KIWANGO CHA MUNGU
KUTUNZA KIWANGO CHA MUNGU KATIKA KIZAZI CHETU
Na Apostle Darmacy
UTANGULIZI.
Pamoja na mabadiliko makubwa ya nyakati zetu katika siasa, uchumi
utamaduni (maadili) na kidini. Mungu anacho kiwango chake ambacho ndicho
anakubaliana nacho katika maisha yetu. Ili tuweze kuishi na kufiti
katika mipango na makusudi yake ni lazima tuangalie kukitunza kiwango
cha Mungu katika maisha yetu.
“Kwa kuwa mimi Bwana si kigeugeu (sibadiliki)”
Malaki 3:6
Biblia inaonyesha kuwa tumeitwa na tumfananie Mungu na kamwe si Mungu
atufananie sisi. Kwa hali hiyo kama hali yetu haifanani na Mungu wito ni
sisi kubadilika na wala si Mungu abadilike awe kama tunavyotaka sisi au
rafiki zetu, mazingira yetu au jamii. Biblia huonyesha kuwa sisi
tunabadilishwa toka UTUKUFU hadi UTUKUFU. Mungu anatunza kiwango chake
na kiwango cha Mungu kinakwenda sawa sawa na Neno lake.
Biblia huonyesha mtu hufanana na mawazo yake.
“Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo…”.Mithali 23:7
(Tafsiri ya King James hutumia kufikiri badala ya kuona katika nafsi.)
Neno la Mungu ni mawazo ya Mungu; kwa hiyo linamfunua Mungu vile
alivyo. Ili tumfananie Mungu inabidi tulitafakari Neno lake. Ndipo
litaumba picha ya ki-Mungu katika mawazo yetu. Wala tusifanye
kuifuatisha dunia na kuwaza ya dunia tu.
“Wakuu wa Yuda ni kama watu waondoao alama ya mpaka; nitawamwagia ghadhabu yangu kama maji”
Hosea 5:10
Wito wetu ni kutunza kiwango cha Mungu. Sisi ni vielelezo. Kiwango cha
Mungu kinamtambulisha Mungu wetu katika jamii kama Jehova Nissi. Yaani
yeye ni bendera yetu. Mfano mzuri ni jinsi Musa katika vita dhidi ya
Amaleki alivyonyanyua kiwango cha Mungu (fimbo iliyowakilisha mamlaka ya
Mungu) na hapo Joshua alishinda vita. Watumishi na viongozi wa kiroho
wakinyanyua kiwango hiki ambacho ni neno la Mungu kina Joshua (kanisa)
wanashinda vita. Kiwango kikiondolewa kanisa na taifa hupoteza
mwelekeo. Kutoka 17: 11-15
DOUBLE AGENT
Kuna watu ambao katika ujasusi( upelelezi) hufanya kazi pande zote
mbili huku kila upande ukiamini unafanyiwa kazi wenyewe. Double agent
anakubalika pande zote na hulipwa mshahara na pande zote. Na katika
ujasusi huyu ndiye mtu wa hatari ambaye akipatikana hawezi kusamehewa.
Ndani ya kanisa pia wamo double agents. Kanisa la Laodikia walionywa
kuacha tabia hii mbaya.
“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala moto (wewe ni double agent);” Ufunuo 3:15
Haiwezekani kutunza kiwango cha Mungu kisha ukaonekana kote kote.
Lazima uweke msimamo na dira itakayotambulisha matakwa na kiwango cha
Mungu.
Ni lazima tufike mahali tunamtambulisha Mungu katika kila hatua ya maisha yetu kwa viwango vya
UPENDOwetu,
UAMINIFU, USAFI, UVUMILIVU, UKARIMU, HURUMA, UNYENYEKEVU NA UTII.Sharti
ifikie hatua maisha yetu yanaakisi hali ya Mungu wetu. Hapo tunaweza
kuwa manabii( wasemaji wa Mungu) kwa kizazi chetu. Watu wanaotuona
wapate ujumbe wa jinsi Mungu alivyo na anavyotaka katika maisha yao.
Hatuwezi kuridhia maovu na kuchukuliana na udhaifu wa dunia hii na bado
tutegemee kuwa nuru. Mungu atusaidie kuwa watu wanaosimamia kiwango cha
Mungu katika siku zetu na hapo maisha yetu yatakuwa na faida katika
ufalme wa Mungu.
Mungu akubariki.
Toa Maoni Hapa Chini