Mkuu
wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amesema amepanga kupeleka maombi
Umoja wa Mataifa ya kuwasaidia kuanzisha kiwanda cha kusindika nyanya
wilayani humo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo endelevu ya
dunia kipengele cha uondoaji wa umaskini.
By Zainul Mzige
Alisema anaamini katika kukabili
umaskini ni lazima kuwapo na viwanda vinavyowezesha bidhaa ghafi za
wakulima kupata soko na kwa wilaya hiyo kuondoa tatizo la soko la nyanya
kutawezesha wananchi wake kupiga vita umaskini.
Aidha alisema kwamba serikali
imejiandaa vyema kutekeleza malengo hayo ya dunia kutokana na hatua
mbalimbali inazochukua katika kuhakikisha haki na ustawi wa wananchi
wake.
Sanjari na kueleza hatua hizo pia
alitumia nafasi hiyo kukanusha swali la mwandishi wa habari kwamba
serikali ya Tanzania haijawaandaa wananchi kutekeleza malengo hayo.
Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika
la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez na Ofisa wa Mawasiliano na
Ushirikiano NUNV kutoka Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa
Mataifa nchini, Didi Nafisa wakitazama vibao vya malengo ya maendeleo
endelevu (SDGs) walipofika ofisini kwa Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard
Kasesela ajili ya kumuaga kabla ya kuelekea jijini Mbeya.
Mkuu wa wilaya alisema maandalizi yapo
na si kweli kwamba serikali haijafanya maandalizi kwa kuwa moja ya
lkengo katika malengo hayo inazungumzia maandalizi ya utekelezaji.
Alisema serikali inatambua thamani ya
maandalizi katika utekelezaji wa malengo hayo ndiyo maana inashirikiana
bega kwa bega na Umoja wa Mataifa katika kuandaa watu kuelewa malengo
hayo na kuyatekeleza.
“Ili kuondoa umaskini…hatuwezi
kupitisha malengo hayo bila kushirikisha wananchi… suala la
ushirikishaji ni lengo la 17, ni lengo ambalo linataka kila mtu ashiriki
katika maendeleo,” alisema Kasesela ambaye alikumbusha nguzo tano za malengo hayo ili kuyafanikisha.
Alisema pamoja na kuondoa umaskini
malengo hayo yamesimama katika kuhakikisha kwamba watu wanaishi kwa
amani na ustawi, kukiwa na usawa wa kijinsia na kila mtu kunufaika na
hali ya rasilimali na uchumi uliopo.
Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika
la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez akimkabidhi cheti balozi wa
malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard
Kasesela aliposhiriki katika semina ya SDGs iliyofanyika katika Chuo
Kikuu cha Iringa.
Aidha alisema
kitendo cha mabadiliko yanayozungumzwa ya kuondoa umaskini kutoonekana
vijijini kunatokana na ukweli kwamba taifa kwa muda mrefu ilikuwa
inakabiliwa na tatizo la rushwa.
Alisema japo
serikali imekuwa ikipigana na rushwa kubwa, tatizo la vijijini lilikuwa
kukosekana kwa haki kwa wananchi kutokana na rushwa hali iliyokwamisha
maendeleo ya watu binafsi na hata serikali za vijijini.
“Kutokana
na hili unaona mafanikio ya kupiga vita rushwa inasaidia kukabili
changamoto za malengo ya dunia ya kuondoa umaskini na kuweza kuwa na
nchi yenye staha na kujali wananchi wake” alisema Kasesela.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya malengo ya dunia yakifanyiwa kazi kwa namna inavyostahili taifa hili litafika mbali.
“Kufuta
umaskini moja kwa moja ni hatua.. Kufuta umaskini moja kwa
moja…kusimamia haki.. semina zimepungua.. safari za hovyo zimepungua na
sherehe zisizokuwa na tija zimepungua.. lengo la kuhakikisha afya kwa
kila mmoja kwa kuwa na zahanati kila kijiji,” anasema Kasesela ni
sehemu ya kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya tano katika
kufikisha wananchi wake katika ustawi na hivyo kutekeleza malengo ya
dunia.
Mkuu wa
wilaya ya Iringa, Richard Kasesela akitoa maelezo ya namna
atakavyoshirikisha wananchi wake SDGs wanaofika ofisini kwake kupata
huduma mbalimbali kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa
nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez
aliyefika ofisini kwa DC Kasesela kwa ajili ya kumuaga kabla ya kuelekea
jijini Mbeya.
Aliwaambia
waandishi wa habari waliokuwa katika kampeni ya uhamaishaji wa malengo
ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa wilayani Iringa, Mkuu huyo wa
wilaya alisema kwamba taifa hili limepiga hatua kubwa katika utekelezaji
wa malengo ya dunia na kwamba hilo linaanzia vile vile katika elimu kwa
watu wake.
Hata hivyo
alisema la maana zaidi ni kuhakikisha kwamba mtu mmoja mmoja anatekeleza
malengo hayo kuwa ni ya wote na wala si ya serikali pekee.
“Malengo ni yetu sisi sote si ya mtu mmoja ni mimi nitafanya nini kuondoa umaskini na kuondoa njaa” alisema Kasesela huku akitole amfano wa mkoa wenye chakula kingi kama wa Iringa kuwa na tatizo la udumavu.
“Mkoa
wenye chakula na watoto wamedumaa, ulaji mfumo wa ulaji .. sasa lazima
kufundishana watu wale chakula kilichobora…Waweze kula matunda kumi na
nne na mboga kila siku,” Alisema.
Alisema
amefurahishwa sana kwa Umoja wa Mataifa kuendesha kampeni za kubadili
watu fikira kwani wakibadilika utekelezaji wa malengo hayo utakuwa
mwepesi zaidi.
Mkuu wa
wilaya ya Iringa, Richard Kasesela katika picha ya pamoja na Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika
la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez aliyemtembelea ofisini kwake mjini
Iringa.
Huku akiahidi kuwa championi wa Umoja
wa Mataifa katika kuhamaisha utekelezaji wa malengo hayo 17, alisema
moja ya kitu cha kwanza katika kuondoa umaskini ni kuhakikisha kwamba
wakulima wa nyanya wanapata sehemu ya kuuzia nyanya zao badala ya kuoza.
Alisema watauomba Umoja wa Mataifa
kusaidia kujenga kiwanda cha kutengeneza rasilimali za nyanya kama
walivyowasaidia watu wa Simiyu wa kuanzisha kiwanda chaki na maziwa.
Amesema kuwepo kwa kiwanda kutasaidia
sana kuwa na soko la uhakika na kwamba wananchi umaskini wao utapigwa
vita kwa namna inayofaa zaidi.
credit to
Zainul Mzige
Operations Manager @ Mo Blog