KWA NINI IMANI YA MWANAMKE MKANANAYO ILIONEKANA KUWA KUBWA?
Nakusalimu kwa jina la Bwana, amani na iwe kwako.
Katika Mathayo 15:21-28 maandiko yanasema “Yesu akaondoka
huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke
Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu,
Bwana, mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye
hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema,
Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu,
akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye
akamsujudia, akisema, Bwana, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema
kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana,
lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu
akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama
utakavyo. Akapona binti yaka tangu saa ile”
|
|
Katika zamu hii nimeona vema kujibu swali jingine linalohusu imani
ya mwanamke Mkakanayo. Huyu Mama alikuwa mwenyeji wa nchi ya Kanaani
ambayo ilikuwa karibu na pwani ya Bahari ya kati kutoka Sidoni. Kwa
bahati nzuri Yesu alikuwa amekwenda katika miji ya Tiro na Sidoni
kihuduma, ndipo akakutana na mama huyu ambaye alikuwa anahitaji msaada
wa Yesu apate kumponya bintiye.
Haikuwa jambo rahisi kwa Yesu kuachilia uponyaji uende kwa yule
binti. Lakini baada ya mvutano wa muda mrefu, Yesu alimwambia yule mama ‘Imani yako ni kubwa, na iwe kwako kama utakavyo’. Sasa swali la msingi ninalotaka kujibu ili nasi tupate kujifunza ni hili; kwa
nini imani ya yule mama ilionekana kuwa kubwa kiasi cha kuamua uponyaji
utoke kwa Yesu na kwenda kwa binti yake na kumponya saa ile ile?
|
WWK T.A.G. Forest |
Yafuatayo ni mambo matatu yaliyompelekea Yesu kusema, Mama, imani yako ni kubwa;
Kutokukata tamaa/kuchoka.
Kwa mara ya kwanza yule mama alipoeleza hitaji lake kwa Yesu,
maandiko yanasema Yesu hakujibu neno. Na kwa hiyo tunaweza kusema, Yesu
hakusikiliza wala kujali maombi ya yule mama. Naam mwitikio huu wa Yesu
haukumvunja moyo yule mama akaendelea kuomba tena kwa kupiga kelele ili
Yesu amsaidie.
Aliyapuuza/hakujali maneno ya wanafunzi na wale walifuatana na Yesu.
Kwa kadri yule mama alivyooendelea kumsihi Yesu amponye mwanaye,
ilifika mahali wanafunzi wa Yesu waliona anapiga kelele. Hivyo wakamsihi
Yesu amfukuze ili asiendelee kuwapigia kelele. Sijui kama unaliona
jambo hili kwa upana wake. Huyu mama ana hitaji katika nyumba yake,
anajieleza kwa Yesu, Yesu ana nyamaza, kama vile haitoshi Wanafunzi wa
Yesu wanasema anapiga kelele. Sasa kilichomsaidia yule mama ni kupuuzia
kauli zote zenye kumvunja moyo, yeye alitaka kusikia kutoka kwa Yesu na
si wanadamu. Kwa hiyo hakuruhusu maneno yao yamvunje moyo/yaweke mpaka
kwa kile anachoamini.
Alikuwa na ufahamu wa masuala ya kiroho(imani).
Ukweli huu tunaupata baada ya kuona majibu ya huyu mama pale, Yesu,
alipomwambia; kwanza hakutumwa kwa watu wa taifa (kabila) lake na pili
kumponya bintiye ni sawa na kuwatupia mbwa chakula cha watoto. Katika
hali ya kibinadamu majibu ya Yesu na wanafunzi wake kwa huyu mama,
yalitosha kumfanya huyu mama kukata tamaa na ikibidi kumtukana Yesu na
wanafunzi wake pia. Lakini mwanamke huyu wa ajabu hakufanya hivyo.
Ile kuendelea kuomba kwa unyenyekevu kwa Bwana amponye bintiye na pia
kujibu kwamba hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao,
ilidhihirisha kwamba ni lazima huyu mama, ingawa alikuwa Mkaanani kuna
namna alikuwa ana ufahamu wa mambo ya imani katika Kristo (neno la
Mungu). Kwa hiyo hakikumsumbua watu (Yesu) wanasema nini, ndani yake
alikuwa na ufahamu na imani kwamba hakuna jambo la kumshinda Bwana, na
hivyo ndani yake akazidisha uhakika kwamba bintiye atapona tu.
