JINA LA YESU KRISTO – MOJAWAPO YA FUNGUO ZA UFALME WA MBINGUNI
Sehemu 1
|
Mwl Christopher Mwakasege |
“Nami nakuambia ….. na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu;
wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za
ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa
limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa
limefunguliwa mbinguni” (Mathayo 16:18 – 19).
Maneno haya ya Yesu Kristo yanatuonyesha kuwa, nia yake ni kulijenga
kanisa lililo na mamlaka kuliko shetani. Kanisa ni mwili wake (Waefeso
1:22 – 23). Wakristo waliookolewa kwa damu ya Yesu Kristo ni viungo vya
mwili wa Kristo – ni viungo vya kanisa (1 Wakorintho 12:12, 13, 27). Kwa
hiyo Yesu Kristo anaposema atalijenga kanisa lake wala milango ya kuzimu
haitalishinda – ana maana ya kuwa, kila mkristo aliye wake anajengwa
kiroho awe na mamlaka ya kumshinda shetani.
Ni budi tufahamu ya kuwa, Yesu Kristo hawezi kutuambia tufungue kama
hakuna kitu cha kukifungua. Hawezi kutuambia tufunge kama hakuna kitu
cha kufunga. Kwa hiyo ni lazima kuna vitu vya kuvifunga na kuna vitu vya
kuvifungua.
Pia, tufahamu ya kuwa, Yesu Kristo hawezi kutuambia tufunge na kufungua
kabla hajatupa uwezo na mamlaka ya kufanya hivyo. Uwezo na mamlaka
tunapata ndani ya Kristo aliyetukabidhi funguo za ufalme wa mbinguni.
Itakuwa haina maana kwa Yesu Kristo kutukabidhi funguo bila ya
kutufundisha namna ya kuzitumia. Hawezi kutukabidhi mamlaka bila
kutufundisha namna ya kuyatumia.
Yesu Kristo anasema tukifunga au tukifungua, mbinguni nako kunatia mhuri
kitendo hicho. Hatuwezi kufanya hivyo kama tulichokifanya hakifanani na
mapenzi yake. Ndiyo maana tunaomba kuwa mapenzi yake yatimizwe hapa
duniani, kama yanavyotimizwa huko mbinguni. Kwa maneno mengine tunaweza
kusema ya kuwa ukifanya kitu chochote katika mapenzi ya Mungu, Ufalme wa
mbinguni utakuwa upande wako.
Aina za Funguo:
Biblia inazungumza juu ya funguo za aina tano zifuatazo:
1. Funguo za Ufalme wa Mbinguni – Mathayo 16:19 – Yesu Kristo amekabidhi
funguo hizi kwa wakristo (Kanisa).
2. Funguo za mauti na za kuzimu – Ufunuo 1:18 – Funguo hizi anazo Yesu
Kristo – baadaye atampa Malaika mmoja funguo za kuzimu ili amfunge
Ibilisi (Ufunuo 20:1-3).
3. Ufunguo wa nyumba ya Daudi – Isaya 22:22; Ufunuo 3:7. Ufunguo huu
anao Yesu Kristo.
4. Ufunguo wa kawaida wa mlango – Waamuzi 3:25.
Neno
‘funguo’ lililoandikwa katika Mathayo 16:19; Ufunuo 1:18; Isaya 22:22 na
Ufunuo 3 – 7 lina maana ya ‘mamlaka’. Kazi ya funguo ni kufunga na
kufungua. Kwa hiyo ukipewa funguo maana yake umepewa mmalaka ya kufunga
na kufungua.
Kwa mfano, mtu akikupa funguo za chumba – maana yake una mamlaka juu ya
chumba hicho kukifunga na kukifungua. Mtu yeyote akitaka kuingia kwenye
chumba hicho hawezi kufanya hivyo bila kupata ruhusa toka kwako ya
kumfungulia. Ukipewa funguo za gari maana yake kwa muda huo ambao una
funguo hizo za gari, una ‘mamlaka’ juu ya hilo gari kulifunga lisitumike
au kulifungua litumike. Mtu akitaka kulitumia ni budi aje kwako kwa
ajili ya kufuata funguo.
Kwa hiyo Yesu Kristo aliposema ametupa funguo za ufalme wa mbinguni
alikuwa ana maana ya kuwa ametupa ‘mamlaka’ ya ufalme wa mbinguni. Ni
vizuri ufahamu hapa ya kuwa ufalme wa mbinguni ni ufalme wa Mungu ulio
na mamlaka juu ya falme nyingine zote – ufalme wa shetani, ufalme wa
wanyama, ufalme wa wadudu, ufalme wa mimea, ufalme wa ndege, na
kadhalika. Ikiwa wewe ni mkristo uliyeokoka basi fahamu ya kuwa, una
mamlaka uliyopewa na Yesu Kristo juu ya falme hizi zote!
