|
Aposlte Darmacy |
JE KUOKOKA MAANA YAKE NINI?
1.Utangulizi
Watu wana mawazo mbali mbali kuhusiana na maana ya kuokoka.
Wengine hufikiri kusali kanisa la walokole ndio kuokoka. Wengine
hufikiri kuacha tabia fulani fulani mbaya kama ulevi, uzinzi n.k ndiyo
kuokoka. Utasikia mtu anamwambia mwenzake, siku hizi umeokoka nini,
mbona hubanduki kanisani? Je kusali sana ni kuokoka? Hebu tuangalie
Mungu anatundisha nini kuhusu maana ya wokovu. Yako mambo matatu
yanayofafanua maana ya kuokoka.
2. JAMBO LA KWANZA KUPOKEA MSAMAHA WA MUNGU BAADA YA KUTUBU KWELI.
“Katika yeye huyo (Yesu) kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Efeso 1:7
Wokovu ni kupokea msamaha wa Mungu ulioletwa hapa duniani na Bwana
Yesu. Yesu alikufa msalabani ili kulipa adhabu ya dhambi zako.
“uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuilekea
nuru, na nguvu za shetani na kumwelekea Mungu, kisha wapate msamaha wa
dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa inani iliyo kwangu
mini.” Matendo 26:18
Ili watu waweze kupokea msamaha wa dhambi lazima kwanza
wafumbuliwe macho na kujijua ni wenye dhambi. Badala ya kujitetea na kutetea mtindo mbaya wa maisha walio nao,waazimie kwa moyo wote
kubadili mwelekeo
wa maisha yao. Wawe na mtazamo mpya unaotokana mambo mabaya ya giza
(shetani) na kuelekeza mioyo yao kumtii Mungu. Lazima kukataa wazi wazi
kuzifuata na kuzitumikia nguvu za shetani na kuamua kutumia maisha yao
kumwishia Mungu. Hapa ndipo wanaweza kupata msamaha wa dhambi. Ikiwa
mtu ameamua kubadili mwelekeo wa maisha yake kwa uamuzi wa moyoni
kuachana na mambo ya dhambi na kutumikia au kutegemea nguvu za shetani
basi anapata msamaha wa dhambi zake. Hii ndiyo hatua muhimu
inayomfungulia mtu mlango wa wokovu.
3. HATUA YA PILI NI KUMPOKEA YESU KATIKA MOYO ANAYELETA UZIMA WA MUNGU.
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.”
Yohana 1:12
Msamaha wa Mungu katika maisha ya mtu hufuta dhambi alizofanya huko
nyuma. Lakini ili kuishi maisha ya kimungu lazima asili ya dhambi
ibadilishwe na mtu apate maisha mapya ya Mungu.Kumpokea Yesu kunaleta
uzima wa Mungu ndani yako. Tunashirikiana na Mungu maisha yake. Badala
ya kuishi na nguvu, akili na maisha yetu, tunaishi na uzima wa Mungu.
Uzima huu huitwa uzima wa milele.
“ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa
mwana wake wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima
wa milele.” Yohana 3:16.
Kutokana na upendo wa Mungu katika maisha yetu, alimleta Bwana Yesu
ili tuweze kushiriki uzima wake. Haitoshi kusafishwa dhambi, ili kuishi
kama Mungu anavyotaka lazima tuwe na uzima toka kwa Mungu. Uzima wa
Mungu hutupa asili mpya ya kiMungu inayoshinda dunia na majaribu yake.
Hivyo kuokoka ni kumpokea Yesu katika moyo wako na kuupata uzima wa
Mungu. Na kumpokea Yesu kunaleta uzima wa Mungu aktika maisha yako
4. JAMBO LA NNE KUOKOKA NI KUHAMISHWA TOKA UFALME WA SHETANI NA KUINGIZWA KATIKA UFALME WA MUNGU.
“Naye alituokoa katika nguvu za giza, na akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa mwana wa pendo lake;” wakolosai 1:13
Kuna falme mbili zinazopingana na kila mtu ni raia katika mmojawapo
wa falme hizi. Kuokoka ni kuondolewa katika ufalme wa giza (shetani) na
kuhamishiwa katika ufalme wa Mungu. Unakubali kutubu na kumwelekea Mungu
si tu unasamehe dhambi lakini pia unahamishwa na kuingizwa katika
ufalme wa Bwana Yesu (mwana wa pendo la Mungu) ikiwa umeokoka huna haja
tena na msaada wa shetani katika maisha yako. Hirizi, utabiri na nyota,
mapicha mabaya ya uasherati, mazindiko, ibada za mizimu za kimila pamoja
na zana za ibada huvihitaji tena. Ulipotubu umebadili msimamo na
mwelekeo wako hivyo unayaondoa vitu hivi katika maisha yako maana wewe
si raia wa ufalme wa shetani hata ukautii na kuutumikia. Yesu ndiye
mfalme wako na anawajibika kukulinda.
HITIMISHO
Mambo hayo matatu hapo juu yanaungana pamoja kutupa maana ya kweli ya
kuokoka. Mtu asiyekuwa na hayo hata kama ana sifa ambazo watu na
madhehebu wanazikubali bado hajaokoka. Kuokoka si kuja mbele na kuombewa
juu ya hitaji fulani kama ugonjwa, mahitaji ya maisha n.k Kuokoka ni
kutubu na kupokea msamaha wa dhambi, kumpokea Yesu moyoni anayeleta
uzima wa Mungu na kuhamishwa toka ufalme wa giza hadi ufalme wa Bwana
Yesu.
PIMA UELEWA WAKO.
1. Je kabla ya somo hili wewe ulikuwa unafikiri wokovu maana yake ni nini?
2. Taja mambo matatu ambayo kwa pamoja yanaeleza maana ya kuokoka.
i……………………………………………………………
ii……………………………………………………
iii………………………………………
3. ikiwa mtu hajaamua kuacha maisha ya dhambi anaweza kupata msamaha wa dhambi ikiwa ataungama mambo aliyokesea zamani? (Soma
Matendo 26:18)
4. Soma
Yohana 1:12 je uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu unatoka wapi?
5. Unafikirije, Je mtu akipewa uwezo na Mungu anaweza kuokoka?
CHUKUA HATUA.
1. Ikiwa ulikuwa na vitu hivi mtafute mchungaji au mtu
aliyeokoka, mweleze ukweli kisha mshirikiane kuomba na kuharibu zana
hizi za shetani kama hirizi, mazindiko, picha chafu za mapenzi, vitu vya
ibada za mizimu n.k
2. Mshukuru Mungu kwa kukusamehe dhambi zako, kukupa uzima wake
na kukuhamisha toka ufalme wa shetani akakuingizia katika ufalme wake.
Toa Maoni Hapa Chini