Thursday, February 23, 2017
MAGAZETI YA LEO IJUMAA FEBRUARY 24,2017
- Next You are viewing Most Recent Post
- Previous Denice Simeo Youth Development Expert atoa ushauri kwa vijana wa chuo
google+
There is greatness inside of you
I believe that there is a seed of greatness in all human beings. Therefore the aim of my blog is to bring to my readers awareness of things that are happening around us. I will focus majorly on inspirational news that can motivate my readers to doing more with their lives too. If you are too busy to get acquainted with what is in the newspapers or you have read the papers but have not felt any inspiration or motivation, please log on this page and be inspired to walk in your purpose and dream.
WAJIBU WA MTU ALIYEOKOKA
Na Apostle Darmacy
Utangulizi:
Kutokana na wingi wa watu walioko duniani
kwa sasa pamoja na bidii ya kanisa katika kutumia tekinolojia mpya za
mawasiliano kuwafikishia wenye dhambi injili, ni wazi ulimwengu tulio
nao, una idadi kubwa ya waamini kuliko nyakati zilizotangulia katika
historia ya kanisa. Hata hivyo, uwingi huu, bado hauendani na hali
halisi ya idadi ya watu walioko duniani na uwezo wa kanisa katika
kuwafikia wenye dhambi. Dunia kwa sasa ina watu zaidi ya bilioni sita na
wakati huo huo, wafuasi wa kweli wa Kristo wakiwa pungufu ya milioni
500.
Tunapoiangalia idadi hii, tunaweza kuona
kuwa haiendani kabisa na nguvu kazi iliyopo ndani ya kanisa
inayojumuisha watu, uwezo wa kifedha, ufahamu na vitendea kazi.
Kutofautiana huku kunaonyesha wazi kuwa kuna kasoro ya kitabia na
utendaji kwa waamini wa kanisa la siku za mwisho. Kasoro hii inaonyesha
kuwa, wengi wa waamini wako ndani ya wokovu ila hawafahamu wajibu walio
nao ndani na nje ya kanisa la Kristo. Ili kulipunguza tatizo hili au
kulimaliza waamini kama mwili wa Kristo, wanatakiwa waelewe kwa kina
kile wanachotakiwa kukifanya ndani na nje ya kanisa baada ya kumpokea
Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao.
Huduma za msingi zinazopaswa kufanywa na waamini ni pamoja na hizi yafuatayo:-
KUOMBEA VIONGOZI WA SERIKALI
“Basi, kabla ya mambo yote, nataka
dua, na sala, na maombezi, na shukrani; zifanyike kwa ajili ya watu
wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya
utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni nzuri, nalo
lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote
waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.” 1 Timotheo 2:1-4
Wajibu wa kwanza unaopaswa kufanywa na
waamini baada ya kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha
yao, ni huu wa kuombea viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali.
Maombezi haya yahusishe uongozi wa serikali za mataifa yaliyo na nguvu
za kiuchumi na kijeshi kuliko mengine chini ya jua. Kwa mfano, bajeti za
mataifa mengi yaliyo chini kiuchumi, yanategemea kwa kiwango kikubwa
misaada ya mataifa haya yaliyo na nguvu kiuchumi. Kutokana na ukweli
huu, kama uongozi wa serikali za mataifa makubwa utayumba, uchumi wa
mataifa machanga utayumba pia.
Katika andiko letu hapo juu, mtume Paulo
anamwagiza Timotheo kuwafundisha waamini kuwatanguliza viongozi wa
serikali mbalimbali katika maombi, kwa kutumia neno ‘kabla ya mambo
yote.’ Neno kabla ya yote hapa, ni sawa na kusema, kabla ya kujiombea au
kabla ya kuwaombea wengine, ombea kwanza viongozi wa serikali katika
ngazi mbalimbali. Kama nilivyotangulia kusema, maombi haya yaguse
ulimwengu mzima, ukianzia na viongozi wa serikali ya nchi yako, serikali
za mataifa yanayoizunguka nchi yako, bara lako na ulimwengu kwa ujumla.
