Na Apostle Darmacy
UKUMBI wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, jana
uligeuka ulingo wa masumbwi, baada ya wabunge wa kambi ya upinzani
kupigana hadharani na askari wa Bunge.
Wabunge hao walichapana
ndani na nje ya ukumbi, hali iliyosababisha tafrani kubwa, huku maofisa
usalama na askari polisi kutoka kituo kikuu mjini Dodoma, wakilazimika
kuitwa kwenda kuongeza nguvu ili kukabiliana na hali hiyo.
Hatua
ya vurugu hizo, ilikuja baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe kunyanyuka ili kutaka kutoa hoja, ambapo Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai alimtaka kukaa chini hali iliyowafanya wabunge wote wa
upinzani kunyanyuka wakiashiria kumuunga mkono.
Mbowe, alisimama bungeni baada ya kutangazwa matokeo ya kutaka
kuendelea na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mkoani, Ali Khamis Seif
(CUF), kuomba mwongozo wa Spika wa kutaka Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uahirishwe hadi pale yatakapopatikana
maoni ya wadau kwa upande wa Zanzibar.
Hoja hiyo, ilionekana kuwa
mwiba mkali, baada ya Seif pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Tundu Lissu kutoa taarifa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Sheria na Katiba, Pindi Chana (CCM), kuwa amelidanganya Bunge kwa
kutoa taarifa ya uongo.
Baada ya hoja hizo, Naibu Spika Ndugai,
aliamuru kupigwa kura za kutaka kuendelea na mjadala huo ambapo wabunge
157 wakitaka kuendelea na mjadala huo, huku 59 wa kambi ya upinzani
wakitaka usiendelee.
“Baada ya kutangazwa kwa matokeo haya ya
kuamua kuendelea na mjadala ama laa kama alivyowasilisha mheshimiwa Ali,
sitataka kupokea taarifa yoyote.
“Ninachotaka kuwahakikishia
kiti changu kinatenda haki kwa kila upande wa vyama humu ndani, ila
ninachotaka kusema hakilali kitu hapa,” alisema Ndugai.
Wakati
Ndugai, akiwa amemtaka mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), ili aweze
kuendelea na hoja hiyo ndipo aliposimama Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akitaka kutoa taarifa huku Naibu Spika
akimzuia kwa kumtaka akae chini hali iliyowafanya wabunge wote wa
upinzani kunyanyuka ndani ya Bunge kama njia ya kupinga hali hiyo.
Wabunge
hao waliosimama ni wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, hali
iliyomfanya Naibu Spika Ndugai kutoa amri kwa askari wa Bunge kumtoa nje
Mbowe.
Agizo hilo la Ndugai liliibua hisia kutoka kwa wabunge wa
vyama hivyo na kwenda karibu na kiti cha Mbowe kama njia ya kumlinda
ili asiweze kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge na askari hao kama
ilivyoamuriwa.
Mvutano huo, ulioanza saa 6:35 mchana hadi saa 7
mchana, ilimlazimu Ndugai kutoa agizo tena mara ya pili kwakumtaka
kiongozi wa askari hao kutekeleza agizo hilo kwa kumtoa nje Mbowe.
Toa Maoni Hapa Chini