Thursday, February 23, 2017
MAGAZETI YA LEO IJUMAA FEBRUARY 24,2017
- Next You are viewing Most Recent Post
- Previous Denice Simeo Youth Development Expert atoa ushauri kwa vijana wa chuo
google+
There is greatness inside of you
I believe that there is a seed of greatness in all human beings. Therefore the aim of my blog is to bring to my readers awareness of things that are happening around us. I will focus majorly on inspirational news that can motivate my readers to doing more with their lives too. If you are too busy to get acquainted with what is in the newspapers or you have read the papers but have not felt any inspiration or motivation, please log on this page and be inspired to walk in your purpose and dream.
KUMALIZA MWENDO KISHUJAA
Na Askofu Rodrick Mbwambo
Utangulizi:
1 Samweli 13:13-14
Baada ya Mungu kuwaumba wanadamu wa kwanza
na kuwaweka katika bustani ya Edeni, aliwaruhusu kula matunda ya miti
yote ya bustani, isipokuwa matunda ya mti wa kujua mema na mabaya.
Katika kuwakataza matunda ya mti huo, aliwaambia, “siku mtakapokula,
hakika mtakufa.” Kwa maneno mengine, Mungu aliwaambia kuwa, “siku
mtakapokula matunda ya kujua mema na mabaya, maisha yetu hayatakuwa tu
na mwanzo, ila yatakuwa na mwisho pia.” Baadaye Adamu na Eva
kudanganywa na kula matunda ya mti huo, kwa mara ya kwanza mauti iliweza
kuingia kwa wana wa Adamu na kuyafanya maisha yao kuwa na mwanzo na
mwisho pia.
Tunapouangalia mwanzo wa maisha ya
mwanadamu, tunaweza kuugawanya mwanzo huo katika vipindi vikubwa viwili.
Kipindi cha kuzaliwa na kipindi cha utoto. Hali kadhalika kipindi cha
kumalizia nacho, kiko katika sehemu kubwa mbili. Kipindi cha kwanza ni
kile cha kutafuta na kutumikia kusudi la maisha, na kipindi cha pili ni
kile cha kulikamilisha kusudi hilo. Ukiangalia vipindi hivi viwili vya
maisha ya wanadamu, unaweza kuona kuwa, hakuna mwanadamu anayewajibika
katika kile kipindi cha kwanza cha maisha yake. Katika kipindi hiki cha
maisha, mwanadamu hapati nafasi ya kuchagua familia ya kumzaa wala eneo
nzuri linalofaa kwa ajili ya kuzaliwa kwake.
Kutokana na ukweli huu, hakuna mtu
anayeweza kulaumiwa kwa jambo lolote lililotokea katika kipindi hiki cha
maisha. Uharibifu pekee ambao mwanadamu atahusishwa nao, ni ule
unaotokea katika kipindi cha kumalizia maisha, kinachoanzia pale akili
ya mtu inapovikwa uwezo wa kuyabeba maisha yake. Uzembe kidogo katika
kipindi hiki, utaufanya mwisho wa mtu kuwa mbaya kama ilivyotokea kwa
mfalme Sauli. Kama ilivyo kwa wanadamu wote, maisha yake ya utoto
yalikuwa kama ya watoto wengine, ila alimalizia vibaya kutokana na
kushindwa kulitumikia vema kusudi la maisha yake. Katika hili ninataka
utambue kuwa, mashujaa wa imani kamwe hawataabishwi na vile utoto wao
ulivyokuwa, bali hutaabishwa na vile mwisho wa maisha yao utakavyokuwa!
Kwa kuwa ni mapenzi ya Mungu kuwaona watoto wake wakimalizia vizuri,
katika somo la leo tutajifunza kuwa kinyume na madhaifu yaliyoonyeshwa
na Sauli katika kipindi chake cha mwisho, ili hatimaye, tumalize mwendo
kama mashujaa.
