Na Apostle Darmacy
KESI inayomkabili Askofu Mkuu wa Kanisa
la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe, imechukua sura
mpya baada ya mama mzazi wa Jaji Agustine Shangwa anayesikiliza shauri
hilo kumvaa mwanaye na kumtaka ajieleze kwa nini amekataliwa na
walalamikaji.Jaji Shangwa alisema kesi hiyo imemletea
mzozo na mama yake mzazi anayeishi Bukoba ambaye baada ya kusoma taarifa
za kukataliwa kusikiliza shauri hilo zilizochapishwa na gazeti moja la
kila siku (sio Tanzania Daima), alimpigia simu na kumhoji kwa nini
hawatendei haki walalamikaji.
Alidai kuwa kitendo cha
walalamikaji kukimbilia katika vyombo vya habari hakikuwa cha kistaarabu
kwa kuwa yeye katika kesi hiyo ni mshauri tu na sio msikilizaji.
Pamoja
na kutoa siri hiyo, Jaji Sangwa amechukua uamuzi mwingine mzito wa
kukataa kujitoa katika kesi hiyo kama alivyotakiwa na walalamikaji
waliodai kutokuwa na imani naye kwa vile alionyesha upendeleo kwa
mshtakiwa.
“Jamani mimi nilikuwa nikiwashauri tu nyie
walalamikaji lakini mkaenda kwenye gazeti hilo na sijui na kwa watu
gani wengine kulalamika kuwa siwatendei haki, hadi mama yangu
akaniuliza, sasa nendeni mkaseme tena kuwa leo nimerudia kutowatendea
haki, maana hao waandishi wana vinasa sauti vinarekodi kila kitu,”
alisema Jaji Shangwa na kusababisha watu kucheka.
Akieleza sababu
za kugoma kujitoa, Jaji Shangwa alisema walalamikaji wameshindwa kutoa
hoja za maana ambazo zingeweza kumfanya ajiondoe kwenye kesi hiyo.
Jaji
Shangwa alitoa uamuzi huo mwishoni mwa wiki akisema amefikia uamuzi huo
wa kukataa kujiondoa kwenye kesi hiyo kwa kuwa yeye si msikilizaji bali
ni msuluhishi.
“Msisononeshwe na uamuzi huo, mimi ni Jaji
Msuluhishi tu katika kesi hii na si Jaji Msikilizaji. Hivyo kama
usuluhishi wa kesi hii ukishindikana jalada litarudishwa kwa Jaji
Mfawidhi ili ampange jaji mwingine wa kuisikiliza kesi hii,” alisema
Jaji Shangwa.
Walalamikaji katika kesi hiyo ya tuhuma za
ubadhirifu wa mali na pesa zaidi ya shilingi bilioni 14 pamoja na
ukiukwaji wa katiba ya kanisa hilo, Dezedelius Patrick, Angelo
Mutasingwa na Benedict Kaduma walimtaka Jaji Shangwa ajiondoe mwenyewe
katika kesi hiyo kwa madai kuwa hawana imani naye.
Walalamikaji
hao walimwandikia barua Msajili wa Mahakama Kuu Dar es Salaam, Agosti
26, mwaka huu, wakimtaka Jaji Shangwa ajiondoe mwenyewe katika kesi hiyo
wakidai kuwa amekiuka maadili ya kitaaluma, taratibu na heshima ya
mahakama na ameonyesha upendeleo kwa mlalamikiwa.
Wanadai kuwa
mlalamikiwa hakuwasilisha maelezo yake ya maandishi (WSD) ndani ya siku
21 na kwamba siku ya kutajwa kwa kesi hiyo wakili wake Miriam Majamba
alitoa sababu za uongo lakini jaji hakutilia maanani na badala yake
Agosti 2, 2011 yeye alitoa hukumu dhidi yao wakati kesi hiyo haijafikia
hatua hiyo.
Walalamikaji hao wanadai maneno ya jaji huyo
yalikuwa na upendeleo wa waziwazi kwa Kakobe. Katika ushauri wake katika
kesi hiyo, jaji huyo alisema, “Nyie walalamikaji nasema bila
kumung’unya maneno kuwa madai yenu yote ni majungu… Kakobe ni mungu wa
kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, kanisa ni mali yake… kwa hiyo
kama anakula fedha za kanisa anakula fedha zake, hakuna wa kumhoji kwani
lile ni kanisa lake na ni mali yake,” alisema.
Walalamikaji hao
wananukuu maneno ya jaji huyo aliyedai: “Kakobe atawashinda kesi hii na
kuwadai pesa nyingi, kwa hiyo futeni kesi, kama na ninyi mnataka
kaanzisheni makanisa yenu, uaskofu wake alijipa mwenyewe sio kama
makanisa mengine wanaosomea.”
Kwa mujibu wa hati ya madai
iliyowasilishwa mahakamani, walalamikaji hao wanamtuhumu Kakobe kuwa
amekuwa akikusanya fedha kutoka kwa waumini wake kwa madai ya kufanyia
shughuli na miradi mbalimbali ya kanisa na kuzitumia isivyo halali.
Mbali
na kufuja fedha hizo kama vile kugharamia kampeni za kisiasa, pia
wanadai kuwa amekuwa hatoi taarifa ya mapato na matumizi ya fedha
anazozikusanya.
Miongoni mwa madai hayo ni makusanyo ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya kununulia vifaa vya kuanzisha televisheni.
Hata
hivyo wanadai kuwa badala yake Kakobe anadai kuwa vifaa hiyo
amevirudisha Marekani alikovinunua kwa kuwa eneo la mradi huo
limeathiriwa na mradi wa umeme wa msongo mkubwa na kwamba kwa sasa
anataka kuhamia jijini Boston Marekani.
Kuhusu ukiukwaji wa
katiba ya kanisa hilo, walalamikaji hao wanadai kuwa katiba inataka
kuitishwa kwa mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano ambacho ndicho
chombo cha juu cha maamuzi lakini Kakobe hajawahi kuitisha mkutano huo
tangu mwaka 1989.
Pia wanadai kuwa katiba hiyo inataka kanisa
liwe na Katibu Mkuu na Mweka Hazina ambao ndio watakaolinda mali za
kanisa lakini Kakobe amekuwa akifanya maamuzi na shughuli zote peke
yake.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Oktoba 24 mwaka 2011.
Toa Maoni Hapa Chini