Bwana Yesu asifiwe, baada ya siku mbili za
salamu ninatamani nikushirikishe sasa ujumbe huu muhimu kwako wa kuzijua sababu
za Mungu kujibu maombi yako.
Ninaamini unamaombi mengi ambayo umemuomba
Mungu na bado hujajibiwa.
Hii mistari itatuongoza leo kuelekea kwenye
somo letu.
Daniel 9:2-3, 22-24
Habakuki 2:1-3
Mhubiri 3:1-3
1 Nyakati 12:32.
Ni desturi ya Mungu kujibu maombi yako,
Mathayo 7:7
''Ombeni nanyi mtapewa.. ''
Shida iliyopo kwa watu wengi siyo kuomba,
shida iliyopo ni kuona kile wanachokiomba kinatoa lini na saa ngapi, wengi
hakiwasumbui kuomba bali kinawasumbua kuona Mungu anawajibu lini.
Ni wajibu wa Mungu kujibu maombi ya watoto
wake.
1. Mungu ana muda wa jambo unaloliomba
kwake.
Siku zote tambua moja ya sababu za Mungu
kujibu maombi yako ni muda na nyakati alizozikusudia Mungu juu ya jambo hilo,
lipo kwenye muda, keep on waiting, endelea kungoja maana hilo japo lipo kwenye
muda, muda wake ukifika utaliona likitokea.
Hii ni Bible study kidogo, natamani
ujifunze na mimi katika hii mistari michache ya vitabu vinne tofauti ili uone
jambo ambalo Mungu anatutazamisha juu ya MUDA ULIOAMRIWA wa jambo unaloliomba
kwake.
Danieli 9:2-3
''katika mwaka kwanza wa kumilika kwake,
mimi Danieli kwa kuvisoma vitabu,nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la
BWANA lilimjia Yeremia nabii ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka
sabini, nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga na kuvaa nguo za magunia na majivu''
Baada ya Daniel kuvisoma vitabu unaona
akipata jibu ya nini alichokuwa anakitafuta, majibu yake aliyapata kwa sababh
jambo hilo alilokuwa analiomba lilikuwa limefungwa ndani ya muda ambao ulikuwa
umeamriwa na Mungu mwenyewe.
Danieli aliamua kuingia kwenye maombi
watoke kwenye utumwa baada ya kuona Taifa la Israel likiendelea kukaa kwenye
Nchi ya utumwa, hii inanipa kutazama yakwamba walikuwa wamechoka kukaa
utumwani, Mungu anamjibu juu ya kile anachokiomba yakuwa kipo kwenye muda
ulioamriwa juu yao ni majuma sabini yaani MIAKA SABINI.
Habakuki 2:1-3
''Mimi nitasimama katika zamu yangu,
nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi
nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu, BWANA akanijibu, akasema,
iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma
kama maji, Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili
kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa
haina budi kuja, haitakawia''.
Mhubiri 3:1-3
''Kwa kila jambo kuna majira yake,Na wakati
kwa kila kusudi chini ya mbingu, Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa;Wakati
wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa
kupoza;Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga''
Daniel 9:22 ''Akaniagiza, akaongea nami,
akasema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu, Mwanzo wa
maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe
unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya, Muda wa
majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili
kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya
uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia
mafuta yeye aliye mtakatifu''.
1 Nyakati 12:32
''Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili
za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israel wayatende; vichwa vyao walikuwa
watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao''.
Nimekutazamisha uone hiyo mistari yote
jinsi inavyozungumzia habari ya nyakati za kila jambo ambalo Mungu anakuwa
amelikusudia lifanyike, kwa maana nyingine majira, au muda ulioamriwa juu ya
jambo hilo.
Kwa nini jambo unaloliomba kwake likae
kwenye muda/nyakati.
1. Ni ili kuwa na uwezo wa kumudu ukipewa
hilo jambo, Isaya 54:2 '' Panua mahali pa hema yako... '' maana yake ongeza
uwezo wa kumudu, increase the capacity to handle things.
2. Ni ili kutimiza mapenzi ya Mungu juu ya
hilo jambo, ndiyo maana ukiomba mapenzi ya Mungu unapata amani katika
kulingojea hilo maana halitakawia wala kusema uongo. Habakuki 2:1-3,
Mathayo 26:41-44.
Mungu wangu akubariki sana kwa kujifunza
pamoja na mimi.
Na Mwl David Sedekia
P. O Box 1652
Dodoma
Tanzania.