KUCHAGUA KUMFURAHISHA MUNGU
“Ndipo Sauli akamwambia Samweli,
Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA, pia na maneno yako;
kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.” ISamweli 15:24
Mara zote katika kipindi cha kulitafuta
kusudi la maisha na kulitumikia, mapenzi ya wanadamu huwa yanavutwa
katika maeneo makubwa mawili. Eneo la kwanza linalowavuta, ni lile
linalohusiana na miili yao, linalowataka kuwapendeza wanadamu kuliko
kumpendeza Mungu aliyewaumba. Eneo lingine, ni lile linalozihusu roho
zao linalowasukuma kumpendeza Mungu kuliko kuwapendeza wanadamu.
Tunapokiangalia kipindi cha Sauli kulitafuta kusudi la maisha yake na
kulitumikia, tunaweza kuona kuwa, alianza vizuri kama lilivyokuwa
limeanza kanisa la Efeso, lakini baada ya miaka 40 ya kuufurahisha moyo
wa Mungu, likajikuta likipokea barua ya onyo kuwa, “limeuacha upendo wake wa kwanza.” Ufunuo 2:4.
Wema wa Sauli katika kipindi chake cha
kujiweza, tunaweza kuuona kwa uwazi, tangia siku ile alipokutana na
kusudi lake la maisha la kuliongoza taifa la Israeli. Badala ya kuandaa
sherehe ya kuteuliwa kwake, aliingia mafichoni kama dalili ya ku jiona
kutoistahili nafasi hiyo. 1 Samweli 10:21-22. Wema huu
wa Sauli ambao ndio tunaouita kuupendeza moyo wa Mungu, unaonekana pia
kwa kuuangalia uhusiano wa awali kati yake na Samweli. Samweli katika
miaka tuliyo nayo, tunaweza kumlinganisha na mchungaji wa kanisa la
mahali. Ukiuangalia uhusiano huo, unaweza kuona kuwa, kila mara Sauli
alipotaka kufanya jambo fulani kubwa litakaloamua mwelekeo wa maisha
yake au wa taifa lake, alitafuta kwanza, ushauri kutoka kwa Samweli.
Tabia hii ya Sauli, katika kuupendeza moyo
wa Mungu ndiyo inayotawala karibu kwa kila mtu, pale anapotoka kumpokea
Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Katika siku hizi za kwanza za
wokovu, ni vigumu kumwona mwamini anayekwenda kinyume na mchungaji wa
kanisa lake la mahali. Kila mara katika kipindi hiki, utamkuta mchungaji
akiwa mbele, huku waamini wapya kama kondoo, wakiwa nyuma yake
wakimfuata popote anapokwenda. Ni baada ya kipindi fulani cha
kuufurahisha mchungaji wa Mungu, ndipo waamini hawa wanapoanza
kusikiliza sauti za ‘wachungaji wapitaji’, kuliko ile ya mchungaji wao.
Katika hili, nakumbuka kikao kimoja
nilichokifanya na baadhi ya waamini waliokomaa katika kanisa fulani la
mahali. Katika kikao hicho, mwamini mmoja alisimama, na kudai kuwa,
alielezwa maneno fulani na mshirika mwingine, ambayo ndiyo yaliyozaa
kikao hicho. Katika kikao hicho ulionekana umuhimu wa kumtaja mtu huyo,
ili kulimaliza jambo hilo kwa njia inayofaa. Cha kusikitisha ni kuwa,
mwamini huyo alikataa kata kata, kumtaja mtu huyo, licha ya kutakiwa
kufanya hivyo na mchungaji wake. Kitu kilichoonekana katika kikao hicho,
ni kuwa ndugu huyu, alikuwa ameamua kumhifadhi mtu huyo badala ya
kumhifadhi mwakilishi wa Mungu katika kanisa ambalo yeye ni mshirika
wake. Tabia iliyoonyeshwa na ndugu huyu, haikuwepo katika siku za awali
za kuokoka kwake. Ni baada ya miaka kadhaa ya kuupendeza moyo wa Mungu,
ndipo mazoea yalipopata nguvu ndani yake na kumfanya asienende sawa na
uongozi wa kanisa lake la mahali.