KUOMBEA VIONGOZI WA KANISA
“Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.” Matendo 12:5
Kama vile wazazi walivyo wa thamani katika
maisha ya watoto wa kimwili, viongozi wa kanisa (la kiulimwengu na lile
la mahali) nao, ni wa muhimu sana katika maisha ya waamini. Viongozi
hawa ndio wanaoandaa na kuratibu malezi ya waamini kuanzia hatua ya
uchanga hadi kukomaa kwao. Hali kadhalika, viongozi hawa kwa kiwango
kikubwa ndio wanaosababisha baraka za kiroho na za kimwili za waamini.
Kutokana na nafasi ya viongozi katika kanisa la Kristo, kila mwamini
anatakiwa kuwa na bidii kuwaombea. Kwa kuwa kila mwamini amepandikizwa
katika kanisa fulani la mahali, wajibu huu wa kuwaombea viongozi
unatakiwa uanzie Yerusalemu ambayo ni kanisa lake la mahali.
Katika andiko letu hapo juu, tunaona kuwa
waamini wa kanisa la kwanza walikuwa kielelezo kizuri katika hili. Wao
walitambua kuwa, kama adui ataelekeza mshale mmoja kwa mwamini wa
kawaida, kwa kiongozi ataelekeza mishale saba. Kwa kulielewa hili,
walijijengea tabia ya kuwaombea viongozi wao kwa bidii. Umuhimu wa
kuwaombea viongozi umeelezewa pia katika nyaraka mbalimbali
zilizoandikwa na Mitume. Mara kwa mara katika nyaraka hizo, neno la
Mungu linawakumbusha waamini kuweka bidii katika kuwaombea viongozi
katika kanisa. 2Timotheo2:1-2, 1Thesalonike 5:25; 3:1, Waebrania 13:18, Yakobo 5:16. Waamini
wasipoelewa umuhimu wa kuuombea uongozi unaowatunza, Ibilisi atapata
nafasi ya kuushambulia uongozi huo na kuharibu malezi yao.
Kuhusiana na kile kinachoweza kutokea pale
waamini wanapowaombea viongozi wao, nina mfano halisi unaohusu muujiza
ulionitokea nilipokuwa nikirejea nyumbani, baada ya kukamilisha huduma
katika kijiji kimoja cha mkoa wa Pwani, mwaka 2005. Kabla ya safiri
hiyo, mama mmoja katika kanisa alihimizwa na Roho wa Mungu kuniombea.
Wakati wa kurejea nyumbani, ‘boneti’ ya gari nililokuwa nikiliendesha
ilifunguka na kufunika kioo cha mbele. Kwa kuwa ulikuwa usiku wenye mvua
kali, gari iliserereka huku na huko na kimiujiza likasimama tena
barabarani! Jambo la kumshukuru Mungu ni kuwa, wakati huu wa kuserereka,
hakukuwa na gari lolote lililopita katika barabara ile. Wakati wa
kushuhudia kisa hiki kanisani, Roho Mtakatifu alikumkumbusha yule mama
juu ya maombi aliyoyafanya kwa ajili yangu!
Kama wewe u mwamini ila ulikuwa hujaona
umuhimu wa kuwaombea viongozi wa kanisa, unatakiwa kuanza kufanya hivyo
kwa bidii. Anza kwa kuwaombea viongozi wa kanisa linalohusika kukulisha
na kukulea kiroho na kisha gusa viongozi wa sharika zingine katika mwili
wa Kristo. Taja katika maombi yako viongozi wa kanisa katika mabara ya
Ulaya, Asia, Afrika, Amerika Kaskazini na Kusini na Australia na
Newzeland. Ukizembea katika hili, utapoteza baraka za Mungu katika
maisha yako ya kiroho na yale ya kimwili.
KUTEGEMEZA VIONGOZI
Sambamba na kuwaombea viongozi wa kanisa,
waamini wanao wajibu wa kutegemeza viongozi wa kanisa kihali na mali.
