HATUA 12 KATIKA MAOMBI YA KUJIFUNGUA KUTOKA
KATIKA VIFUNGO MBALIMBALI NA NAMNA YA KUOMBA.
|
Mwl.Tuntufye A. Mwakyembe |
1.
Unapotaka kuomba maombi haya
hakikisha unaamini kuwa Mungu yupo na kuwa anazo nguvu za kukufungua hata
ukiomba wewe mwenyewe….Isaya 61:1 aya
ni maneno ya Bwana Yesu “Roho ya Bwana
Mungu i juu yangu, kwa sababu Bwana amenitia mafuta, niwahubiri wanyenyekevu
habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka
uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.”
2.
Amini kuwa Mungu huwapa thawabu
wale wamtafutao kwani Maandiko yanasema katika … Ebrania 11:6 b kuwa “Kwa
maana mtu amwendeae Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa
thawabu wale wamtafutao.” Kama ukiamua kumtafuta amehaidi kukusaidia
3.
Omba huku ukiamini Mungu anakwenda
kukufungua, kukuweka huru, kukujibu mahitaji yako… Ebrania 10:38 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani;
naye akisitasita, roho yangu haina furaha naye”.
kumbuka msingi mkubwa wa maombi haya ni kuamini, ukisita sita Mungu hana
furaha nawe.
4.
Kwenye Moyo wako tengeneza shauku
ya kuutua mzigo wako kwa Yesu, iwe ni hamu yako iwe ni haja yako, pia iwe ni matamanio yako …Math 11:28 anasema “Njoni
kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha…”
Hakuna mwanadamu anayeweza kuutua mzigo wako isipokuwa Bwana Yesu
5.
Tubu kwani inawezekana umehusika
kwa namna moja ama nyingine kumpa ibilisi nafasi ya kukunyanyasa, na kama
hujahusika tubu kwa ajili ya waliohusika ikiwa unawajua, inaweza kuwa wazazi au
ndugu wa karibu Mungu atasamehe …Isaya
43: 25 “Mimi, naam, mimi,Ndimi niyafutae makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe,
wala sitazikumbuka dhambi zako” Ukitubu kwa kweli Mungu amesema hata
zikumbuka dhambi zako na hivyo utakuwa na ujasiri wa kuendelea kusogelea
kusogelea madhabahu yake kwa maombi
6.
Wasamehe wote waliosababisha mateso
na uchungu kwenye maisha yako…Math 6:14 “Kwa
maana mkiwasamehe watu makosa yao Mungu wa mbinguni atawasamehe ninyi makosa
yenu… Marko 11:26 “Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni
hatawasamehe ninyi makosa yenu.” Kumbuka
kisasi ni juu ya Bwana samehe alafu mwambie Bwana Yesu akufungue.
7.
Omba kwa kukiri ukitamka kwa kinywa
chako… Warumi 10:10 “Kwa maana kwa Moyo
mtu huamini hata kupata haki, na kwa
kinywa hukiri hata kupata wokovu” pia ukisoma… Mithali 18:21 anasema “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa
ulimi; nao waupendao watakula matunda yake” tumia kinywa chako kukiri
uzima, omba kwa kutamka, tafuta mazingira ambayo hauta msumbua mtu mwingine,
tamka kwa kinywa chako Ushindi, mafanikio , uzima huku ukikemea yale
usiyoyataka na Mungu atafanya.
8.
Omba kwa kutumia Damu ya Yesu … Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa Damu
ya mwana kondoo...” Damu ya Yesu inatupa ushindi pia ukisoma …Isaya 53:5
anasema “Bali alijeruhuwa kwa makosa
yetu alichubuliwa kwa maovu yetu adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake na kwa
kupigwa kwake sisi tumepona.” Ukiendelea katika… 1petro 1:18a-1 Ninyi mfahamu
kuwa mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo bali kwa Damu ya thamani kama ya
mwanakondoo asiye na hila asiye na waa yaani kristo. Kwa hivyo amini kabisa
kuwa ipo Damu ya Yesu itakayo kusaidia kushinda maana anasema wakamshinda kwa
Damu ya mwana kondoo.
