Nguvu,Imani na udhirisho wa kimungu kupitia Daud



i


Apostle D
MAMBO YA MSINGI 20 YA KUJIFUNZA KUTOKA KWA HABARI YA DAUDI NA GOLIATHI.
1SAMWELI 16:1-55, NA 18: 1-5.
-
JINA LA YESU lina uwezo mkubwa kuliko majina yote. Daudi akasema
nakujia kwa Jina la BWANA. Tumia jina hilo unapotaka maombi yako yawe na
ushindi.
-
Mawe matano yanawakilisha huduma tano, uchungaji, utume, unabii,
ualimu na uinjilisti. Hawa wote wanatakiwa kuwepo katika kanisa na
kulelewa na mchungaji ndio maana ya Daudi kuweka mawe hayo ndani ya
mkoba wa kichungaji.
-
Daudi alichukua mawe matano pia kwa sababu alipeleleza na kujua
Goliathi ana ndugu wengine wanne wenye mwonekano kama wake (THEOLOGY).
Katika hili tunajifunza kujipanga kwa changamoto za baadaye hata kama
bado hazijafika. Kama leo ni shwari basi jipange kwa ajili ya Kesho. Kwa
lugha ya uchumi tunasema jifunze kuweka akiba.
-
Upako wa Kwanza ulimpa Daudi nguvu ya kujihesabia mshindi hata kabla
ya watu kujua kuwa yeye ni mshindi. Alitafuta kutumia nguvu yake.
Usikae kimya wakati kuna jambo linaharibika na unajua kabisa unao uwezo
wa kuweka mambo kwenye mstari.
-
Ajionavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo. Sauli na majeshi ya
Israeli walijiona wanyonge na dhaifu kwa Goliathi.(walifadhaika na
kuogopa sana) lakini Daudi alijiona kuwa mshindi na kweli akamshinda
Goliathi.
-
Daudi alitumia silaha dhaifu (kombea na jiwe) lakini alishinda,
maana yake hata kama unahisi huna nguvu nyingi, huna pesa nyingi, huna
jina kubwa, huna elimu kubwa, unadharaulika kama Goliathi alivyomdharau
Daudi, Mungu akikutia nguvu, kile kidogo ulichonacho kinaweza fanya
mambo makubwa saana! Efeso 3:20 Mungu hufanya zaidi hata tuwazayo na
tuombayo.
-
Daudi hakutafuta umaarufu, kwa sababu kama angependa umaarufu basi
baada ya kuua dubu na simba angejitangaza lakini alitulia mpaka
alipokutana na Goliathi. Tena hata baada ya kumuua Goliathi ni wana wa
Israel walioanza kumwimbia nyimbo nzuri zaidi ya zile za mfalme. Si yeye
aliyejitangaza. Nia yake haikuwa kujulikana bali kufanya mapenzi ya
Mungu. Usihubiri au kuimba ili tukujue bali fanya kwa ajili ya ujenzi wa
ufalme wa Mungu. Mungu akikuinua hutapata shida ya kujitangaza.
-
Mungu huwainua watu kutoka kiwango kimoja kwenda kingine. Upako
mmoja hadi mwingine. Daudi alipomuua simba na dubu ndipo alipoweza
kumuua Goliathi. Unapotulia na kunyenyekea chini ya Mkono ulio hodari wa
Mungu,basi Yeye atakuinua kwa wakati wake(1Petro 5:6). Muda mwingine
Mungu anaonekana kama anachelewa kwa sababu tunataka kuruka hatua,
katika maisha yako, Mungu anajua hatua unazotakiwa kupita, ukiisha kuua
simba na Dubu Mungu atakuwezesha kumuua Goliathi. Mungu anapotaka
kukuinua lazima aruhusu tatizo ambalo wewe peke yako ndo utakuwa na jibu
lake.
-
Tunajifunza pia kwamba matatizo siku zote yapo tu haijalishi
unafanya kazi gani. Usifikirie kwamba ukiwa mtumishi basi majaribu
yanapungua.ooh, mengi tu. Popote ulipo jifunze kuwa mwaminifu na Bwana
atakuinua. Daudi alikuwa mwaminifu kwa kuhakikisha usalama wa wanyama
malishoni ndipo Mungu akamwamini na kumpa Taifa zima la Israel.
Umeshindwa kuongoza familia yako, utawezaje kuendesha kanisa la watu
mia? Umeshindwa kuongoza idara ya watu 6 unataka kuwa mkurugenzi wa
kampuni ili iweje? Usije sema labda nikioa ndo nitaacha uzinzi, labda
nikipata milioni mia ndio nitaacha wizi, au labda nikibadilishiwa kazi
ndo nitaacha rushwa. HAPANA, tenda kwa uaminifu hapohapo ulipo na Bwana
atakuona.
-
Katika kila jambo, hata kama dunia nzima watasema hili haliwezekani wewe soma LUKA 1:37. “hakuna la kumshinda Mungu”
Ndio maana kaka zake walipomkebehi Daudi, yeye hakujali akamfuata
Goliathi na kumuua. Vikwazo vya mafanikio yako vinaweza kutokea hata
ndani ya familia yako au kwa watu wako wa karibu sana, tena wanaoonekana
wenye uwezo kuliko wewe, hakuna sababu ya kukata tamaa ni mwanzo mwisho
tunasonga mbele. Umetengwa baada ya kumpokea Yesu? Kaza buti songa
mbele mpaka Goliathi atie amri chini.
-
Daudi hakufurahia watu wa Mungu wanapotukanwa. Kama mtu wa Mungu
kamwe usifurahie watu wanapomsema mtumishi wa Mungu vibaya, hata kama ni
kweli katenda uovu, endapo ni mpakwa mafuta wa Bwana kuna utaratibu wa
kuyasema na si kuropoka tu. Kumbuka watu wa karibu ya Musa waliadhibiwa
na Mungu kwa sababu walimsema vibaya Musa japokuwa ni kweli alikosea.