Tabia iliyoonyeshwa na mwamini huyu, ya
kuwaogopa wanadamu kuliko kumwogopa Mungu, ndiyo iliyochangia kumfanya
mfalme Sauli kumaliza vibaya kipindi cha mwisho cha maisha yake. Mara
kwa mara alipofanya kinyume na mchungaji wa kanisa lake (Samweli), jibu
lake lilikuwa, “Naliwaogopa wale watu.”1 Samweli 10:21-22. Kile
kinachoonekana hapa ni kuwa, maaskari wa Sauli hawakufurahishwa na
maneno waliyoambiwa na Sauli ya kuteketeza nyara zote zilizopatikana
katika vita yao na Waamaleki. Kwa maneno mengine, mfalme Sauli alijikuta
akiwa katika ‘ulimbo’ wa ama kumfurahisha Mungu au kulifurahisha jeshi
lake. Kwa kuwa mauti ya aibu ilikuwa tayari imeanza kusafiri ndani yake,
Sauli alichagua kuwafurahisha wanadamu!
Tukirudi huko nyuma, tunaweza kuona kuwa,
kuwaogopa wanadamu ndiko pia kulikomkosesha Haruni, pale
alipowatengenezea wana wa Israeli ng’ombe wa dhahabu wa kuwaongoza
kuwarudisha katika nchi ya Misri. Kutoka 32:21-25
Ninachotaka ukione katika kipengele hiki ni
kuwa, Mungu amekuleta duniani ili utafute kusudi la kuishi kwako na
kuweza kulitumikia kwa bidii. Ili uwe na mwisho mwema, mara tu baada ya
kutambua kusudi la maisha yako, ni vema uhakikishe kuwa, unalitumikia
huku ukimpendeza Mungu badala ya kuwapendeza wanadamu. Uamuzi huu
utakapokuwa chaguo lako la kwanza, wale watakaofanikiwa kuona kipindi
cha mwisho cha maisha yako, watafungua vinywa vyao na kusema, “hakika mtu huyu alikuwa mwenye haki!”Luka 23:47
SHIKAMANA NA NENO LA MUNGU
I Samweli 13:14; 15:1-3, 8-9
Katika kuyaangalia maisha ya Sauli,
tunaweza kusema kuwa wakati fulani katika kipindi chake cha mwisho,
neema ya Mungu ilikuwa juu yake kiasi cha kumfanya aisikie mara kwa mara
sauti ya Mungu, aliye hai. Katika kulifanikisha kusudi la maisha yake,
Mungu alimtokea kwa namna moja au nyingine na kumpa majukumu na jinsi
ya kuyafanya majukumu hayo. Hata hivyo pamoja na kusikia huku, aliishia
kuwa na mwisho wa kuaibisha kwa kule kutokuwa mtendaji wa yale
aliyoyasikia. Mara zote Mungu anaposema wanadamu, hufanya hivyo ili
mwanadamu aweze kukitendea kazi kile alichokisikia. Ni katika hili,
Biblia inasema wazi kuwa, “tusiwe tu wasikiaji wa neno bali tukawe pia watendaji wa neno.” Yakobo 1:22.
Ushindi wa mtu kamwe hautatokani tu na yale
anayoyafahamu, bali hutokana na yale anayoyafahamu na kuyatenda!
Kukosekana kwa tabia hii ya kuwa mtendaji wa neno, ndiyo iliyomfanya
mfalme Sauli akutane na kifo cha aibu katika mlima wa Gilboa. Mwamini
yeyote anayetaka kumaliza kwa ushindi sehemu yake ya mwisho ya maisha
yake, anatakiwa afanye kinyume na kile kilichofanywa na mfalme Sauli,
kwa kuwa mtendaji wa neno la Mungu.
KUTOOGOPA SHAMRASHAMRA KATIKA KAMBI YA ADUI
“Samweli akasema, Umefanya nini? Naye
Sauli akasema, Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali
nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa, NAO WAFILISTI WAMEKUSANYIKA
PAMOJA HUKO MIKMASHI.” 1Samweli 13:11
Jambo lingine lililochangia kifo cha aibu
kwa mfalme Sauli, ni hili lililoandikwa katika andiko letu hapo juu.
