Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wapo wanaojiita wafanyabiashara,
lakini ni matapeli wa kimataifa nao wamepewa vibali vya kumiliki bastola
na wakati mwingine huzionyesha waziwazi wakiwa baa.
“Ufyatuaji wa risasi siku hizi umekuwa
holela…ninavyofahamu ukifyatua hata risasi moja, lazima uandikishe
maelezo polisi ulifyatua kwa sababu zipi siku hizi lakini hilo
halifanyiki,” ilidokezwa.
Inadaiwa kuwa kutokana na kuwapo kwa ulegevu wa
vyombo vya dola hususan Polisi, baadhi ya wamiliki wa bastola hizo
wamekuwa wakizikodisha kwa majambazi ambao huzitumia katika uporaji.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ulegevu huo katika
kudhibiti matumizi ya silaha, kumetoa mwanya kwa baadhi ya wamiliki
kukodisha bastola zao na kurudishiwa baada ya matukio pasipo
kugunduliwa.
Mkoa wa Mwanza
Uchunguzi unaonyesha kuwa watu wengi wamepata silaha kwa njia ya haramu.
Baadhi ya watu wamenunua kutoka kwa wakimbizi na
wengine wakipata vibali vya kumiliki kupitia kwa mawakala au maofisa wa
polisi wasiokuwa waaminifu.
Lugwecha Makune Mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, alisema kuwa hali ya uhalifu mjini Mwanza hivi sasa inatisha.
Alisema kuwa hivi sasa wahalifu wengi wanatumia bastola kupora watu mitaani tofauti na zamani walikuwa wakitumia mapanga.
Mkoa wa Kagera
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake,
mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Ngara alisema kuwa silaha nyingi hasa
bunduki za rashasha (sub machine gun) zinanunuliwa nchini Burundi.
“Wakati kambi za wakimbizi za Lukole zikifanya
kazi, silaha zilikuwa zikipatikana kwa wingi, lakini kwa sasa kwa kuwa
wakimbizi hao wameondoka, silaha zinafuatwa hukohuko,” alisema na
kuongeza:
“Kuna watu wana uhusiano na wenyeji wa Burundi,
basi wanaziagiza tu… bunduki moja ya SMG ni kama Sh200,000 wanakuletea.
Unajua kule kwa sasa kuna njaa kali kwa hiyo yale makundi ya waasi
yalikuwa na silaha nyingi hayana jinsi ila kuziuza ili kujikimu
kimaisha.”
Kwa upande wake Ofisa Mfawidhi wa Idara ya
Uhamiaji katika mpaka wa Rwanda na Tanzania (Rusumo), Mahirande Samuel
alisema ni vigumu kudhibiti wahamiaji haramu hasa katika mpaka wa
Burundi kwani ni mkubwa na uwezo ni mdogo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera,
Philip Kalangi alisema wahamiaji hao wamekuwa wakishiriki katika matukio
ya uhalifu wakishirikiana na wenyeji.
“Wahamiaji haramu wamechangia sana katika matukio
ya uhalifu. Wanaharibu mazingira kwa kuchoma misitu, kuchoma mkaa,
kupasua mbao na ujangili. Tunafaya juhudi kutekeleza agizo la Rais la
kuwaondoa nchini na kazi inaendelea vizuri,” alisema na kuongeza:
“Hadi sasa tumeshakamata silaha aina ya bunduki za
gobori 50 ambazo zimesalimishwa, ila wanaosalimisha hatuwajui maana
huzitupia kwa viongozi wa vijiji na kukimbia. Silaha tulizokamata ni
mbili ambazo ni SMG ikiwa na risasi 70 na gobori moja.
Maoni ya watu mbalimbali
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Profesa Humprey Moshi alisema kuongezeka kwa matukio ya watu
wanaotumia silaha, ni matokeo ya ukosefu wa amani katika nchi za jirani
ambao umesababisha wahalifu kuingia nchini kwa njia za kificho wakiwa na
silaha
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence
Mpangala alisema upatikanaji wa silaha kiholela unatokana na kubadilika
kwa mfumo wa maisha na kwamba baadhi ya watu siku hizi wanamiliki
silaha kama njia mojawapo ya kujipatia fedha kwa njia za uhalifu.
“Kuna mianya mingi ya kumiliki silaha kinyume na sheria, Serikali imeweka sheria ambazo ni lazima zifuatwe,” alisema.