"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa
maarifa ……." (Hosea 4:6). Maneno haya yaliyosemwa
na Mungu kwa kinywa cha Nabii Hosea yana ukweli ndani yake hata hivi leo.
|
Na Mwl C. Mwakasege |
Mama mmoja aliyekuwa na watoto sita (lakini
alikuwa hajaolewa), alipelekwa na mwenzake kwa Askofu wa dhehebu lao ili
wapate msaada kwa kuwa walikuwa na maisha ya shida sana. Yule mama pamoja
na watoto wake sita walikuwa wanakaa katika nyumba ya makaratasi, na
hawakuwa na chakula cha kutosha.
Askofu alimuuliza yule mama amewapateje wale
watoto wote sita na huku alikuwa hajaolewa.
Yule mama akajibu akasema; "Mtoto wa kwanza
nilimpata kwa kuwa nilikuwa nataka mtoto, niliona nazeeka bila ya kuolewa
nikaona nizae mtoto, Lakini mtoto wa pili nilimpata wakati nilipokuwa
natafuta chakula cha mtoto wa kwanza. Mtoto wa tatu nilimpata nilipokuwa
natafuta chakula cha watoto wawili niliokuwa nao. Na hali hii imeendelea
mpaka sasa nina watoto sita – na sijui nitaendelea na hali hii mpaka
lini".
Ni wazi kabisa si mapenzi ya Mungu huyu mama
aishi maisha ya namna hiyo. Vikwazo vya uchumi ambavyo vilimzunguka yule
mama na watoto wake vilitoka kwa ibilisi.
"Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa
maarifa ……." (Hosea 4:6). Maneno haya yaliyosemwa
na Mungu kwa kinywa cha Nabii Hosea yana ukweli ndani yake hata hivi leo.
Watu wengi sana siku hizi wanaangamizwa, wanadhulumiwa, wanahuzunishwa na
maisha kwa sababu tu wamekosa kuyajua maarifa ya Mungu yaliyomo katika
Neno lake.
Wakati fulani nilikuwa nafundisha katika
semina moja juu ya uhusiano wa maendeleo ya mtu na Wokovu, na wakati wa
kipindi cha majadiliano Mchungaji mmoja akatueleza habari iliyotufikirisha
sana.
Akasema ya kuwa katika kanisa alilokuwa
analihudumia miaka ya nyuma aliwahi kufuatwa na mama mmoja wa usharika huo
ambaye alikisema ya kuwa yeye alikuwa mmoja wa wakina mama thelathini
ambao hawashiriki chakula cha Bwana kwa kuwa walikuwa wanaishi hapo mjini
kwa njia za umalaya. Ombi lao kwa mchungaji wao lilikuwa ni kwamba akiweza
kuwasaidia kupata kazi za halali waache umalaya. Wao wametafuta kazi bila
ya mafanikio, na wanafanya umalaya si kwa sababu wanapenda, bali kwa kuwa
hawakuwa na njia nyingine ya kupatia fedha.
Ni jambo la kumshukuru Mungu, ya kuwa
mchungaji yule aliweza kuwatafutia kazi wale wakina mama wote katika
kiwanda kimoja, na maisha yao yakabadilika wakaacha umalaya, na kuishi
maisha ya kikristo yenye ushuhuda.
Ni watu wangapi ambo wanaishi maisha yao
kinyume na maadili ya kikristo ili kupata fedha za kuwasaidia kila siku? –
Ni wazi kuwa ni wengi. Je! hawawezi wakapata riziki yao bila kudhulumu au
kuiba au kudanganya au kuzini? – Ni wazi kuwa wanaweza. Sasa, ni kwa nini
wanaishi kwa jinsi hiyo?
Jambo ambalo watu wanahitaji kujua ni kuwa
baba wa uongo yaani shetani amewadanganya kwenye mawazo ya kuwa hakuna
njia nyingine ya halali ya kupatia fedha isipokuwa hizo. Na shetani
anausimamia uongo huo ili uonekane kuwa ni kweli kwa kuwawekea watu hasa
wakristo vikwazo vigumu vya kiuchumi.
Unaweza ukawa unajiuliza vikwazo hivyo ni
vipi? Vikwazo hivi vinatofautiana katika watu mbalimbali na mahali
mbalimbali. Kuna watu wengine wataona hakuna mradi wa halali wanaoufanya
unaofanikiwa. Mwingine miradi yake inafanikiwa, lakini fedha yote inaishia
kutafutia matibabu ya magonjwa yaliyomo ndani ya nyumba yake ambayo
hayaishi.
Mwingine anapata magari mengi, lakini
hayaishi kupata pancha na kuharibika au kuanguka. Mara nyingi utawasikia
watu wa jinsi hii wanasema wana mkosi. Kwa kweli si mkosi bali vikwazo vya
kiuchumi toka kwa shetani ili ushindwe maisha na UANZE KUTAFUTA MAISHA
MAZURI KWA NJIA ZILIZO KINYUME NA MAADILI YA KIKRISTO YALIYO
MATAKATIFU.
Jambo ambalo wakristo wengi
hawalifahamu
Mimi na mke wangu miaka ya mwanzo tulipookoka
hasa mwaka 1984 na 1985 tulikumbana na vikwazo vigumu sana vya kiuchumi.
Tuliona jinsi maisha yalivyokuwa yanarudi nyuma – fedha tuliishiwa,
chakula tuliishiwa, nguo tuliishiwa, vitu ndani vilianza kuharibika na
hatukuwa na fedha za kuvitengenezea. Tulijaribu kulima bustani za mboga,
hazikufanikiwa. Tulijaribu kupika chapati za kuuza, hazikununuliwa
zikaharibika tukazitupa.