Kabla ya andiko hili, kulikuwa na matayarisho makubwa ya vita baina ya
Israeli na mahasimu wao wakubwa, taifa la Wafilisti. Habari za vita hii
zilipomfikia Samweli, alimtahadharisha Sauli asiingie vitani, hadi pale
atakapokuja kuongoza ibada ya kumtolea Mungu dhabihu. Ni wakati wa kutoa
dhabihu hii, ndipo Mungu anapoongea pia kuhusiana na vita iliyokuwa
ikilikabili taifa lake. Kweli Sauli alingojea muda wa siku saba kama
alivyoahidiwa na Samweli, ila kwa sababu ambazo hazikubainishwa katika
neno la Mungu, Samweli alichelewa kufika.
Wakati Sauli alipokuwa katika
kuchanganyikiwa kutokana na mtumishi wa Mungu kuchelewa, wapelelezi
walimjia kumweleza vile maadui walivyokuwa wakijikusanya katika eneo la
Mikmashi. Taarifa hizi zilizua mtafaruku mkubwa sana katika kambi ya
Israeli na hakukuwa na Kalebu wala Joshua wa kuwatia maaskari wa Sauli
moyo! Hesabu 14:1-10. Kile kinachoonekana hapa ni kuwa, baada ya taarifa
hizi, wapiganaji wa Sauli, walimshauri kutoendelea kumngojea mtumishi
wa Mungu. Hapa tena mfalme Sauli akajikuta katikati ya ulimbo wa mambo
mawili, kudharau kile kinachofanywa na adui na kuendelea kumngojea
Samweli, ama kuogopa maadui na kuacha kuitii sauti ya Mungu. Yeye kama
ilivyokuwa kwa Haruni, aliamua kuwaunga waasi mkono na kuacha kuendelea
kuitii sauti ya Mungu.
Somo ambalo Sauli alitakiwa kujifunza
wakati huu wa kujaribiwa kwa imani yake, ni kuwa, yeye ni mpakwa mafuta
wa Mungu, mwenye neno kutoka kwa Mungu lililomtaka kumngojea mtumishi wa
Mungu. Mtu aliyeitwa na Mungu na wakati huo huo, akawa na neno la Mungu
ndani yake, hatakiwi kuogopeshwa na kile kinachotendeka katika kambi ya
maadui. Sauli akapoteza alama za ushindi kutokana na uasi uliotokana na
kuogopa maadui.
Kile kilichomwangusha Sauli katika
kipengele hiki, ndicho kinachowaangusha watoto wa Mungu katika kanisa la
siku hizi za mwisho. Waamini wengi hushindwa kuendelea kushikamana na
neno la Mungu, kutokana na kuchelewa au kutokuja kabisa kwa yale
waliyoyatarajia kutoka kwa Mungu. Kama ilivyokuwa kwa Sauli, wakati
hitaji la mtu linapoonekana kukawia, ndipo maadui wa msalaba nao,
wanapopata nafasi ya kupanga mashambulizi dhidi ya imani na utii wa
mwamini. Mwamini yeyote yule anayetaka kumaliza vema sehemu ya mwisho ya
maisha yake, anatakiwa avue kabisa woga wa kuogopa yale yote
yanayofanywa na adui kwa ajili yake. Afanye hivi huku akikumbuka kuwa,
“kila silaha itakayoundwa na adui dhidi yake, haitafanikiwa.” Isaya
54:17
HESHIMU HUDUMA ZA WENGINE
“Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka
ya kuteketezwa na sadaka ya amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa. Hata
mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe Samweli
akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu.” 1 Samweli
13:9-10
Katika andiko letu hapa juu, tunakutana na
jambo lingine, lililochangia kuudhoofisha mwisho wa mpakwa mafuta huyu
wa BWANA. Tunapoliangalia taifa la Israeli kama taifa teule la Mungu
katika agano la kale, tunaona vile Mungu, alivyokuwa akiwaita watu na
kuwapa majukumu na huduma mbalimbali. Ugawaji huu wa majukumu kwa uwazi
ulianzia Jangwani, wakati Mungu alipowaagiza wana wa Israeli kutengeneza
mahali atakapokutania nao. Kuanzia wakati huo, wako walioitwa na Mungu
kuwa makuhani, waimbaji, wabebaji wa hema, wenye kubeba vyombo vya hema
na kadhalika. Baada ya kuingia katika nchi ya Ahadi, utaratibu huu
uliendelea kutumika kwa kumweka Sauli kuwa mfalme katika taifa na
Samweli kuwa kuhani. Kutokana na ukweli huu, yako mambo yaliyotakiwa
kufanywa na mfalme na yako yale yaliyotakiwa kufanywa na kuhani. Kwa
utaratibu huu, lilikua kosa kubwa pale alipotokea mtu wa kuingilia
majukumu ya mtu mwingine.