Kama tulivyoona katika kipengele cha kuombea uongozi, kutegemeza
viongozi kunatakiwa kuanzie kwa kanisa la mahali na baadaye kusambae kwa
viongozi wa kanisa wa mabara yote. Ni kweli katika makanisa mengi
viongozi wanapewa posho, ila posho hii ya kijumuiya hailengi kumzuia
mwamini kutoa msaada wa kibinafsi. Misaada ya kimwili inayoweza kutolewa
na waamini kwa viongozi wao ni pamoja na chakula, mavazi, nguvu kazi,
ujuzi, pesa na kadhalika. Kama kanisa lina viongozi zaidi ya mmoja, ni
busara kuwabariki viongozi hao kupitia kwa kiongozi wao. Msaada
unaotolewa unaweza kupelekwa kwa mchungaji kiongozi ukiwa na maelezo ya
kule unakotakiwa kwenda.
Waamini wanapokuwa na moyo wa kuwategemeza
viongozi wa kanisa lao la mahali, ni wazi watakuwa tayari kukutana na
mahitaji ya watumishi wengine katika sharika nyingine. Katika
kuwategemeza viongozi, waamini wafundishwe kutoipigia panda misaada yao
pale wanapoitoa. Kwa mfano kama mwamini amempatia kiongozi shati,
asiwatangazie wengine pale atakapomwona kiongozi huyo akiwa amelivaa
shati hilo. Kiongozi peke yake ndiye anayeruhusiwa kutangaza zawadi
aliyopewa na yule aliyempatia zawadi hiyo. Kama kiongozi ataamua
kutangaza zawadi aliyopewa, naye afanye hivyo kwa hekima ili kukwepa
kuifungulia mlango roho ya uroho katika maisha yake. Kamwe asitangaze
alichopewa ili kuwahamasisha wengine, ila afanye hivyo kuonyesha
shukrani yake kwa yule aliyetoa pamoja na kumtia moyo.
MWAMINI AULINDE MWILI WA KRISTO
“…Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.” 1 Wakorintho 12:12-27
Wajibu mwingine wa waamini, ni huu wa
kulilinda kanisa la Mungu. Katika andiko letu hapo juu, mtume Paulo
anawataka waamini watambue kuwa, wao ni viungo vya mwili wa Kristo,
hivyo ndani ya kanisa wako waamini wanaofanya kazi kama mikono, miguu,
kucha, vidole, macho, pua na kadhalika. Kwa kuwa viungo vyote vya mwili
vinashiriki maumivu pale kiungo kimoja kinapoumia, waamini nao ni
wanatakiwa wawe tayari kushiriki taabu za waamini wengine na kuwalinda.
Kuhusiana na ulinzi huu, ni vema kila mwamini ahakikishe kuwa anakuwa
kinyume na kitu au hali yoyote ile iliyo na shabaha ya kumletea mwingine
madhara. Katika hili, waamini wanatakiwa wafuate nyayo za waamini
katika siku za kwanza za kanisa kwa kufunua mipango mibaya iliyoelekezwa
kwa ndugu zao, kabla ya kuleta madhara. Matendo 9:24; 23:12-24.
Sambamba na waamini kulindana wao kwa wao,
wanatakiwa wazidishe ulinzi kwa kiongozi wa huduma au wa kanisa
wanalotumika nalo. Kutokana na kuongezeka kwa harakati za adui za kutaka
kuwaangamiza viongozi wa kanisa, waamini wawe radhi kujitolea kuyalinda
makazi ya viongozi wao mchana na usiku.
KUFANYA KAZI ZA MIKONO KANISANI
Katika ushirika kuna kazi nyingi
zinazohitaji nguvu au ujuzi wa kimwili katika kuzifanya. Kazi hizi
zinaweza kufanywa na waamini kwa kujitolea badala ya kufanywa kwa pesa.
Kazi hizi ni pamoja na uchoraji wa ramani za majengo, kujenga majengo ya
ushirika, kupandikiza maua, usafi, kupanga viti kabla ya ibada, kufuta
vumbi katika viti vya kukalia ibadani, kujenga majukwaa ya mikutano,
kupika wakati wa mikutano, ulinzi na kadhalika. Waamini wafanye hivi kwa
furaha wakijua kuwa, kuna baraka zisizo na kifani katika kufanya hivyo.