Naam ile kusema hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana
zao, kauli hili ilimfanya Yesu kuachilia uponyaji kwenda kwa binti yake
saa ile ile na ndipo akasema, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo.
Sijui kama umeliona jambo hili mpenzi msomaji, imani ya yule mama ili kuwa kubwa kiasi cha kutenda kwa kadri ya matakwa yake kuhusu binti yake. Ni
imani iliyoje kutoka kwa mwanamke wa pande za Kaanani, mahali ambako
kwa mujibu wa Yesu hapakuwa kipaumbele chake kuwafikia/kuwasaidia. Naam
imani ya huyu mama ilivuka fikra na mipaka hiyo na kumfanya Yesu
kuachilia uponyaji kawa kdari ya matakwa na muda anaotaka yule mama
(Such a wonderful faith).
Tunajifunza nini?
Naam hata leo kuna sababu kubwa tatu zinazofanya watu washindwe
kupokea majibu ya mahitaji yao au yale wanayoamini kwamba Mungu
atawafanyia;
Utasikia mtu anasema huu ni mwaka wa tatu, tano au saba namuomba
Mungu sioni majibu, nimechoka, bora kwenda kwa waganga wa kienyeji au
kuacha wokovu. Haajalishi kwa jinsi ya kibinadamu majibu yako
yamechelewa kwa kiasi gani, usikate tamaa. Si lengo la Yesu kukutesa au
kukuhuzunisha maana, Bwana hapendi kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu
(Maombolezo3:33). Hivyo usikubali kukata tamaa kwa sababu iwayo yote,
mruhusu Yesu akusaidie, usijaribu kutegemea akilia zako. Zidisha imani
yako kwake, atafanya tu, mpendwa.
Kwa mujibu wa Yakobo 3:1-12 Ulimi ni kiungo kidogo lakini chenye
madhara makubwa. Ulimi ni moto, uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo
mauti na hakuna awezaye kuufuga. Kwa huo twamuhimidi Bwana na kwa huo
twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mafano wa Mungu nk. Jambo ninalotaka
kusisitiza hapa ni kwamba usikubali maneno ya kusikia yakakusababishia
ugonjwa wa nafsi yako na hivyo kuharibu imani yako. Kazi ya
kinywa ni kusema, huwezi kuzuia watu wasiseme, ila unaweza kuzuia
wanayosema kama ni mabaya yasitimie kwenye maisha yako. Naam ni kwa
kutumia damu ya Yesu kuyafuta na kwa kutumia neno la Mungu kuumba kile
unachotaka.
Kukosa ufahamu wa neno la Mungu kuhusu imani
Maandiko yanasema neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika
hekima yote… (Wakolosai 3:16). Kwa nini likae kwa wingi? Mwimbaji wa
Zaburi anajibu ni kwa sababu neno la Mungu ni taa ya miguu yetu, mwanga
wa njia zetu(Zab 119:105). Hivyo litakusaidia kushinda vikwazo vya imani
yako, maana kila imani sharti ijaribiwe. Yesu mwenyewe alijaribiwa
alipokuwa jangwani lakini kwa sababu ya ufahamu wa neno la Mungu
alimshinda Shetani. Hakikisha unakuwa na nidhamu ya kujisomea neno la
Mungu kila leo.
Kwa sababu imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, tena
bayana ya yale yasiyoonekana (Waebrania 11:1), tunaweza kusema kwamba
ukubwa wa imani ya huyu Mama ulitokana na uhakika aliokuwa nao kwamba
Yesu atamponya mwanawe licha ya upinzani aliokutana nao kuhusu imani
yake. Si tu kwamba yule mama alikuwa ana amini Yesu atamponya
bintiye, bali yeye alishaona kwa imani kwamba Yesu amemponya mwanawe na
hivyo alikuwa anang’ang’ania utimilifu wa kile alichoona kwa imani. Naam
alikiona alichokiamini, hivyo alikijua anachokiamini, akakipata
alichokiona.
Naam hakikisha unaongeza imani yako kila siku, ili ifikie na kuzidi
ile ya Mwanamke Mkananayo na hivyo iweze kuamua majibu kwa kadri ya
matakwa na muda wako kutoka kwa Yesu.
Mungu akubariki.
Toa Maoni Hapa Chini