TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Afrika ijifunze kutoka Korea, Mawaziri.
Nchi
za Afrika zimehimizana kutumia sera , mbinu na mfumo wa maendeleo
uliotumiwa na Jamhuri ya Korea kufanya mapinduzi makubwa ya uchumi,
viwanda na teknolojia katika kipindi cha miongo michache iliyopita.
Hayo yamejiri kwenye Mkutano wa Mawaziri wa nchi za Afrika na Korea uliohitimishwa leo jijini Addis Ababa, Ethiopia.
"Katika
miaka ya 1960 hali ya uchumi na mazingira ya Korea yalikuwa yanalingana
na bara la Afrika, hivyo, mfumo ulioifanya Korea kufanya mapinduzi ya
uchumi unafaa kutumiwa na bara la Afrika kwa kuwa mazingira yetu
yanafanana".
Katika
mkutano huo ambaoTanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga, Mawaziri
walielezea kuridhishwa na ushirikiano huo tokea ulipoanzishwa mwaka
2006, kwa kuwa unazingatia maslahi ya pande zote na haufungamani na
masharti ya aina yoyote.
Walisema kuwa Bara la Afrika lina fursa lukuki zikiwemo maliasiri kama madini, mafuta na ardhi nzuri kwa kilimo.
Rasilimali
hizo miaka yote zimekuwa zikiuzwa nje bila kuendelezwa kutokana na
ukosefu wa viwanda na teknolojia, hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kulifanya bara hilo kubaki nyuma kimaendeleo.
Hivyo, kupitia jukwaa hilo la ushirikiano na Korea, bara la Afrika litapokea misaada ya fedha za maendeleo na teknolojia itakayotumiwa kujenga viwanda vya kusindika rasilimali ili kuziongezea thamani.
Kwa
kuwa maendeleo na amani na usalama ni vitu vinavyotegemeana, Mawaziri
walisisitiza umuhimu wa kutunza amani barani Afrika kwa kushirikiana na
Korea.
Walibainisha masuala mbalimbali yanayotishia amani ya dunia
likiwemo tatizo la ugaidi wa kimataifa. Walikubaliana kuwa ugaidi ni
changamoto ya ulimwengu mzima na ili ufumbuzi wake upatikane lazima
wadau duniani kote washirikiane.
Ushirikiano
wa nchi za Afrika na Korea unatimiza miaka 10 mwaka huu tokea
ulipoanzishwa mwaka 2006. Kwa muktadha huo, ulisisitizwa umuhimu wa
kufanya tathmini na ufuatiliaji wa miradi ya utekelezaji ili kubaini
mafanikio mapungufu na changamoto. Hiyo itasaidia kuchukua hatua stahiki katika kufikia malengo yaliyowekwa na umoja huo.
Kwa
upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se
alieleza mafanikio ya ushirikiano huo tokea kunzishwa kwake. Alisema
katika eneo la ushirikiano wa kiuchumi na Afrika, Korea ilikuwa mwenyeji
wa Mkutano wa tano wa Mawaziri wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea
na Afrika mwezi Oktoba 2016.
Katika
mkutano huo, Korea iliahidi kutoa Dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili
ya kusaidia masuala ya kiuchumi barani Afrika. Fedha hizo zinatarajiwa
kuongezeka mara dufu katika
kipindi kijacho. Aidha, Korea inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa
Jukwaa la ushirikiano wa viwanda kati ya Korea na Afrika katika wiki
mbili zijazo.
Vile
vile, Korea imeongeza mara dufu misaada ya maendeleo kwa bara la Afrika
na ile misaada ya maendeleo inayohusisha nchi mbili (bilateral) itaongezeka kutoka asilimia 24 hadi kufikia asilimia 35 itakapofika mwaka 2020.
Waheshimiwa
Mawaziri walihitimisha mkutano wao kwa kuridhia nyaraka mbili ambazo ni
Tamko la Addis Ababa na Mwongozo wa Ushirikiano kati ya Korea na
Afrika. Mwongozo huo umeainisha miradi mbali mbali itakayotekelezwa
katika kipindi cha miaka mitano 2017 - 2021. Maeneo hayo ni pamoja na:
biashara, kuendeleza viwanda na uwekezaji; uzalishaji katika kilimo na
kiwango cha mavuno; uchumi wa bahari, uendeshaji wa bandari na usafiri
wa majini; kuwaendeleza vijana na kuwajengea uwezo wanawake.
Wajumbe walikubaliana kuwa mkutano ujao utafanyika Seoul, Korea mwaka 2021.
Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI.
TAREHE 08 DESEMBA 2016
|