Zipo faida nyingi sana za kuwepo maombi ya muda mrefu kwa
mtu anayetaka kuona MUNGU akimpigania katika mambo yake.
1) Maombi haya
yanatoa nguvu ya kutosha ambayo humfanya MUNGU atume malaika zake waje
kushughulika na haja yako.
Efeso 3:20
Yakobo 5:16b, Matendo 12:5-11
Danieli 10:1-2,11-14.
Kutokana na utaratibu wa MUNGU wa kutenda kutokana na nguvu
wanazoachilia watu wake basi ni muhimu kuwa watu waombe kwa muda mrefu ili
wajenge nguvu ambayo MUNGU anapoitumia unakuja ushindi.
= Namna nyingine
za kuachilia nguvu za kiroho tofauti na maombi.
· Kusoma sana
NENO LA MUNGU.
Katika neno la Mungu unapata msaada na mwongozo wa kiimani
ambao huo unakupa mbinu za kuishi maisha matakatifu. Unapoishi katika utakatifu
ndipo unapojenga mazingira mazuri ya MUNGU kusikiliza maombi yako na
kukuhudumia.
1 Petro
3:12, Zaburi 16:3
2
Nyakati 7:14-16.
>Neno la Mungu
hukupa nguvu ya kushinda majaribu,na unaposhinda jaribu kwa neno unakuwa tayari
umeachilia nguvu ambayo MUNGU anaitumia kukufungulia baraka zingine. Mathayo
4:1-10.
· Kutoa SADAKA
Hii ni moja ya njia muhimu sana katika kuachilia nguvu ya
kiroho. Unapotoa sadaka unaigusa madhabahu ya MUNGU na kumfanya ashuke
kukuhudumia.
Malaki
3:10, Matendo 10:30-31.
Hapa Mungu anatusihi tumjaribu kwa sadaka ili afungue
milango ya baraka kutumwagia; hiki ndicho alichofanya kornelio na Mungu
akamkumbuka.
· KUSIFU kwa hali ya juu na katika roho.
Mungu wetu ni Mungu anayependa kusifiwa, kwa hiyo unapotoa
sifa kwake unauburudisha moyo wake na kumfanya ashuke kukuhudumia haja yako.
Matendo
16:25-26
· USHUHUDA wa
matendo makuu ya Mungu.
Hapa unamwinua Mungu na kumuaibisha shetani hivyo MUNGU
anatukuka na kukusaidia zaidi ili uendelee kumshuhudia na kumtukuza,
Ufunuo
12:11a
2) Maombi haya
yanakupa nguvu ya kutosha kuweza kupambana na milango ya kuzimu.
1 Petro 5:8-9a
Kuna wakati unaweza kujiuliza ni kwa nini unaandamwa na roho
chafu au nguvu za giza licha ya kwamba umeombea jambo hilo hata kwa muda mrefu.
Unachoyakiwa kujua ni kwamba nguvu unayoachilia bado haijatosha kuyaangusha
malango ya kuzimu yanayokuandama;hivyo inakupasa uombe zaidi hadi uone ushindi.
Mtumishi
mmoja alikuwa akishudia jinsi alivyoandamwa na roho ya uzinzi kwa muda mrefu,
akasema niliomba sana lakini roho hiyo haikuniacha. Baada ya hapo nilifunga kwa
muda wa mwezi mmoja lakini sikupata ushindi,ndipo nikaenda kuwashirikisha
wanamaombi wenzangu na wakafunga siku tano, ndipo MUNGU akatoa maono kwamba
ukoo wetu unaandamwa na uzinzi hivyo alikuwa amenipa mzigo mimi wa kuomba mpaka
roho hiyo itakapoachia ukoo; alisema.
Tunachojifunza hapa ni kwamba wakati
mwingine hupati majibu ya maombi yako kwa sababu umebeba mzigo mkubwa ambao
unahitaji nguvu kubwa kuutua,hivyo unapoona hali kama hizo omba msaada wa watu
wengine wakusaidie kuachilia nguvu iletayo ushindi.
3) Maombi haya humkumbusha MUNGU kuhusu hitaji
lako ulilowahi kumwomba.
Isaya 62:6-7,1 Samweli1:10-12,20
Luka 1:5-20.
Kuna wakati unapoomba, unajibiwa lakini MUNGU anakuwa
anasubiri kuiona juhudi yako katika kufuatilia maombi unayoomba. Kwa hiyo
usipoomba mara kwa mara unakuta majibu yanachelewa kwa kutokukumbushia kwako.
