TAARIFA KWA UMMA SIKU YA UTALII DUNIANIA 2016 NA MAONESHO YA KARIBU KUSINI
(Tourism for All – Promoting Universal Accessilibity)
Wizara ya Maliasili na Utalii
kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mradi wa kuboresha
Mtandao wa Hifadhi za Kusini mwa Tanzania (SPANEST) pamoja na Wadau wa
Sekta ya Utalii nchini watashiriki katika Maadhimisho ya Siku ya
Utalii Duniani kwa mwaka 2016 sambamba na Sherehe za maadhimisho ya
‘’Karibu Kusini ‘’ Karibu Tanzania Southern Circuit’’ ambayo Kitaifa
yataadhimishwa Mkoani Iringa kwenye viwanja vya Kichangani kuanzia
tarehe 25 hadi 29 Novemba, 2016.
Lengo la maadhimisho hayo ni
kuweka uelewa kwa Jamii kuhusu umuhimu wa utalii na thamani yake ikiwa
pamoja na kuutangaza Utalii kwa kuihamasisha jamii kutumia fursa za
utalii zilizopo katika kuinua uchumi wa wakazi wa Ukanda wa Kusini mwa
Tanzania na Taifa kwa ujumla
Kauli Mbiu ya maadhimisho ya Siku
ya Utalii Duniani kwa mwaka 2016 ni “Utalii kwa wote – wote
wawezeshe’’ (Tourism for All – Promoting Universal Accessilibity). Kwa
kuzingatia Kauli Mbiu hii, Serikali inatambua kuwa kuna watu wenye
mahitaji maalumu kama vile walemavu, wazee na watoto ikisisitiza
miundombinu rafiki, gharama nafuu kutembelea vivutio vya utalii na
gharama nafuu za usafiri ili kuhakikisha kwamba, utalii unawahusisha
watu wengi zaidi kunufaika nao.
Katika Maadhimisho hayo, Wizara
itakuwa na washiriki ambao ni Idara pamoja na Taasisi zake mbalimbali.
Idara zitakazoshiriki ni Utalii, Wanyamapori, Mambo ya Kale na Misitu na
Nyuki.
Kwa upande wa Taasisi
zitakazoshiriki ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha
Utalii, Makumbusho ya Taifa, Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mamlaka ya Usimamizi ya Wanyamapori (TAWA)
Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania,
(TFS) Taasisi ya Utafiti wa Misitu na Wadau wa Wizara ya Maliasili na
Utalii.
Wadau wa Sekta ya Utalii kutoka
mikoa ya Nyanda za Juu Kusini watashiriki kuonesha bidhaa na huduma zao
muhimu. Mikoa hiyo ni pamoja na Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na Songwe
Aidha, Wizara itatoa punguzo kwa
watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na vivutio vya
utalii vilivyokaribu na mji wa Iringa ambavyo ni Ismila,Kalenga na Boma
la Mkuu wa Wilaya kwa gharama nafuu.
Kupitia Maadhimisho hayo wito
unatolewa kwa kuwaalika wadau wote wa utalii na jamii husika kwa pamoja
na kuadhimisha siku hii kama ishara ya jitihada za pamoja za kuufanya
utalii nguzo ya kweli ya maendeleo ya jamii na maendeleo ya jamii ni
chanzo cha sekta ya utalii endelevu zaidi
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maliasili na Utalii.