Andiko letu hapo juu linatuonyesha kuwa,
pamoja na Sauli kuuelewa mgawanyiko huu, bado aliamua kuteketeza dhabihu
kwa ajili ya Mungu, huduma iliyopaswa kufanywa na Samweli. Inawezekana
baada ya Samweli kuchelewa, Sauli aliangalia lile zoezi zima la kutoa
dhabihu na kusema, “si hivi tu, hata mimi naweza kufanya!” Kile
tunachojifunza hapa ni ile hatari inayoweza kumpata mwamini ambaye kwa
makusudi na kwa msukumo mbaya, anayeamua kutoka katika wito wake na
kuingilia wito au huduma isiyo yake.
Katika hili nakumbuka kisa nilichoelezwa na
rafiki yangu, kinachomhusu rafiki yake aliyeamua kuacha huduma ya
uchungaji na kuingilia ile ya uinjilisti, eti kwa vile huduma ya
uchungaji, haina pesa! Hali hii inaonekana pia kwa watumishi ambao hapo
mwanzo walikuwa wabeba maono, ila baadaye wakayageukia maono ya watu
wengine kutokana na tamaa ya pesa. Leo hii vibao vya majina ya huduma
nyingi vinagezwa mara kwa mara, kutokana na wahudumu kutangatanga
kihuduma kutokana na kutamani mapato ya aibu.
Wakati mwingine roho hii ya kutoziheshimu
huduma za watu wengine, ndiyo inayowasukuma watumishi walio na majukumu
makubwa kwenye kanisa, kuamua kutafuta kutumika katika nafasi katika
ofisi za kisiasa. Katika hili ni vema tuelewe kuwa, watumishi wa Mungu
wako katika makundi makubwa mawili. Wako walioitwa katika utumishi ulio
rasmi wa moja kwa moja, na wako wale wanaomtumikia Mungu kupitia muda
wao wa ziada baada ya kukamilisha majukumu yao ya kazi ya kila siku.
Nafsi za kisiasa nazo ziko za aina mbili, ziko nafasi zinazodaia
asilimia mia ya muda wa mtu na ziko zile zinazodai sehemu tu ya muda wa
mtu. Kwa mfano, nafasi za urais, ufalme, uwaziri… ni miongoni mwa nafasi
zinazodai asilimia mia za muda wa mtu. Wakati nafasi kama zile za
udiwani, ubunge na mjumbe wa shina, zinadai sehemu tu ya muda wa mtu.
Mtu aliyeitwa kumtumikia Mungu moja kwa moja (full time), atakuwa
anaingilia huduma ya wengine, pale atakapokubali nafasi ya kisiasa
itakayogharimu asilimia mia ya muda wake.
Ili hali hii ya kuingilia huduma za watu
wengine isitokee bila kukusudia, yako mambo mawili yanayotakiwa kufanywa
na waamini. Kwanza, wanatakiwa waelewa kile walichoitiwa kukifanya
katika kuishi kwao chini ya jua. Ili kuelewa nafasi ya kitumishi katika
familia ya Mungu, baada ya kuokoka, mwamini anatakiwa atafute kanisa
litakalomlea kiroho na kumkuza kiimani. Sambamba na kutafuta kanisa
litakalomtunza, anatakiwa awe na huduma anayoifanya katika kanisa hilo.
Kuokoka bila kuwa na kanisa la kumlea mtu na kutokuwa na wajibu wowote
katika kanisa la mahali, ni kusihi katika ukengeufu.