Yesu Kristo anaendelea kusema kuwa; lolote utakalolifunga duniani,
litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani,
litakuwa limefunguliwa mbinguni.
Kwa mfano ukiamua kumfunga ibilisi asikusumbue katika maisha yako,
mbinguni pia wanasimamia utekelezaje wa jambo hili. Hata kama ibilisi
ataamua ‘kukata rufaa’ juu ya uamuzi wa kumzuia asikusumbue na akaenda
kwa Mungu kuomba aachiliwe – Mungu atamwambia ‘rudi kwa aliyekufunga,
akikufungua nami nitakufungua, lakini asipokufungua nami sikufungui’
Unaweza kusema mbona shetani alipewa ruhusa na Mungu kumjaribu Ayubu.
Kumbuka kuwa Ayubu aliishi katika agano la kale na sisi tunaishi katika
agano jipya ambalo ndani yake tuna mamlaka ya kumfunga shetani kwa jina
la Yesu Kristo.
Kuna wakristo wengi wameonewa na ibilisi kwa kuwa hawajui mamlaka waliyo
nayo na namna ya kuyatumia.
Jambo jingine ninalotaka uone hapa ni kwamba Yesu Kristo alisema ametupa
“funguo ZA ufalme wa mbinguni”; na hakusema ametupa ufunguo wa ufalme wa
mbinguni.
Neno hili ‘ZA’ lina maana ya kuwa kuna funguo za ufalme wa mbinguni
zaidi ya mmoja. Kumbuka kuwa kuna tofauti ya funguo za ufalme wa
mbinguni na zile funguo za mauti na za kuzimu
Funguo za mauti na za kuzimu alikuwa nazo shetani hadi aliponyang’anywa
funguo hizo na Yesu Kristo kwa kufa kwake msalabani na kufufuka. Funguo
za mauti na za kuzimu anazo Yesu Kristo sasa.
Funguo za ufalme wa mbinguni anazo Yesu Kristo, lakini amezikabidhi kwa
wakristo waliomo duniani wazitumie
Ukifuatilia maneno yaliyomo katika
agano jipya utaona ya kuwa kuna funguo NNE za ufalme wa mbinguni nazo ni:
1. Jina la Yesu Kristo
2. Damu ya Yesu Kristo
3. Neno la Yesu Kristo
4. Nguvu za Roho Mtakatifu
Katika somo hili tunajifunza juu ya jina la Yesu Kristo ambalo ni
mojawapo ya funguo za ufalme wa mbinguni.
Tumia mamlaka uliyopewa:
Kuna wakati fulani ambapo nilihangaika siku nyingi kwa kuomba na kwa
kulia usiku na mchana ili shida niliyokuwa nayo iniondoke bila mafanikio.
Nilikuwa naomba kwa Mungu, lakini sikuona mabadiliko yoyote, ilikuwa
kama vile Mungu ameziba masikio yake asisikie maombi yangu. Pamoja na
maombi niliongeza kulia zaidi lakini sikufanikiwa pia.
Nikiwa katika hali ya kukata tamaa huku nikijiuliza kwa nini naomba kwa
Mungu lakini shida inayonisumbua haiondoki – Roho Mtakatifu alisema
ndani ya roho yangu maneno haya; “shida yako inayokusumbua imeletwa na
shetani. Unayo mamlaka ya kumkemea shetani naye ataondoka na shida
uliyonayo itakwisha. Kama hufahamu juu ya mamlaka uliyonayo soma vitabu
vya Waefeso, Wafilipi, Wakolosai na vitabu vingine katika Biblia”
Niliposikia maneno hayo nikaomba tena; “Ee Bwana nifundishe juu ya
mamlaka uliyonipa ili nipate kuyatumia.”
Namshukuru Mungu ya kuwa alisikia sala yangu na alianza kunifundisha juu
ya mamlaka aliyonipa, na bado anaendelea kunifundisha hatua kwa hatua
kila siku.
Nilipoendelea kujifunza ndipo nilipotambua kuwa si kila shida uliyonayo
itaondoka kwa maombi – bali shida nyingine zinaondoka kwa KUAMURU katika
jina la Yesu Kristo shida hiyo iondoke au kwa KUAMURU hali unayoitaka
itokee.
