu wasio na hatia.
Katika
hotuba yake kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Idara ya Maandiko na
Uanafunzi, ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Askofu Mkuu wa
Kanisa hilo, Dk. Barnabas Mtokambali alisema kuwa, kwa sasa roho ya
Mpinga Kristo inatenda kazi nchini na ndiyo iliyosababisha Watanzania
kuingia katika orodha ya wale wanaoteswa duniani.
“Hii si mara ya
kwanza, kanisa la kwanza liliwahi kuingia katika mateso makali na
maangamizi, ukisoma Biblia katika kitabu cha Matendo ya Mitume, unaona
hatua kadhaa za kanisa lilipopitia katika mateso na hatua ambazo
lilichukua hata kuishinda,” alisema kiongozi huyo.
Akichukua
tahadhari kubwa, Dk. Mtokambali alisema kuwa, roho ya mpinga Kristo
ilishaangamiza Ukristo katika mataifa kadhaa ambayo awali yalikuwa ni ya
Kikristo kwa asilimia 80 hadi tisini lakini sasa umefutika.
Alitaja
baadhi ya mataifa ambayo Ukristo umemalizwa kuwa ni pamoja na Misri,
Tunisia na Lebanon, ambayo sasa asilimia 80 ya watu wake sio Wakristo
tena.
Huku akinukuu maandiko ya Biblia kutoka katika vitabu vya
Matendo ya mitume na Yohana, alisema kuwa kanisa la kwanza lilipoingia
katika mateso kama lilivyo kanisa la Tanzania, halikukimbilia siasa wala
harakati, bali lilipiga magoti na kumuabudu Mungu wa mbinguni.
“Naliita
Kanisa la Tanzania kuachana na siasa, kuachana na mambo ya harakati
lichukue hatua ile ambayo kanisa la kwanza, lilichukua. Kanisa lidumu
katika maombi kwa kuwa masuala haya ni ya rohoni, hatuwezi kuyashinda
kwa njia nyingine yoyote,” alisema Askofu na kuongeza:
“Mateso ya
kanisa hayawezi kupata suluhu kutoka kwa mawanadamu, hatuwezi kupata
msaada kutoka kwa Mbunge, chama cha siasa au mabadiliko ya
uongozi…..msaada wetu watoka mbinguni tu. Kwa kutambua hilo nimeagiza
maombi ya mwaka mzima ili kukabiliana na roho hii ambayo inataka kuufuta
Ukristo kabisa kwenye sura ya nchi.”
Alisema, swali kubwa analojiuliza ni hatua gani Kanisa la Tanzania linachukua baada ya kuwa sasa limeingia katika mateso?
“Ikiwa
Kanisa la Tanzania litachukua hatua zilizochukuliwa na kanisa la
kwanza, ninahabari njema kwao kuwa Mungu atalitetea kama alivyowatetea
mitume waliokuwa kwenye mateso,” alisema kiongozi huyo.
Alinukuu maandiko kutoka Matendo ya Mitume 12:12, huku ujumbe wake ukiwa na kichwa; Utendaji wa Mungu kutuokoa.
Kiongozi
huyo alisema kuwa, wanasiasa wanamtazamo wao, wanaharakati wana mtazamo
wao, lakini kanisa linapaswa kuwa na mtazamo wa kiroho katika kipindi
chote cha mateso yake.
Alisema kuwa, historia inaonesha kuwa
wakati wote ambao kanisa liliiingia katika mateso likamgeukia kristo
ulitokea uamsho mkubwa, hivyo hata wakati huu ambao kanisa la Tanzania
linateswa, ni vyema likachukua hiyo kama fursa ya kuamka na kuhubiri
Injili kwa nguvu zote.
“Nasema tena, usalama wa Tanzania upo
kanisani tu, kanisa likilala amani haitakuwepo, usalama hautakuwepo,
naliita kanisa liamke na kuingia katika maombi marefu bila kuchoka,”
alisema.
Toa Maoni Hapa Chini