Jambo lingine litakalozuia kuingiliana
kihuduma, ni pale kila mwamini atakapotambua kuwa, kamwe hajaitwa na
Mungu kufanya kila kitu. Kila mwamini ameitwa ili kufanya huduma fulani
itakayosaidia kumjenga mwingine, hali kadhalika waamini wengine wameitwa
kufanya mambo yatakayosaidia kumjenga. Mwamini akishauelewa wajibu wake
ndani ufalme wa Mungu, anatakiwa kudumu katika huduma hiyo hadi pale
mapenzi ya Mungu kwake kuhusiana na huduma hiyo, yatakapokamilika. Kama
atakuwepo mwamini wa kuacha huduma aliyoitiwa kwa kuongozwa na msukumo
mbaya, atapoteza pia neema ya Mungu iliyokusudiwa kumuumbia mwisho ulio
na nushindi. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa mfalme Sauli, alimalizia
vibaya, pale alipokubaliana na msukumo usio wa Kimungu kufanya huduma
isiyo yake.
Kama wa Mungu wa siku hizi za mwisho
wanataka kuwa na mwisho mzuri, wanatakiwa kudumu katika huduma
walizoitiwa pamoja na kuheshimu huduma zinazofanywa na wengine.
KUTOKUBALI JESHI LA MUNGU LILITUKANWE
“Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane.” 1 Samweli 17:10
Jambo lingine lililomfanya mfalme Sauli
kuwa na mwisho wa aibu, ni ile hali yake ya kukaa kimya wakati adui
alipoyatukana majeshi ya Mungu aliye hai. Ili kukielewa kipengele hiki,
naomba ufuatane nami mpaka kwenye eneo la Soko, mahali majeshi ya
Israeli na Wafilisti, yalipokuwa yamejipanga kwa vita. Neno la Mungu
linapoelezea juu ya vita hii, linasema kuwa, katika kilima kimoja
yalisimama majeshi ya Israeli, na katika kilima kingine jeshi la
Wafilisti.
Kwa kuwa ulimwengu unaoonekana uko sambamba
na ule usioonekana, nyuma ya kila kilima, kulikuwa na nguvu za kiroho
zilizokuwa zikitumainiwa na majeshi haya. Kwa upande wa Wafilisti
alikuwepo mungu wa kipagani aitwaye Dargoni, na katika jeshi la Israeli,
alikuwepo Yahwe Mungu, muumba wa mbingu na nchi. Kutokana na mwonekano
huu, kitendo cha Goliathi cha kulitukana jeshi la Israeli, moja kwa moja
kililenga kumtukana Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Ukweli huu ndio
uliomsukuma kijana Daudi kutamka maneno yafuatayo; “Atafanyiwaje
yeye atakayemwua Mfilisti huyu, na kuwaondoalea Israeli aibu hii? Maana
Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu
aliye hai?” 1 Samweli 17:26. Ninachotaka ukione hapa ni kuwa, kuna hasara kubwa sana pale tunapokaa kimya wakati Mungu wetu anapotukanwa na adui.
Kuna njia kuu mbili zinazotumiwa na adui
kumtukana Mungu. Njia ya kwanza, ni ile ya kutamka maneno mabaya dhidi
ya Mungu au dhidi ya chochote kile kilicho mali ya Mungu. Hata kusema
kinyume na neno la Mungu, nako ni kumtukana Mungu. Kwa mfano, nyoka
alipomjia Eva na kulikanusha neno la Mungu, hilo lilikuwa tusi mbele za
Mungu. Njia ya pili, ni ile ya kutenda kinyume na neno la Mungu. Mtume
Paulo alipokuwa akivielezea vitendo vilivyo kinyume na neno la Mungu,
aliandika yafuatayo:- “Matendo ya mwili….. Wagalatia 5:19-20.
Mwamini anayeweza kumaliza maisha yake kwa
ushindi, ni yule anayejifunga mkanda na kukabiliana na upotofu wa aina
yoyote ile, uwe katika maneno au katika matendo. Katika hili,
hatuzungumzii kuchukua mapanga au mabomu na kuanza kuangamiza watu.
