Maana ya neno pepo linamaanisha, pepo mbaya, shetani, mwovu, mharibifu na
mwangamizi. Hao ni malaika waliomuasi Mungu wakatupwa duniani. “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake
wakapigana na Yule joka (Shetani), Yule joka naye akapigana nao pamoja na
malaika zake; Nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.
Yule joka akatupwa, Yule mkubwa, Yule wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani,
audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa
pamoja naye.” Ufu 12:7-9.
1. Ili kutoa pepo, kuna mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa:
Ni lazima uwe na nguvu za Roho
Mtakatifu.Tunaweza kujifunza kwa Yesu alivyoweza kutoa pepo kwa uwezo na nguvu
za Roho. Imeandikwa, “…..awaaamuru pepo wachafu kwa
uwezo na nguvu, nao hutoka.” Luka
4:36.
2. Kutoa pepo kwa jina la Yesu. Aliye na amri
na mamlaka ya kutoa pepo ni mkristo ambaye amemwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na
mwokozi wa maisha yake. “Na ishara hizi zitafuatana
na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo……” Math 16:17. Wale ambao bado hawajamwamini Yesu na kuokoka, Si vyema
kujaribu kutoa Pepo kwa sababu hatatoka, vile vile wanaweza kushambuliwa na hao
walio na Pepo, kama wale wana wa Skewa,
Kuhani Mkuu.
“.....wakajaribu kutaja jina la
Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nakuapisha kwa Yesu,
Yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi,
Kuhani Mkuu, walifanya hivyo..... na yule mtu aliye pagawa na pepo wachafu
akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile
hali wa uchi na kujeruhiwa.” Mdo
19:13-16.
3. Kufanya maombi kila siku na wakati
mwingine kufunga. Bila kufanya hivyo haiwezekani kwa neno lolote, ndio maana Yesu alisema “Lakini kwa namna hii haitoki ila
kwa kusali na kufunga.” Mat
17:21.
4. Kutoa pepo kwa imani. Unaweza kujifunza
kwa wale wanafunzi wa Yesu waliposhindwa kumtoa pepo Yule kijana. Walishindwa kwa sababu ya upungufu wa imani.
Wangekuwa na imani wangeweza kumtoa Yule pepo. “Kisha
wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakisema, mbona sisi hatukuweza
kumtoa? Yesu akawaambia kwa sababu ya upungufu wa imani yenu…..” Mat 17:19-20.
5. Kutoa pepo kwa amri na mamlaka. Unaamuru
kwa jina la Yesu atoke naye hutoka. Tunaweza kujifunza kwa Mtume Paulo
alivyomtoa pepo Yule kijakazi, akaamuru kwa kumwambia Yule pepo, “..…nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo mtoke huyu,
Akamtoka saa ile ile.” Mdo 16:18.
6. Makosa yanayofanyika
kwa wale ambao wanakemea pepo, kwa kuwaambia ninakuangamiza kwa damu ya Yesu,
ninakuteketeza kwa moto, au ninakufunga. Kufanya hivyo ni kinyume na mamlaka ya
Mungu aliyowapa watoto wake. Kwa sababu hiyo, Mungu hajatupa mamlaka ya kuwaangamiza,
Kuwateketeza, wala kuwafunga. Bado pepo watakuwepo katika dunia hii kwa sababu
wakati wao wakuhukumiwa na kuteswa haujafika. Ndio maana pepo walipomuona Yesu,
“…..wakasema,Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je!
Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?” Mat 8:23.
7.Wakati wa kumhudumia mwenye pepo si sahihi kuongea na mapepo na kuwaliza
maswali wametoka wapi, nani akawatuma, ni kwa nini wanamtesa huyo mtu. Hatupaswi
kumsikiliza shetani na mapepo yake kwa sababu wao ni waovu na waongo siku zote. “....Asemapo uongo husema yaliyo yake
mwenyewwe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo” Yn 8:44.
Yesu Krsto hakufanya hivyo ambaye ndiye kielelezo chetu katika utumishi,
ijapokuwa alimwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na kuteseka siku nyingi
alimuuliza swali akitaka kujua jina lake, si jina la pepo.Badala yake pepo
waliokuwa wamemtawala yule mtu walijibu wao ni jeshi. “Yesu akamwuliza jina lako nani? Akasema jina
langu ni jeshi; kwa sababu pepo wengi
wamemwingia”. LK 8:30.
Pepo atolewapo hutaka kurudi.
Pepo anapotolewa ndani ya mtu aliyempagawa huondoka na baadae hurudi na
kuangalia kama anaweza kuingia tena.Ikiwa mtu huyo anaishi maisha ya
dhambi huona nyumba ni chafu na kuingia."
Pepo
mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa
kupumzika, aspate. Halafu husema, nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka;
hata akija aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda akachukua
pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa
humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.
Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya". Mt12:43-45.