Hillary Clinton na Donald
Trump wamefanya mikutano ya dakika za mwisho mwisho kuwahimiza raia wa
Marekani wawapigie kura zikiwa zimesalia saa chache kabla ya uchaguzi
kufanyika.
Wote wawili wamefanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya kushindaniwa ya Carolina Kaskazini, Pennsylvania na Michigan.
Bi Clinton amewahimiza wapiga kura kuunga mkono kuwepo kwa “Marekani yenye matumaini, inayojumuisha wote na yenye ukarimu”.
Bw Trump naye amewaambia wafuasi wake kwamba wana “fursa nzuri ya kuvunja mfumo mbovu na usio na maadili”.
Kura za maoni zinaonesha Bi Clinton wa chama cha Democratic akiwa
asilimia nne mbele ya mpinzani wake Bw Trump wa chama cha Republican.
Wapiga kura wengi kuliko awali, zaidi ya 46 milioni, tayari wamepiga kura za mapema.
Kuna ishara za wapiga kura wa asili ya Kihispania (Latino/Mexico)
kujitoleza kwa wingi, jambo ambalo wengi wanaamini litamfaa Bi Clinton.
Uchaguzi mkuu unafanyika baada ya kampeni kali ambapo wapiga kura walirushiana matusi na kila mmoja alikabiliwa na kashfa.
Kwenye hafla Philadelphia, Pennsylvania, Bi Clinton ameungana na
nyota Bruce Springsteen na Jon Bon Jovi jukwaani pamoja na mumewe Bill,
Rais Obama na mkewe Michelle.
Bw Obama amewataka wapiga kura kukataa kutawaliwa na woga na badala yake waamue kukumbatia matumaini.
Mkutano wa mwisho wa kampeni wa Bi Clinton ulikuwa Raleigh, Carolina Kaskazini, ambao angemshirikisha Lady Gaga.
Awali, alisema kwenye mahojiano redioni kwamba akishinda atampigia
simu Bw Trump na kwamba anatumai mgombea huyo wa chama cha Republican
anaweza “kutekeleza mchango muhimu” katika kuunganisha tena taifa hilo.
Bw Trump, kwenye mkutano wake wa kampeni mjini Scranton katika jimbo hilo alisisitiza kwamba kampeni yake imekuwa ikiimarika.
Mkutano wake wa mwisho ulikuwa Grand Rapids, Michigan.
Awali, aliwaambia wafuasi wake jimbo la Florida kwamba yeye “si mwanasiasa” na kwamba anawajali wao pekee.
Mfanyabiashara huyo alimweleza Bi Clinton kama “mtu mwovu zaidi
aliyewahi kuomba kuchagulikuwa kuwa rais”, akirejelea uchunguzi wa FBI
kuhusu hatua ya Bi Clinton ya kutumia sava ya kibinafsi ya barua pepe
kutuma barua pepe rasmi alipokuwa waziri wa mambo ya nje kati ya 2009 na
2013.
Jumapili, Bi Clinton alipata nafuu baada ya FBI kusema barua pepe
mpya zilizokuwa zimegunduliwa kwenye uchunguzi mwingine hazikutoa
ushahidi wowote wa kumpata na hatia.
Hayo yakijiri, meneja wa kampeni wa Bw Trump, Kellyanne Conway
amepuuzilia mbali wasiwasi miongoni mwa jamii ya kimataifa kuhusu
uwezekano wa mgombea huyo wa Republican kushinda.
Akiongea na BBC Jumatatu, alisema ukosoaji ambao umekuwa ukitoka nje
ya nchi “hauashirii sifa halisi za Donald Trump na sababu zinazomfanya
awanie urais na sifa atakazokuwa nazo jukwaa la kimataifa akishinda”.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande alikuwa amesema bilionea huyo humfanya “ahisi kutapika”.
Bw Trump amekabiliwa na shutuma kali hasa kutokana na madai ya
kuwadhalilisha kingono wanawake, madai ambayo Bw Trump ameyakanusha.
Aidha, kuna kadha zilizotolewa zikimuonesha akitoa matamshi ya
kuwadhalilisha wanawake. Bw Trump alisema mazungumzo hayo yalikuwa ya
mzaha na ya faraghani.
Bw Trump pia ametuhumiwa kwa kueneza chuki dhidi ya wageni baada ya
kuapa kuwapiga marufuku Waislamu wasiingie Marekani kwa muda kama njia
ya kukabiliana na ugaidi.
Aliwaeleza raia wa Maexico kuwa “wabakaji” na kadhalika, alisema
angejenga ukuta kwenye mpaka wa Marekani kuwazuia Wamarekani wasiingie
nchini humo.
Credit to