Upo uhusiano mkubwa sana kati ya mafanikio na hali yako
ya kiroho. Binadamu anasehemu kuu mbili ambazo zinamuunda, sehemu hizo ni utu
wa ndani na utu wa nje. Utu wa nje ni miili yetu na utu wa ndani ni roho zetu. Mambo
mengi ambayo hutokea nje ni matokeo ya utu wa ndani. Hivyo utu wa ndani (roho)
ni sehemu muhimu sana kuamua nini kwa nje tufanye.
Hakuna jambo lolote linalofanyika nje, bila kuongozwa na
utu wa ndani. Ndani yako ndiko kunakotoka mawazo, fikra, mtizamo na hisia ambazo
kwa pamoja huamua tuyatendayo kwa nje. Utu wetu wa ndani unahitaji kulindwa
sana ili usisababishe madhara yoyote kwa utu wa nje.
Utu wetu wa nje unaweza kulishwa na ukaonekana kwenye
hali njema ya kiafya lakini ndani yetu tumeumbwa ili kujiunganisha na Mungu
baba ili kuwa katika hali bora. Kudhibiti na kuimarisha afya yetu ya kiroho ni
suala la lazima ili kuwa kwenye hali njema.
Kutokujiunganisha na Mungu huleta athari kubwa sana katika mafanikio
yetu katika maisha, kuna wakati tumekuwa tukitenda mambo mabaya kiasi cha
kutuumiza ndani yetu hadi kupelekea kujisikia vibaya, hii inatokana na ukweli
kwamba roho zetu zinamwitaji Mungu ili kujiendesha. Roho zetu zinahitaji mambo matakatifu
ili ziwe na afya bora.
Hivyo hali bora ya kiroho huruhusu mafanikio mema,
mafanikio yadumuyo kiroho na kimwili. Ni bahati mbaya sana wengi huchukulia
mafanikio kwa dhana hasi, huchukulia mafanikio ni kuwa na pesa nyingi, kitu
ambacho si sahihi. Mafanikio hayaelezeki kwa kipimo cha pesa nyingi japo kuwa na
pesa huambatana na mtu mwenye Mafanikio. Utajiri wa pesa ni kasehemu kadogo
sana katika mafanikio.
Mafanikio yanapaswa kuelezeka kwa kuangalia ni kwa namna
gani mwanadamu ametekeleza kusudi la maisha yake. Kusudi la uumbwaji wako na
Mwenyezi Mungu, Mfano kama wewe uliumbwa kuwa mwaimbaji, je ni kwa kiwango gani
umeweza kutimiza kusudi hilo kwa kiwango cha uwezo uliopewa na Mungu? Hicho ndicho
kipimo sahihi cha maanikio, fedha, Mali, Utajiri hutokea kama matokeo ya
kutimiza kusudi hilo.
Lakini kupata tu pesa nyingi sio mafanikio, na hata kama
ni mafanikio kwa mtazamo mmoja basi ni mafanikio mabaya, kama pesa hizo
zimepatika kinyume na tafsiri ya mafanikio niliyoitoa. Mafanikio mazuri
hukufanya kuwa mwenye furaha kubwa, amani ya roho, utoshelevu na Kuridhika. Na kiu
kuu ya mafanikio mazuri ni kuona wengine wanasaidika kutokana na mafanikio hayo.
Sasa ili uweze kufikia Mafanikio mazuri ninayokusudia
kuyazungumzia leo, ni lazima mafanikio hayo yapaliliwe njia yake na mahusiano
mazuri na Mungu. Samaki ili aweze kuishi ni lazima abaki kwenye maji lakini kwa
uumbwaji wetu ili kufanikisha njia zetu ni lazima kujiunganisha na Mwenyezi
Mungu ambaye ndiyo Muumbaji wetu.
Kadhalika ili ufanikiwe lazima uwe na hali tulivu ya
ndani, yaani lazima mawazo na fikra zako kuwa chanya. Kuwa na hali chanya ya ndani
ni lazima uzuie mdomo wako kusema maneno mabovu, maneno yasio matakatifu
huaribu kabisa mawazo na fikra zetu, na kadhalika kinywa huumba.
Pia lazima uzuie macho na masikio yako kusikia mambo
mabaya, kwani kupitia milango hiyo tunaweza kuharibu kabisa mtizamo wetu wa
ndani hivyo kuathiri matendo yetu. Au wakati wingine huaribu uwezo wetu wa utu
wa ndani kutenda kazi. Kuharibika kwa hali ya utu wetu wa ndani tegemea kuharibika
kwa hali ya utu wa nje.
Ni vyema ukatambua kuna mafanikio katika utajiri wa pesa
na mali lakini unaotesa sana. Sasa kuna faida gani kuwa na mapesa, majumba,
magari na mali nyingi lakini huna furaha wala amani ya vitu hivyo? Sikia acha
kutafuta utajiri wa namna hiyo kwa sababu hautokufikisha popote zaidi ya kukuua
na shinikizo la damu, vidonda vya tumbo, mstuko au msongo wa mawazo.
Tengeneza mahusiano mema na Mungu wako kwa sababu hiyo
ndiyo kiu ya utu wako wa ndani. Amani na furaha ya ndani huachilia nguvu ya
utendaji kwa kile unachokifanya mpaka ufanikiwe. Amani na Furaha hiyo ni
matokeo ya kuwa katika hali nzuri kiroho. Tafuta mafanikio yaletwayo na Mungu
na si ya mapenzi ya wanadamu.
Hakikisha kila kukicha unaianza siku yako kwa sala kadhaa
za kumshukuru Mungu kwa siku mpya, na kukabidhisha shughuli zote za siku
zisimamiwe na Mungu. Kwa kufanya hivyo utakuwa unaufanya utu wako wa ndani kuwa
na amani na furaha itakayokusaidia kupata chochote ukitakacho.
Fanya matendo ya upendo kwa wengine, kupitia matendo hayo
unavuta nguvu ya furaha na amani ndani yako.
Jiwekee malengo ya muda mrefu ya kiroho. Ni muhimu kuweka
malengo kuhusu hali yako ya kiroho. Mfano unaweza kusema “nitahakikisha maneno
yote nitakayo kuwa nayasema ni lazima yawe matakatifu”, au “nitaanza kwenda
kanisani au msikitini na kutoa sadaka”, au “nitafanya toba kila mara
nakadhalika”.
Acha kutenda dhambi, mafanikio hayapendi mtu mzinzi,
mlevi, msema uongo, mnafiki, msengenyaji, malaya, mvuta sigari, mwizi na tabia
kama hizo. Utendaji wa dhambi huaribu kabisa mahusiano yako na Mungu wako, na
ukiaribu mahusiano hayo unajenga kikazo cha kukufikisha unakotaka.
Badilika na anza kushughulikia afya yako ya kiroho ili
upate mafanikio mazuri na yadumuyo.
credit
Ni mimi rafiki
yako,
Alex Mushi,
alexmushi@rocketmail.com