Mungu aliye hai, ni mtoa uzima hivyo haungwi mkono kwa njia hii. Ni
Shetani peke yake ndiye anayehitaji kuungwa mkono kwa njia hii, maana, “Yeye ndiye anayekuja kwa lengo la kuiba, kuchinja na kuharibu.” Yohana 10:10. Mungu
aliyeumba mbingu na nchi ana uweza wa kipekee, usiohitaji kutetewa kwa
njia yoyote ile. Kutokana na ukweli huu, pale tunapoona jina lake
likitukanwa, tunachotakiwa kufanya, ni kufanya yale yatakayomponya yule
aliyemtukana Mungu, badala ya kumwangamiza mkosaji.
Sauli alipoteza alama za ushindi, pale
alipokaa kimya na kumwachia adui aendelee kulitukana jina la BWANA wa
majeshi. Katika hili si kwamba alifurahia kuona jina la Mungu wake
likitukanwa, ila hofu ya kifo, ndiyo iliyolegeza viungo vyake. Daudi
yeye kama mwamini mwenye kiu ya kumaliza mwendo kwa ushindi, naye
alisikia matusi ya adui, ila yeye akachagua kupambana, badala ya kukaa
kimya.
Kile Mungu anachotafuta wakati huu ambao
jina lake linatukanwa kuliko vipindi vyote vilivyowahi kuwepo katika
historia mwanadamu, ni kupata wanawake na wanaume, watakaoamua
kukabiliana na adui pale atakapoinuka kulitukana jeshi lake. Aina hii ya
waamini watapatikana pale, kanisa la Mungu litakapojivua roho ya hofu
iliyokuwa kwa Sauli na kuvaa roho ya ujasiri iliyokuwa ndani ya Daudi.
Kwa yule atakayechagua fungu la Daudi badala ya lile la Sauli, huyo
atakuwa na heri katika kumaliza maisha yake hapa duniani.
KUIKATAA ROHO YA HUSUDA
“Basi Sauli akaghadhibika sana, na
maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi
wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezacho kupata, isipokuwa ni ufalme.
Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.” 1 Samweli 18:8-9
Andiko hili, linaonyesha mabadiliko makubwa
yaliyomtokea Sauli baada ya kipindi kifupi tu cha kutawala kwake. Yeye
aliyeenda mafichoni huko mwanzo ili asitawazwe kuwa mfalme juu ya
Israeli, sasa anahofia kuipoteza nafasi hiyo. Hii ndiyo hatari
inayowakabili wanadamu wote wanaoishi chini ya jua, wanaanza vizuri, ila
baada ya kitambo fulani, wanayafanya chakula mambo ambayo hapo awali,
yalikuwa matapishi kwao.
Katika hili, namkumbuka yule shujaa wa
injili, aliyeishi nchini Marekani katika karine ya 19. Mwanzoni mwa
huduma yake watu walipomjia na kumpa cheo cha utume, yeye (Alexander
Dowe) alikataa na kusema kuwa, si mtume na hata hastahili kulegeza
gidamu za viatu vya mitume wa Bwana. Hata hivyo jinsi alivyozidi
kutumiwa na Mungu, ndivyo mabadiliko yasiyofaa yalivyojitokeza katika
maisha yake. Historia ya maisha yake inaoonyesha kuwa, wakati wa mwisho
wa maisha yake, si tu alikubali kuwa yeye ni mtume, ila alienda mbali
zaidi kwa kudai kuwa, yeye ndiye Eliya ajaye! Tunachojifunza hapa ni
kuwa, kipindi cha mwisho cha maisha ya mtu, ni cha hatari kuliko kile
cha mwanzo cha maisha yake.
Wivu ulio na sumu ndani yake, kitu kibaya
mno ndani na nje ya ufalme wa Mungu. Wafalme na watumishi wengi,
wamepoteza heshima zao na kumaliza mwendo kwa aibu, kutokana na kuruhusu
uovu huu katika maisha yao. Sisi kama waamini wanaoishi siku za ufahamu
mkubwa wa kumjua Mungu, tunatakiwa kumpinga Shetani pale anapotusogeza
karibu na roho hii ya husuda. Kwa kuwa husuda ni jambo lililo kinyume na
mapenzi ya Mungu, ni lazima tujivue roho hii ili tuwe na mwisho uliojaa
neema na amani ya Mungu.