9. Omba
kwa kutumia Jina la Yesu… Yoh 14:14
“Mkiomba neno lolote kwa jina langu,
nitalifanya.” Pia ukisoma Marko 16:17 “Na Ishara hizi Zitafuatana na
hao waaminio: kwa jina langu watatoa pepo
watasema kwa lugha mpya…” Hakikisha maombi yako yanajengeka katika
misingi ya jina la Yesu…tumia jina la Yesu kukemea, kuomba na katika kila hali
ya kuitaji msaada toka kwa Mungu.
10.
Tumia moto wa Roho Mtakatifu… wakati
mwingine kwenye maandiko umejulikana kama moto ulao… Eliya aliwahi kuamuru Moto toka Mbinguni ukashuka na kuteketeza
Askari waliokuwa wametumwa na mfalme dhidi yake…2Wafalme1:10 “Eliya akajibu
akamwambia Yule akida wa hamsini ikiwa mimi ni mtu wa Mungu na ushuke Moto
kutoka Mbinguni ukuteketeze wewe na hamsini wako Moto ukashuka ukawateketeza
yeye na hamsini wake”. lakini pia
aliamuru Moto ushuke nao ukashuka na kuteketeza sadaka… Falme 18:37 Unisikie ee Bwana unisikie ili watu hawa wajue ya kuwa
wewe Bwana ndiwe Mungu na kuwa wewe unawageuza
moyo wakurudie ndipo Moto wa Bwana ukashuka ukateketeza sadaka ya kuteketezwa
na kuni na mawe na mavumbi ukayaramba yale maji yaliyokuwemo
kwenye mfereji…Elewa wazi kabisa kuwa unao uwezo wa kushusha moto hata kama
hautauona kwa macho ya kibinadamu lakini lakini uwe na uhakika utateketeza na
kuharibu vitu vya adui katika ulimwengu wa roho.
11.
Tumia Neno la Mungu maana li hai tena
lina nguvu Ebrania 4:12 anasema “Maana
neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote
ukatao kuwili; tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta
yaliyomo ndani yake; tena lijepesi
kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo, wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi
mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na
mambo yetu. Hivyo basi uwapo katika maombi haya tumia neno la Mungu kudai
ukombozi wako ndio sababu pia ukisoma Yeremia 1:12 anasema “Ndipo Bwana akaniambia, umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno
langu, ili nilitimize.” Hakikisha unasimamia ahadi za Mungu kila unapoomba
na mkumbushe Mungu kupitia ahadi zake.
12.
Shugulikia chanzo cha tatizo kwa maombi chanzo
cha tatizo chaweza kuwa Roho za upatilizo / kurithi …wapo waliorithi uchawi,
magonjwa, mikosi na mabalaa, kutokufanikiwa, ufukara, utasa na mengineyo mengi.
Kutoka 20:5b anasema “Nawapatiliza wana maovu ya Baba zao…” Hivyo
basi kuna mabaya unayapitia tu kwa sababu ya wazazi wako au watu wa ukoo wako
waliopita… pia ukisoma Maombolezo 5:7
anasema “Baba zetu walitenda dhambi hata
hawako, na sisi tumeyachukua maovu yao” kataa na ujitenge na kila uovu wa
nyuma kwa jina la Yesu kwa Damu ya Yesu na kwa Moto wa Roho Mtakatifu ndio
sababu ukisoma Zab
11:3 anasema “Kama misingi
ikiharibika, mwenye haki atafanya nini?” Unaweza kuwa una haki lakini
ulitolewa kwa mizimu au kwa nguvu za giza lazima ujue na ujinasue kwa maombi
kataaa kabisa hali yoyote ya kuhusishwa na mambo ya kurithi..toka katika
familia na ukoo kwa namna ya magonjwa, mikosi na mabalaa.
Elewa kuwa
unashugulika na Ulimwengu usio onekana ( ulimwengu wa Roho) hivyo ni lazima kujipanga kwa maombi na neno
la Mungu.
Efeso
6:12 anasema “Kwa
maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na
mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika
ulimwengu wa roho”
Kwa hivyo basi pata muda wa kuomba kila wakati maana
unapoomba unampa Mungu nafasi ya kukusaidia na kukutetea katika mambo mengi
ambayo unayahitaji kila wakati.
Kwa mawasiliano zaidi.
Mwl.Tuntufye A. Mwakyembe
+255767629562
+255715629562
Arusha. Tanzania
Pia waweza kutufuatilia kupitia