Maana, dalili, vipimo na matibabu ya tezi dume.



Tezi Dume (Prostate gland)
Tezi dume ni sehemu mojawapo ya mfumo wa uzazi wa kiume. Inaundwa na
sehemu mbili, lobes, ambazo zimeunganishwa na kufunikwa kwa nje kwa
utando wa tishu. Tezi hii ipo mbele kidogo ya puru (rectum) na na chini
kidogo ya kibofu cha mkojo. Tezi dume inauzunguka mrija unaounganisha
kibofu cha mkojo na uume (urethra).
Mojawapo ya kazi za tezi dume ni kutoa majimaji yanayochanganyika na
mbegu za kiume (sperms) wakati wa kilele cha tendo la ngono.
Mchanganyiko huu wa mbegu pamoja na majimaji hayo hufanya shahawa
(semen). Aidha majimaji hayo husaidia kuzipa mbegu za kiume nguvu ya
kusafiri kwenye uke mpaka kufikia kwenye mirija ya fallopian tayari kwa
utungisho na yai la kike. Vilevile husaidia kupunguza hali ya
kitindikali iliyopo katika uke, ambayo kama isiporekebishwa, huweza kuua
mbegu nyingi za kiume na kufanya utungisho kuwa wa tabu.
Kuvimba Tezi Dume (BPH)
Kwa kadiri mwanaume anavyozeeka, ni jambo la kawaida pia kwa tezi dume
kuongezeka ukubwa na kuvimba. Hali hii kitabibu huitwa Benign Prostate
Hyperplasia au wengine hupenda kutumia maneno Benign Prostate
Hypertrophy kwa kifupi BPH. Kwenye makala hii tutautumia sana ufupisho
huu wa BPH ili kurahisisha mambo.
Ukuaji wa tezi dume hupitia
hatua kuu mbili. Hatua ya kwanza hutokea kipindi cha balehe wakati tezi
dume linapoongezeka ukubwa na kuwa mara mbili ya lilivyokuwa hapo awali.
Baada ya hapo ukuaji husimama kwa muda mpaka kijana anapofikisha miaka
25 hadi 30 ndipo hatua ya pili ya ukuaji huanza tena. Ukuaji huendelea
kwa viwango na kasi tofauti kati ya mtu na mtu na hatimaye kusababisha
BPH katika umri wa utu uzima.
Wakati tezi dume linapokua na kutanuka, utando wa tishu unaozulizunguka
hutanuka pia. Hata hivyo ingawa tezi dume huendelea kukua, hufikia
wakati utando wake huacha kutanuka na kufanya tezi dume kubana mrija wa
kutolea mkojo kutoka kwenye kibofu. Hali hii husababisha kibofu cha
mkojo kuwa na ngozi ngumu. Hali hii hufanya kibofu cha mkojo kuhisi
kutaka kutoa mkojo nje hata kama kiasi cha mkojo ndani yake ni kidogo
sana. Hufikia wakati, kibofu huwa dhaifu na kupoteza uwezo wake wa
kuhisi kutoa mkojo na hivyo kufanya mtu anapokojoa kushindwa kutoa mkojo
wote na badala yake hubakiza kiasi fulani cha mkojo kwenye kibofu.
BPH husababishwa na nini?
Chanzo halisi cha BPH au vihatarishi vyake (risk factors) havijulikani
kwa uhakika. Kwa muda mrefu imekuwa ikichukuliwa kuwa BPH hutokea kwa
wanaume watu wazima na wazee tu. Aidha imewahi kuonekana huko nyuma kuwa
PBH haitokei kwa wanaume ambao wamewahi kufanyiwa operesheni ya kuondoa
korodani au wale ambao walizaliwa bila korodani. Hali imepelekea baadhi
ya watafiti kuamini kuwa BPH ina uhusiano mkubwa na umri wa mtu pamoja
na uwepo wa korodani.
Makala ha hapa chini imeandikwa na Asha Bani
NILIWAHI kuandika makala kuhusiana na saratani ya tezi dume baada
ya kufanya mahojiano na mwathirika wa ugonjwa huo, Dk. Emmauel Kandusi.
Kupitia makala ile ambayo alieleza namna ugonjwa huo ulivyo hatari
kwa taifa, wengi walijitokeza kutaka kujua dalili na hali hatarishi za
ugonjwa huo.
Ingawa nilifanikiwa kuwaunganisha na Dk. Kandusi mwenyewe kwa maelezo zaidi, kwa wengine nilishindwa kufanya hivyo.
Kwa mazingira hayo, natumia nafasi hii kueleza mambo kadhaa yahusuyo
ugonjwa huo, nikiamini kama si kuyamaliza, basi nitakuwa nimepunguza
maswali ya wengi.
Nitakachofanya ni kuweka namba ya mawasiliano ya Dk. Kandusi ili waweze kuwasiliana naye moja kwa moja kwa ushauri zaidi.
Dk. Kandusi anaanza kuelezea maana ya saratani kwamba ni jina la
ugonjwa ambalo hutokea wakati chembechembe za uhai katika sehemu fulani
ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu na mfumo wa mwili.
Chembechembe hizi huasi na kutengeneza vivimbe vidogo vidogo.
Lakini kwa kuwa yeye ni muathirika wa saratani ya tezi dume,
anauelezea kwa undani ugonjwa huo unaosumbua watu wa jinsia ya kiume.
