THAMANI YA KIFO CHA YESU PALE MSALABANI
Ni muhimu sana kukumbuka kwamba Yesu alikufa
pale msalabani kwa sababu kubwa mbili moja ni ili kurejesha mahusiano ya Mungu
na mtu kwa lengo la kumsaidia mtu aishi hapa duniani kwa kusudi la Mungu na pili
ili tupate wokovu na kisha kuurithi uzima wa milele.
Biblia katika kitabu cha Mathayo 26:53-54
inasema ‘Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye
ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje
basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?’
Kutokana na andiko hili ni vema tukajifunza kwamba;
Upendo wake (Yesu) ndio uliomsukuma kuyatoa
maisha yake kwa ajili yetu
Yesu alikuwa na uwezo wa kuangamiza askari
waliokuja kumkamata, lakini hakufanya hivyo ili andiko/kusudi la Mungu lipate
kutimizwa.
Ndani ya ufahamu wa Bwana Yesu kulikuwa na
mwanadamu, ndio maana kwa kuangalia ‘future’ ya mwanadamu na kusudi la uumbaji
wa Mungu ilimlazimu kupitia njia ngumu ya msalaba ili atupate mimi na
wewe.
Naam ndugu zangu tujiulize, ni upendo wa
namna gani wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Biblia inasema
katika kitabu cha Waebrania 2:1-3 ‘Kwa hiyo imetupasa kuyaangalia
zaidi hayo yaliyosikiwa tusije tukayakosa. Kwa maana ikiwa lile lililonenwa na
malaika lilikuwa imara, na kila kosa na uasi ulipata ujira wa haki, sisi je!
Tutapataje kupona, tusipojali wakovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na
Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia’
Katika kuendelea kuonyesha thamani ya kifo
cha Yesu pale msalabani Yohana naye aliandika akasema ‘Kwa maana
jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ila kila mtu
amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma mwana
ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika
yeye’ Yohana 3:16-17.
Jambo la muhimu ni kwamba Bwana Yesu hayuko
kaburini tena, naam alikufa na kufufuka ili awalete wengi kwenye ufalme wake.
Hivyo basi mpenzi msomaji nakusihi usiichezee neema hii, nakusihi usomapo ujumbe
huu wewe ambaye hujaokoka, fanya maamuzi ya kuokoka na wewe unayemjua Mungu
maanisha katika wokovu wako.
Twaliabudu na kulisifu jina lako wewe
uliyeutoa uhai wako kwa ajili yetu ee Bwana.
Ahsante kwa siku njema ya leo ambayo Bwana
umeifanya kwa ajili yetu ee Mungu.
Basi ndugu zangu tunapoadhimisha sherehe hizi
za pasaka tusiifanye kazi ya Yesu pale msalabani kuwa ni bure, bali kuanzia sasa
tusienende kama wamataifa waendavyo bali kama wana wa nuru.
Source http://meshackministry.blogspot.com/2012/10/thamani-ya-kifo-cha-yesu-pale-msalabani.html
Toa Maoni Hapa Chini