4) Maombi haya
hukupa nguvu ya kuweza kushinda majaribu.
Kuna wakati watu hujiuliza ni kwa nini watumishi wa Mungu
wanaanguka na kuacha wokovu? Suala ni kwamba unapookoka unatangaza vita na
shetani hivyo kila wakati anakuwa anakuwinda akuangushe,na hivyo anatuma
majeshi yake kukushambulia. Sasa unapokosa nguvu ya kutosha ndipo unakuta mtu
anazidiwa na nguvu za ibilisi na hatimaye anaanguka.
Hii ndio sababu iliyomfanya YESU awasisitize
wanafunzi wake waombe ili wasiingie majaribuni, Mathayo 26:41.
5) Maombi haya
hukujengea mazingira ya kukaa katika utukufu wa MUNGU na kukuwezesha kukaa
mbali na dhambi.
Unapokaa katika maombi kwa muda mrefu, moyo wako unakua
unafunikwa na roho mtakatifu na hivyo muda wako mwingi utakuwa unamtafakari
MUNGU na hii itakuweka mbali na kuzifikiria tamaa za ulimwengu huu.
6) Maombi haya
huubadilisha utu wa kale na kuleta utu ambao ni wa utukufu.
Mtu kabla hajaokoka anakuwa amefungwa kwenye roho mbalimbali
chafu, anapookoka anasafishwa na kupewa utu upya lakini kuna roho nyingine
unakuta zina maagano makubwa na hivyo suala tu la kuokoka haliziondoi roho hizo
ndani ya mtu.
Mtu huyu
atahitajika kuomba kwa muda mrefu au watu wengine wamsaidie ili kuachilia nguvu
ya kutosha itakayotumika kumfungua.
Wakati tuko
shule kuna binti mmoja tulimfanyia huduma, naye alikuwa anaandamwa na magonjwa
ya kila mara tena yasioeleweka. tulipokuwa tunamwombea alikuwa anafunguliwa
lakini baada ya siku chache tu alikuwa akirudia hali zilezile. Hatukukata tamaa
na hatimaye MUNGU akasema kuwa kuna mambo elfu moja yaliokuwa yamemfunga na
baada ya kuomba kwa miezi kama saba Mungu akasema limebakia jambo moja na iwapo
tukilishinda hilo atakuwa huru kabisa.
Sasa unaweza
kuona jinsi ambavyo ni hatari kufanya maombi kwa ufupi.
Kuna wengine
wakati hawajaokoka walikuwa wazinzi au walevi, wanapookoka unakuta roho hizo
bado zinawaandama, na wengine waanza kuona kuwa hawauwezi wokovu. suala ni
kwamba watu hawa wanatakiwa waendelee kuomba zaidi ili MUNGU apate nguvu ya
kutumia ili awafungue.
7) Maombi haya
hukupa amani ya kristo ambayo hukusaidia katika kufanya maamuzi sahihi juu ya
mambo yako.
Kuna wakati watu hufanya maamuzi ambayo baadae huja
wakayajutia, na wakati mwingine unaweza kukuta walimwomba MUNGU. Sasa tujiulize
ni kwa nini wafanye uamuzi ambao baadae wanaujutia?.
Jibu ni
kwamba unakuta maombi aliyofanya mtu huyu hayatoi nguvu ya kutosha kumfanya
MUNGU ashiriki kwenye maamuzi yako. Hiki ndicho kilimfanya YESU aombe usiku
kucha alipotaka kuwachagua mitume na ndicho kiliwafanya mitume waombe
walipotaka kuwaweka wakfu Barnaba na Sauli.
Luka 6:12-13, Matendo 12:3-4.
8) Maombi haya
yatakupa nafasi kubwa sana ya kusikilizwa mbele za Mungu.
Kuna mambo mengine MUNGU anakuwa hana mpango wa kuyafanya
lakini unapozidisha kuliomba basi Mungu anaingia kazini kulishughulikia.
Yakobo 5:17-18.
NB: "Hakuna kipimo kamili cha muda ambao mtu anatakiwa
kuutumia katika maombi kwa siku. Muda wa mtu kuomba utategemea msukumo wa roho
mtakatifu ndani ya mwombaji, lakini pia ni vizuri ukawa na utaratibu kwamba
mwisho wa maombi yako ni pale unapoona majibu ya maombi yako"
Toa Maoni Hapa Chini