Anasema saratani ya tezi dume ni ugonjwa unaopatikana katika mwili wa
kiumbe mamalia dume tu, ambapo chembechembe za uhai katika tezi dume
zinakua bila kufuata utaratibu na mfumo wa mwili.
Hizo huasi na kutengeneza vivimbe vidogo vidogo na mtu kuwa amethirika.
Hali hatarishi
Dk. Kandusi anasema kuna hali hatarishi nyingi ambazo zinachangia
mwanamume kupata saratani ya tezi dume, ikiwa ni pamoja na umri ukifikia
miaka 50 na kuendelea.
Nasaba
Kama katika ukoo kuna historia ya ugonjwa wa saratani ya tezi dume,
suala la nasaba linachangia kumweka mwanamume kuwa hatarini kuathirika
na saratani hiyo kwa misingi ya kinasaba ‘genetic.’
Lishe
Ananasema wanaume wanaopenda kula nyama nyekundu ‘red meat’ yenye
mafuta mengi na aina ya maziwa yenye mafuta mengi wako katika hali
hatarishi ya kuathirika.
Mazoezi
Kama mwanamume hafanyi mazoezi na ana unene hatarishi, sambamba na
ukosefu wa virutubisho D, ana uwezekano mkubwa wa kuugua ugonjwa huo.
Dalili za saratani ya tezi dume
Dk. Kandusi anasema kuwa kuna dalili nyingi za saratani ya tezi dume,
ikiwa ni pamoja na udhaifu katika kujisaidia haja ndogo na pindi
inapopatikana, inakuwa ni ya kukatiza katiza.
Kushindwa kukojoa na kushindwa kuanza kupata haja ndogo huku unapohisi haja ndogo unapata shida pia kujizuia isitoke yenyewe.
“Hisia ya kutaka kupata haja ndogo na hata wakati mwingine kwa usiku
unaweza ukakojoa kitandani, pia unaweza ukapata maumivu na kuhisi mwasho
wakati wa haja ndogo,” anasema Dk. Kandusi.
Anasema hii ni kutokana na uume kusimama kwa shida na hata maumivu makali pindi anapotoa manii wakati wa kujamiiana.
Anasema dalili nyingine ni kuwapo kwa damu damu wakati wa kukojoa na
katika manii, huku kukiwa na maumivu ya viungo, ikiwa ni pamoja na
kiuno, miguu na mgongo.
Pia anaeleza kuwa mgonjwa anaweza kukosa hamu ya kula na kupungua uzito.
Dk. Kandusi anasema pamoja na kuelezea dalili za ugonjwa huo, lakini
mwanamume anapoanza kuziona na kuzihisi kati ya dalili hizo, ni lazima
ajue kuwa chembe chembe za uhai hasi katika tezi dume lake zina umri wa
takriban miaka saba na kuendelea.
Uchunguzi
Anatoa wito kwa wanaume wenye umri wa takriban miaka 50 na kuendelea
kuweka kipaumbele tabia ya kufanyiwa uchunguzi wa tezi dume angalau mara
moja kwa mwaka.
Vipimo
Kuna vipimo vya uchunguzi wa tezi dume kama vipimo ashiria, kitaalamu
‘Prostate Specific Antigen (PSA) na Digital Rectal Examination (DRE),
kwa mujibu wa Dk. Kandusi.
Tiba
Anasema kuna tiba za aina nyingi, ikiwa ni pamoja na ya uangalizi
(active surveillance), upasuaji (surgery) homoni (hormonetherapy),
mionzi (radiotherapy), dripu kemikali (chemotherapy) na kama
ikigundulika una saratani dume unatakiwa kushauriana na daktari wako ni
tiba ya aina ipi inatakiwa kufanyika kati ya hizo.
Pia Dk. Kandusi anatoa wito kwa wanaume wote wenye umri wa miaka 50
na kuendelea wanapopatwa na ugonjwa wa aina yoyote ni vema wakapimwa na
saratani ya tezi dume.
Pia anasema kila mtu anatakiwa kutambua kuwa saratani ikigundulika mapema ni rahisi kutibika.
Hata hivyo, hivi karibuni kikundi cha 50 Campaign walifanya uzinduzi
wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua basi
litakalotumika katika kampeni ya kuhamasisha watu dhidi ya ugonjwa huo,
harambee iliyoendeshwa na raia wa Boston, Shedmin Luvanda, ambaye
alikabidhi hundi ya dola za Marekani 5,000 ambazo zilichangwa na yeye na
marafiki zake wa Boston.
Lengo ni kukusanya kati ya sh milioni 45 na sh milioni 126 kwa ajili ya kununua gari jipya au lililotumika.
Kutokana na ugonjwa huo kuwa hatari hapa Tanzania, ifikapo mwaka 2020
unatarajiwa kuua watu milioni 20, hivyo Dk. Kandusi anaomba taasisi na
watu binafsi kuchangia fedha kwa ajili ya kununulia gari na masuala
mengine ya vipimo na matibabu.
Anasema ili kufanikisha mpango huo, mtu anaweza kuchangia kwa M- Pesa
namba 0754 402033 au kupitia akaunti namba 01J1027311100 katika tawi
lolote la CRDB, ikiwa na jina la akaunti ‘Center for Human Rights
Promotion –CHRP’
0788 150 928
Makala imeandikwa na Asha Bani
Source: Tanzania Daima