ASKOFU mkuu wa Kanisa la Assemblies Of
God Tanzania (TAG) Dk. Barnabas Mtokambali, amewataka waumini na watumishi wa
kanisa hilo kutumia kituo cha Redio Ushindi kueneza injili.
Kauli hiyo ilitolewa jana wakati wa
kuwekwa Wakfu kwa kituo cha Redio cha Ushindi kinachomilikiwa na TAG kilichopo
Isyesye Jiji na Mkoa wa katika hafla iliyofanyika katika Studio za redio hiyo
ambapo Askofu huyo aliwakilishwa na Makamu wake Dk. Magnus Mhiche.
Akizungumza kwa niaba ya Askofu Mkuu,
Dk. Mhiche alisema kituo cha REDIO Ushindi ni kama chombo ambacho wachungaji
wanaweza kukitumia kuvuna waumini na kueneza injili kirahisi kuliko kutembea
kwa mguu kuwafuata waumini.
Alisema redio huwafikia watu wengi zaidi
bila kujali mazingira walipo hivyo ni kama kanisa linalotembea ambalo linaweza
kusaidia harakati na mkakati wa kanisa wa kuwavuta waumini wengi hatimaye
kuongeza idadi ya wafuasi wa kanisa la TAG tofauti na ilivyo sasa.
Aidha aliwataka wafanyabiashara na watu
mbali mbali kutumia kituo hicho kutoa matangazo ya biashara zao pamoja na
huduma ili kuendelea kuunga mkono huduma zinazotolewa na redio hiyo ili iweze
kujiendesha na kuendelea kuwepo.
Hata hivyo Askofu huyo aliwaagiza
wasimamizi wa Redio hiyo kutopokea matangazo yasiyokuwa na maadili ya kidini
kwa madai ya kujali fedha kuliko kuangalia maudhui ya tangazo lenyewe kama
linakiuka miiko ya kanisa.
“ Nitumie nafasi hii kuwaagiza
wasimamizi wa redio sio kila tangazo linatakiwa kupokelewa hapa angalieni
maadili matangazo ya madawa ya kienyeji au pombe hayatakiwi ni bora tukakosa
fedha kabisa” alisisitiza Askofu huyo.
Kwa upande wake Meneja wa Redio hiyo,
Mathew Sasali, alisema kituo hicho kilifunguliwa Juni 1, 2011 hivyo hadi
kuwekwa wakfu kinatimiza miaka 3 na sherehe hizo ni sambamba na maadhimisho ya
miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa la TAG nchini Tanzania.
Aidha katika Risala ya Kituo hicho
iliyosomwa na Mhariri Mkuu wa Redio Ushindi, Robin Ulikaye, ilisema baadhi ya
mafanikio waliyoyapata ni pamoja na kuongeza idadi ya wasikilizaji, kueneza
injili kupitia Redio pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watumishi kutoka 6 hadi
13 sasa.
Source; Mbeya yetu
JOSEPH MWAISANGO
MWANDISHI MKUU
j.mwaisango@tonemg.com
+255 754 374408
|