KUKATAA MSAADA WA ADUI
1Samweli 28:4-6; 3:1,13
Baada ya kuyapitia maandiko yetu hapo juu,
napenda tujikumbushe pia juu ya nafasi ya imani katika maisha yetu ya
kila siku. Biblia kwa upana imesema wazi kuwa, mwenye haki ataishi kwa
imani na imani uja kwa kusikia neno la Kristo. Habakuki 2: 4, Waebrania 10:38, Wagalatia 3:11, Warumi 10:17.
Kutokana na maandiko haya, kama hakutakuwa na kusikia kutoka kwa Mungu,
hakutakuwa na imani na imani inapokosekana, hakutakuwa pia na maisha au
maendeleo ya kiroho.
Hapo mwanzo tuliona vile mfalme Sauli
alivyokuwa akiongea mara kwa mara na Mungu kuhusiana na wito aliomwitia
wa kuliongoza taifa lake. Ni pale tu alipoiruhusu dhambi kuyatawala
maisha yake, hapo ndipo Mungu alipoacha kuzungumza naye. Hali hii ya
ukimya wa Mungu katika maisha yake, ilimwingiza katika makosa zaidi,
pale alipoenda kuomba msaada kwa mwanamke mchawi, kama andiko letu hapo
juu linavyoonyesha. Hapo zamani mwanamke wa jinsi hii alikuwa ni adui
kwake, ila sasa katika kudhikika kwake, anaamua kutafuta msaada kwake.
Kama kuna mambo yanayomchukiza Mungu ni
pamoja na hili la kuwaona watoto wake, wakienda kutafuta msaada katika
kambi ya maadui. Angalia, kitendo cha Sauli cha kutafuta msaada kwa
adui, bado hakikuweza kuubadilisha mwisho wake, sana sana kilizidi
kukifyeka kilele cha maisha yake. Mwamini anayetaka kumaliza mwendo wake
vema, anatakiwa kuikwepa roho hii ya kukimbilia kwa adui kuomba msaada
wakati wa taabu.
KUWA NA UVUMILIVU USIO NA MWISHO
I Samweli 13:6-9
Katika kuiangalia historia ya maisha ya
Sauli, tunaweza kuona kuwa ni mtu aliyeshindwa pia katika mtihani wa
uvumilivu. Alivumilia pale adui alipokuwa mbali naye, ila alipoanza
kusikia vishindo vya magari ya vita, alipoteza uvumilivu wake. Katika
hili mfalme Sauli anawakilisha mamilioni ya waamini, wasiofahamu maana
halisi ya kuvumilia. Mara zote uvumilivu wa mtu huwa haupimwi katika
njia iliyo tambarare, ila hupimwa pale kila kitu katika maisha ya mtu
kinapoonekana kwenda shaghala baghala. Mara zote mtu anapoyaruhusu
makucha ya adui kuushinda uvumilivu wake, ni wazi hata hatua
itakayofuata, ni kuingia katika mwili na kupoteza ushindi katika maisha
yake. Mwamini anayeweza kuishi maisha ya ushindi na kuwa na mwisho
mwema, ni yule atakayeulinda uvumilivu wake wakati wowote na katika hali
zote. Yesu alipoelezea juu ya thawabu ya uvumilivu alitamka wazi kuwa, “atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokoka.” Mathayo 24:13
Omba maombi yafuatayo:- Mungu nisaidie ili niyatende yale yote yatakayoniwezesha kumaliza mwendo kishujaa. AMENI!
Edited by Apostle Darmacy
|
---|
There is greatness inside of you
I believe that there is a seed of greatness in all human beings. Therefore the aim of my blog is to bring to my readers awareness of things that are happening around us. I will focus majorly on inspirational news that can motivate my readers to doing more with their lives too. If you are too busy to get acquainted with what is in the newspapers or you have read the papers but have not felt any inspiration or motivation, please log on this page and be inspired to walk in your purpose and dream.