Kwa hiyo siku moja usiku niliamua kutumia mamlaka niliyonayo katika jina
la Yesu Kristo shetani aondoke katika eneo alilokuwa ananiletea shida –
mara hiyo hiyo kulitokea mabadiliko. Shida iliyonisumbua kwa muda mrefu
ilitoweka mara moja. Badala ya kusubiri Mungu afanye kitu kwanza juu ya
shida hiyo, niliamuru iondoke na Mungu akasimamia utekelezaji wake!
Ndivyo alivyomaanisha aliposema “Lolote utakalolifunga (wewe!) duniani,
litakuwa limefungwa mbinguni” – Maana yake Mungu atausimamia uamuzi wako
wa kulifunga hili jambo! Ukiamua kulifunga, Mungu atalifunga pia!
Anayeanza kufanya kitu ni wewe!
Hivi ndivyo Mtume Petro alivyofanya alipomkuta yule mtu aliyekuwa kiwete
tangu tumboni mwa mama yake – wakati huo alikuwa ana umri usiopungua
miaka arobaini akiomba sadaka katika mlango wa kuingia hekaluni.
Mtume Petro alipomwona hakumwomba Mungu amponye bali alimwamuru asimame
na kutembea kwa Jina la Yesu Kristo! Alisema hivi; “Kwa Jina la Yesu
Kristo wa Nazareti, simama uende”. Halafu; “Akamshika mkono wa
kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa
nguvu. (Yule aliyekuwa kilema) Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda,
akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akirukaruka, na kumsifu
Mungu” (Matendo ya Mitume 3:6 – 8).
Kile alichoamuru Mtume Petro kitokee kwa jina la Yesu Kristo kilitokea.
Alimwamuru yule kilema asimame na kutembea kwa jina la Yesu Kristo na
ikawa hivyo!
Na wewe unaweza kufanya hivyo ikatokea! Kwa nini? Kwa sababu na wewe
umepewa jina la Yesu Kristo lenye uwezo usiobadilika! Kumbuka Yesu
Kristo alisema hivi;
“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; Kwa jina langu watatoa
pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha
kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao
watapata afya” (Marko 16:17-18).
Labda umeyasoma maneno haya mara nyingi kiasi kwamba umeyazoea, na
yameanza kupoteza uzito wake. Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa Roho
Mtakatifu ayahuishe upya maneno haya ndani yako ili uyaone kama Yeye
anavyotaka uyaone.
Siku moja nilikuwa nafundisha neno
la Mungu mahali fulani, na baada ya mafundisho alijitokeza mtu mmoja
aliyesema anaumwa kifua na kwamba aliihitaji aombewe.
Nilimwambia aweke mkono wake kifuani mahali alipokuwa anaumwa – na
akafanya hivyo. Na mimi nikaweka mkono wangu juu ya mkono wake uliokuwa
kifuani pake, halafu nikasema “Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti”!
Nilipotamka tu jina hili la ajabu, yule mtu akaanguka chini na majini
yaliyokuwa yanabana kifua chake na kuleta maumivu yalianza kupiga kelele.
Nikayaamuru yamtoke mtu huyo kwa jina la Yesu Kristo – na yakamtoka
wakati huo huo – mtu huyo akasimama akiwa mzima!
Kwa nini ilikuwa hivyo? Kwa kuwa Yesu Kristo alisema kwa jina lake
tutatoa pepo! Na ndivyo ilivyo! Tumia mamlaka uliyo nayo usiogope! Ikiwa
wewe ni mwamini yaani umeokoka, jina la Yesu Kristo ni lako – ni uamuzi
wako kulitumia au kutokulitumia.
Siku nyingine niliitwa kwenda kumwombea mama mmoja ambaye alikuwa hawezi
kuinuka kitandani kwa muda wa miezi miwili kwa sababu ya ugonjwa wa homa.
Nilipofika katika nyumba hiyo niliweka mkono wangu juu ya kichwa cha
mama yule na kuiamuru homa imwache kwa jina la Yesu Kristo, kisha
nikaondoka. Nilimwacha yule mama akiwa amelala. Kesho yake mtoto alikuja
kuniambia kuwa mama yake amepona, ameamka toka kitandani na anafanya
kazi! Jina la Yesu Kristo libarikiwe milele.
Yesu Kristo alisema tukiweka mikono yetu juu ya wagonjwa kwa jina lake,
watapata afya. Na ndivyo inavyotokea tukitii agizo hili. Kuna uweza
usiopimika katika jina la Yesu Kristo. Ni ufunguo unaowafungua watu toka
katika minyororo ya shetani. Usiogope. Uwe na moyo wa ushujaa na ujasiri
mwingi – tumia mamlaka uliyonayo katika jina la Yesu Kristo.
Toa Maoni Hapa Chini