Kwa kifupi tuliona maisha ya wokovu kuwa ni
magumu, ya shida na ya kimaskini sana. Tulishindwa hata namna ya
kuwasaidia ndugu zetu vizuri. Hali hii ilitutia uchungu sana. Watu
hawakufahamu ya kuwa hali hii ilikuwa inatunyima amani ya kweli ya wokovu
– kwa kuwa tulijitahidi kuwachangamkia wote ili kuficha mapambano
tuliyokuwa nayo kimaisha.
Ilikuwa ni vigumu sana kuishi maisha ya
ushuhuda mzuri wa kikristo katikati ya mahitaji makubwa kama hayo
tuliyokuwa nayo.
Tulijua kuwa Zaburi 23:1 inasema, "Bwana
ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu". Lakini tulikuwa
tumepungukiwa na vitu vingi vya lazima katika maisha. Hatukufahamu kwa
nini sisi kama kondoo wa Kristo tulikuwa tumepungukiwa namna
hiyo!
Tulikuwa tunasoma lakini tunashindwa
kumwelewa Mtume Paulo alipokuwa anasema katika Wafilipi 4:12 kuwa;
"najua kudhiliwa, tena najua
kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa
kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa".
Tuliona ya kuwa Mtume Paulo aliweza kuwa na
amani na ushindi katika hali yo yote aliyokuwa nayo – hata katika
upungufu. Sisi tulikosa amani tulipokuwa tumepungukiwa! Na hili jambo
lilitusumbua sana.
Tulikuwa tunafurahi tunaposoma mstari kama
ufuatao; " …..vyote ni vyenu …. Vile vilivyopo sasa, au vile
vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu, nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa
Mungu" (Wakorintho 3:21,22). Tulikuwa tunafurahi kwa kuwa maneno haya
yanatupa uhalali wa kumiliki vitu vilivyo vya Mungu. Kwa mfano Hagai 2:8
inasema "Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa
Majeshi." Pia, Zaburi 24:1 inasema "Nchi na vyote viijazavyo ni
mali ya Bwana …" Lakini jambo lililotusumbua ni kwamba ingawa mistari
hiyo ilitupa umilikaji juu ya fedha, dhahabu na vyote viijazavyo nchi ili
tuvitumie – SISI HATUKUWA NAVYO WALA HATUKUJUA TUTAVIPATAJE!
Tulifahamu ya kuwa ni mapenzi ya Mungu
tufanikiwe katika mahitaji ya kiroho na mahitaji ya mavazi, chakula, na
malazi; soma kitabu cha 3 Yohana 1:2. Kwa hiyo tulikuwa na hamu kubwa ya
kufanikiwa.
Tulitamani sana kuona maneno ya Wafilipi 4:19
yanatimia kwetu – nayo yanasema hivi;
"Na Mungu wangu atawajazeni kila
mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo
Yesu".
Hali hii ilitufanya tuingie katika maombi
mazito, ili kumuuliza Mungu njia na namna ya kuondokana na hali tuliyokuwa
nayo.
Mambo makubwa matatu yafuatayo, Roho wa Mungu
alituambia kuwa ni chanzo cha matatizo yaliyokuwa yanatukabili: Alituambia
yafuatayo:
Kuwa, ingawa tumezaliwa mara ya pili na
kuingizwa katika ufalme wa Mungu – tulikuwa bado tunategemea utaratibu wa
uchumi wa duniani badala ya kutumia na kutegemea utaratibu wa uchumi wa
mbinguni;
Kuwa, tulikuwa tunapenda kupokea bila ya kuwa
watoaji, na pia tulitaka kuvuna tusichokipanda. Roho Mtakatifu aliuliza
swali, Je! unaweza kwenda kwenye bustani yako kuchuma nyanya huku ukijua
kuwa hujawahi kupanda nyanya? Ni wazi kuwa jibu lilikuwa ni
hapana.
Kuwa, hatujafahamu ya kuwa adui yetu ibilisi
ndiye chanzo cha mahangaiko na mafadhaiko yaliyoambatana na kupungukiwa
mahitaji katika maisha. Na pia tulikuwa hatutumii silaha tulizopewa ili
kuzivunja kazi za ibilisi katika maisha yetu.
Baada ya kupokea majibu hayo kutoka kwa
Mungu, tulitubu na kuomba msamaha. Tuliendelea kumwomba Mungu atufundishe
na atuongoze katika kuishi maisha ya kutumia na kutegemea utaratibu wa
uchumi wa ufalme wa mbinguni.
Mafundisho tuliyoyapata yalituondoa katika
mahangaiko ya kupungukiwa na kutuingiza katika furaha na amani ya
mafanikio NDANI YA KRISTO.
Ndiyo maana tumechukua hatua hii chini ya
uongozi wa Roho Mtakatifu kukushirikisha baadhi ya mafundisho hayo ili
ikiwa umo katika hali ya mahangaiko ya kupungukiwa na mahitaji muhimu ya
maisha upate msaada wa kuondokana nayo.
Kumbuka ni mapenzi ya Mungu ndani ya Kristo
kuwa ufanikiwe na uishi maisha ya ushindi katika maeneo yote ya maisha
yako na katika siku zote utakazoishi juu ya nchi.
Mwl C. Mwakasege
credit to http://maishaushindi.blogspot.com/
Toa Maoni Hapa Chini