Hata kama itabidi malipo fulani yafanyike, malipo hayo yachukue
mwelekeo wa shukrani badala ya mshahara.
Kama waamini watapungukiwa na roho ya
kujitolea katika nyumba ya Mungu, wataanza kuliangalia kanisa kama
mahali pa ajira badala ya kuwa mahali pa kujitolea. Katika hili, uko
mfano ulio hai wa mwamini niliyekutana naye anayetambua umuhimu wa
kujitolea katika mambo yanayouhusu ufalme wa Mungu. Niliutambua moyo
wake pale nilipomwomba kulitengeneza gari langu baada ya gari hilo
kuharibika. Baada ya matengenezo yaliyodumu kwa takribani siku moja,
nilimpa kiasi cha pesa nilichodhania kuwa kinalingana na kazi
aliyoifanya. Baada ya kuzihesabu pesa nilizompa, alinirudishia sehemu ya
pesa zile huku, akisema, “Mchungaji, mbona unanipa pesa zote hizi?!!!” Kama
kanisa la Kristo litakuwa na waamini wa jinsi hii, ni wazi mamilioni ya
mapesa yanayotumika kama malipo, yataweza kutumiwa kuwategemeza
watumishi wanaofanya kazi katika mazingira magumu pamoja na kusaidia
huduma zingine za kijamii.
WAJIBU WA KUSAIDIA MASKINI
“Lakini neno moja walitutakia, tuwakumbuke maskini, nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya.” Wagalatia 2:10
Ukiangalia neno maskini kama linavyoonekana
katika andiko hili, utaona kuwa linamwakilisha mtu yeyote yule
asiyejiweza kiuchumi. Kutojiweza huku kunaweza kutokana na kukumbwa na
majanga ya kiasili, magonjwa, ulemavu wa viungo, vita, kufiwa na
kadhalika. Katika nchi nyingi zilizo nyuma kiustarabu, watu wengi
huamini kuwa swala la kuwasaidia maskini, ni jukumu la serikali au
mataifa yaliyo na nguvu kiuchumi. Dhana hii kwa kiwango kikubwa
inachangia hali ya uwingi wa ombaomba katika mitaa ya nchi hizi.
Tatizo la ombaomba mitaani linaweza
kupungua pale wawakilishi wa Mungu (waamini) watakapojivika tabia ya
kuwasaidia maskini. Misaada kwa maskini inaweza kupelekwa katika idara
za kanisa zinazoshughulikia maskini au katika huduma zinazosaidia
maskini zilizo nje ya kanisa.
WAJIBU WA KUFANYA MAOMBEZI
“Wanafunzi wake, Yakobo na Yohana
walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka
mbinguni, uwaangamize; kama Eliya naye alivyofanya? Akawageukia,
akawakanya. Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo. Kwa maana
Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Luka
9:54-56
Andiko letu hapo juu linaonyesha hali
halisi inayotawala katika kanisa la siku hizi za mwisho. Leo hii badala
ya waamini kuwaangalia wenye dhambi na kuwahurumia, hukimbilia kumwomba
Mungu ili ashushe hasira zake juu yao. Wana wa ngurumo walipoomba kibali
cha kushusha moto wa hukumu, Yesu alikataa kutoa kibali hicho. Wakati
wafuasi wa dini zingine wanapoogopwa kutokana na wepesi wao katika
kumwaga damu za watu walio kinyume nao, Wakristo ni lazima waheshimike
kutokana na bidii yao katika kufuta machozi ya waliao! Jibu la Yesu kwa
wanafunzi wake linaonyesha umuhimu uliopo wa waamini kusimama katikati
ya wenye dhambi na Mungu kwa lengo la kuponya. Katika kuishi chini ya
jua waamini watakutana na mambo mengi yasiyopendeza ndani na nje ya
kanisa, ila katikati ya ubaya huu, zinahitajika rehema badala ya moto
uangamizao. Kila mara waamini wanatakiwa kumwomba Mungu ili awasamehe
wenye dhambi na kuwarehemu.