-
Vita kati ya wana wa Israeli na wafilisti vinawakilisha vita vya
watu wa Mungu dhidi ya Shetani na jeshi lake na imetupasa kulishinda kwa
kukaa ndani ya Neno(ujumla wa huduma tano kanisani) na kulitumia Jina
la Bwana.
-
Shetani ana mikwara mingi sana. Anatumia ufahamu wetu kutufanya
tuhisi kwamba yeye anaweza zaidi yetu. Goliathi alitumia muda mwingi
kuwatisha majeshi ya wana wa Israeli, kama ilivyo leo shetani
anavyokutisha kwamba hutapona, hutafanikiwa, utakufa, utachekwa ukiokoka
nk. Daudi hakutishwa kamwe. Unapoiruhusu roho ya hofu ndani yako basi
unafanyika mateka wa Shetani. Tunatakiwa kuangusha ngome za fikra zetu
zipate kutii uwezo wa Jina la Bwana badala ya kuogopeshwa na matatizo.
Tatizo lako ni la muda mfupi tu amini sasa na Bwana atakutokea na
kukushindia.
-
Usijadiliane na adui. Wana wa Israeli walitakiwa kujipanga kuvamia,
kwa mfano wangeamua watu sita wamvamie Goliathi na wengine wavamie jeshi
la wafilisti wangemaliza kelele zote za Goliathi. Kitendo cha
kujadiliana na Goliathi kilimpa Goliathi nafasi ya kuingiza hofu mioyoni
mwao, don’t compromise with devil’s deceptions /techniques.
-
Daudi alivaa nguo za kijeshi lakini akavua baada ya kuona hazimfai.
Maana yake unaweza kujaribu suluhisho/njia za mtu mwingine lakini
haishauriwi kwa sababu Mungu alikuumba wewe original, unapocopy na
kupaste maana yake uwezo wako na wajibu wako unauweka kuwa kipolo na
ufanisi wako unaweza kuwa na matunda kidogo. Japokuwa unaweza usijue
kama matunda yako ni madogo. Usiseme kwa sababu wengi wanasoma sheria au
udaktari basi na mimi lazima nisome, usiseme kwa kuwa wengi wanapinga
Injili basi na mi naogopa kuwa wa tofauti. Mungu alikuumba ukiwa tofauti
kabisa na watu wengine, Mungu huwa hafanyi duplications. Anaumba vitu
vipya. Hata mapacha wa kufanana nao wanatofauti kubwa sana. Mungu ana
kusudi na maisha yako, tafuta kujua na utende vema.
-
Kuwa na umri mdogo si kigezo cha kukuzuia kufanya mambo makubwa ya
ufalme wa Mungu. Daudi alikuwa na miaka 17 wakati anamuua Goliathi.
Alikuwa mtoto wa mwisho na aliyedharaulika (katika sura ya 16 mzee Yese
hakumuhesabu kati ya watoto wake lakini Samweli alisisitiza kama yuko
mwingine ndipo Yese alipoagiza Daudi aitwe kutoka malishoni) lakini
alitoa suluhisho la nchi nzima. Jitambue na kuelewa ni hazina gani Mungu
ameweka ndani yako! Leo kuna milionea wengi tu ulaya ambao wana umri wa
miaka ishirini, hata wewe unaweza kuwa miongoni mwao. Hii ndio sababu
sioni ugumu kufundisha na kuandika masomo ya mahusiano, kwa sababu Mungu
amenifundisha hata kabla sijaoa.
-
Mtu asiyetahiriwa (asiye na agano la Mungu, yaani mganga wa
kienyeji, mchawi, mshirikina, kibaka, mwuaji, na wafananao na hao) hana
uwezo wa kuyatisha maisha yako ukimtegemea Kristo.
-
Daudi akasema asizimie moyo mtu yeyote kwa ajili ya huyu, mimi
mtumishi wako nitakwenda kupigana na mfilisti huyu. Nami nakuambia leo
usizimie moyo kwa ajili ya jambo hilo (Ukosefu wa ajira, ugonjwa,
fitina, umasikini nk) maana katika yote tunaye atushindiaye, Kristo
atayamulika mapito yako na kukushika kwa mkono wake wa kuume pale tu
utakapoamua kumwamini kwa moyo wako wote.
-
Daudi alimkata kichwa Goliathi kwa upanga (Neno la Mungu ni kama
upanga). Kwa hiyo hakikisha unapoingia vitani una neno la Mungu la
kutosha na unaliweka katika matendo, hata Yesu alipojaribiwa alitumia
Neno la Mungu kwa ufasaha na akamshinda shetani.
-
Mfalme Sauli hakumwacha Daudi arudi nyumbani kwake. Unapokuwa
mshindi, yaani umeleta suluhisho au kufanya jambo la kipekee sehemu
fulan(kanisani, ofisini, idarani, wizarani, ndani ya taasisi nk) lazima
heshima yako itapanda tu, bosi atatamani uwe assistant wake, Daudi
kutoka malishoni mpaka kuishi ikulu si mchezo. Fanya vizuri sehemu
uliyopo ndipo Mungu atakupeleka hatua ya juu zaidi, kuwa mnyenyekevu,
mwenye bidii na mcha Mungu.
Ubarikiwe sana msomaji wangu, yapo Mengi
ya kujifunza lakini kwa sasa tuishie hapa, mweleze na ndugu yako na
rafiki yako habari hizi njema na za kuleta tumaini jipya kwa kizazi
hiki. Haleluuuya
Toa Maoni Hapa Chini