Maombezi haya yahusishe pia kuwaombea wale
wote wanaojishughulisha katika kuifanya kazi ya Mungu katika mataifa
mbalimbali. Katika hili nafasi ya kwanza itolewe kwa wale wanaomtumikia
Mungu katika maeneo ambako mwili wa Kristo (kanisa) unaendelea kuteseka.
MWAMINI WAMEITIWA KUFANYA UFUASI
“Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja
alishuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya
wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha
karibu ya kufa...lakini Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika
hapo alipo, na alipomwona, alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha
zake, akazitia mafuta na divai, akampandisha juu ya mnyama wake,
akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.” Luka 10:30-35
Andiko hili linazungumzia juu ya wema
uliofanywa na Msamaria kwa mtu aliyeangukia mikononi mwa majambazi.
Tunapofuatilia kisa hiki, tunaweza kuona vile mambo yalivyobadilika pale
Msamaria huyu, alipomfikia mhitaji na kumpa msaada. Tukioanisha andiko
hili na maisha mapya ndani ya Kristo, tunaweza kuona kuwa, mwamini
yeyote yule kabla ya kumpokea Yesu, kwa njia moja au nyingine alikuwa
kama huyu ndugu aliyekuwa ameangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Ni pale
tu yule aliyemwongoza kwa Bwana alipomjia, ndipo hali na mwelekeo wake
vilipobadilika. Hapo awali alikuwa anaelekea Kuzimu ila baada ya
kukubali kuokoka, maungamo yake yalimpatia haki ya kufanyika mtoto wa
Mungu. Yohana 1:12.
Mwamini aliyetendewa wema na mwingine kwa
kuonyeshwa nuru ya injili, anatakiwa awe na utayari wa kuwatendea
wengine mema. Wakati fulani mtu mmoja alitamka kuwa, kufanya ufuasi ni
mapigo ya moyo wa Mungu ndani ya kanisa, hivyo kanisa (mwamini) lisilo
na bidii ya kuwaleta wengine kwa Bwana limekufa.
KUITEGEMEZA KAZI YA MUNGU
Huduma nyingine inayotakiwa kufanywa na
waamini, ni hii ya kuitegemeza kazi ya Mungu kifedha. Katika hili
waamini wanatakiwa kufahamu kuwa, katika ufalme wa Mungu hakuna huduma
iliyo na mtu maalum wa kuifanya. Baadhi ya waamini wanaweza kuwa mstari
wa mbele katika kutegemeza huduma fulani, ila hali hiyo haiwaondolei
wengine nafasi ya kushiriki katika kutoa walicho nacho ili kuitegemeza
huduma hiyo. Waamini wasipoujua ukweli huu, watafanya makosa ya
kuuangalia ushirika kama ushirika wa watu fulani.
Mwamini anapouchukulia ushirika kama mali
yake, atafanya kila analoweza kuutegemeza ushirika badala ya kungojea
mwingine afanye. Kama ushirika utakuwa na hitaji la kupata kiwanja,
jengo, vifaa vya muziki, usafiri, majengo ya shule, posho za watumishi,
kulipia huduma za simu, umeme, tovuti, vipindi redioni na kadhalika,
atajiweka mstari wa mbele kutoa ili kugharimia huduma
inayotakiwa.Tukikutana siku nyingine tutaongea huduma nyingine
zinazopaswa kufanywa na waamini, ila kabla ya wakati huo nakuacha na
amani ya Bwana. Ameni
|
---|
There is greatness inside of you
I believe that there is a seed of greatness in all human beings. Therefore the aim of my blog is to bring to my readers awareness of things that are happening around us. I will focus majorly on inspirational news that can motivate my readers to doing more with their lives too. If you are too busy to get acquainted with what is in the newspapers or you have read the papers but have not felt any inspiration or motivation, please log on this page and be inspired to walk in your purpose and dream.